Chan kumlipa mgunduzi wa kinga ya corona wakati Idadi ya vifo ikifikia 1000

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jackie Chan

Mkongwe wa filamu nchini China Jackie Chan ametangaza rasmi kupitia mtandao wa Weibo kuwa atatoa fedha kwa ajili ya mtu yoyote atakayegundua kinga ya ugonjwa wa corona.

Chan ameweka wazi kiu yake ya kutaka kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Corona kwa kutangaza kutoa Zaidi ya dola za kimarekani 140000 kwa mtu ama kikundi kitakacho fanikisha kugundua kinga dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Idadi ya watu waliofariki kutokana na maambukizi ya virusi vipya vya Corona imeongezeka na kufikia 1000 na tayari shirika la afya duniani WHO limeutangaza ugonjwa huo kuwa janga la kimataifa.

Virusi vya corona ni hatari kiasi gani?

Watu zaidi ya 75,000 wanaweza kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, katika mji wa Wuhan, wataalamu wameeleza.

Ingawa makadirio ya chuo kikuu cha Hong Kong yanasema kuwa inawezekana kuwa idadi ikawa kubwa zaidi ya takwimu zinazotajwa rasmi.

Ripoti zinasema kuwa kuna watu ambao walifariki wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza tu, jarida la afya la Lancet linasema kuwa wagonjwa wengi walikufa bila kufahamika kile kilichowauwa.

Ripoti imebaini kuwa wagonjwa 99 walihudumiwa katika hospitali ya Jinyintan huko Wuhan , 40 kati yao walikuwa na magonjwa ya muda mrefu kama magonjwa ya moyo au presha, wengine 12 walikuwa wana kisukari.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jackie Chan kutoa fedha kwa mgunduzi kinga ya Corona

Zuio la watu kusafiri linasaidia?

Maafisa wa afya wameshauri kuhusu zuio hilo.

"Katazo la watu kusafiri linasababisha watu kuingia kwenye matatizo zaidi, kwa sababu watu wanakosa taarifa, usambazaji wa madawa unakuwa duni, uchumi unashuka na hata watu wanatafuta njia ambaozo si rasmi kuondoka katika eneo lililoathirika, mkuu wa shirika la afya alisema siku ya ijumaa.

WHO alishauri kuwa watu wanapaswa kupimwa wakiwa mpakani wakati wanasafiri.

Kwa sababu hatua ya kufunga mipaka inafanya watu kutumia njia za panya kutoka eneo moja kwenda lingine.

China imekosolewa kwa zuio hilo la watu kusafiri.

Hali ya maambukizi hivi sasa ipoje?

Ingawa virusi vimesambaa mpaka nje ya China, kukiwa na ripoti ya maambukizi kwenye mataifa 25, mpaka sasa kumeripotiwa vifo viwili nje ya China- mtu mmoja Hong Kong na mtu mmoja Ufilipino.

Shirika la afya duniani, WHO limetangaza mlipuko wa virusi vya corona kuwa janga la kiafya, likisema ikiwa fedha hazitaelekezwa kupambana na mlipuko, mataifa yatajutia hilo baadae.

Ingawa takwimu rasmi nchini zinasema kuna maambukizi 31,000, baadhi ya wanasayansi wamekisia kuwa idadi inaweza kuwa mara 10 zaidi, kwa kuwa wengi wao huonyesha dalili polepole, na hawapati matibabu, na hivyo kuwaambukiza wengine.

Mada zinazohusiana