Coronavirus: Ongezeko kubwa la vifo na maambukizi jimboni Hubei, China lagharimu ajira za maafisa wa juu

WHO imesema itachukua muda kupatikana chanjo ya kuzuia maambukizi Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption WHO imesema itachukua muda kupatikana chanjo ya kuzuia maambukizi

Vifo 242 kutokana na maambukizi ya virusi vya corona vimerekodiwa katika jimbo la Hubei siku ya Jumatano-mlipuko mbaya kuwahi kutokea

Pia kulikuwa na ongezeko kubwa la maambukizi, watu 14,840 waligundulika na virusi.

China imewafuta kazi maafisa wa juu wawili mjini Hubei saa kadhaa baada ya idadi mpya kutangazwa.

Mpaka ongezeko la Jumatano, idadi ya watu waliobainika kuwa na maambukizi Hubei-ambako mlipuko ulianzia ilikua imetulia

Lakini maambukizi mapya na vifo katika eneo hilo imefanya idadi ya vifo kufikia 1,350 na maambukizi ya watu karibu 60,000 kwa ujumla.

China imekuwa ikishutumiwa kutoweka wazi uhalisia wa ukubwa wa tatizo hilo hapo awali, anasema mwandishi wa BBC Hong Kong Nick Beake.

Profesa David Heymann, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka Chuo cha madawa jijini London amesema: '' Kilichotokea nchini China ni kuwa wamebadili mantiki kuhusu maana ya ugonjwa, sasa wanawachukua watu wenye viashiria vichache.

''Vifo vinatisha, kuna ongezeko la vifo limeripotiwa, lakini ukitazama kwa ujumla, idadi ya vifo na maambukizi bado yao juu, kama vifo vinavyotokana na mafua.''

Haki miliki ya picha Empics
Image caption Kwa ujumla jimbo la Hubei lina maambukizi ya watu 48,206 yaliyothibitishwa.

Katika hatua nyingine, nafasi ya Katibu wa chama cha kikomyunisti Hubei, Jiang Chaoliang, imechukuliwa na mkuu wa chama katika jimbo la Shanghai Ying Yong kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

Mkuu wa chama katika mji mkuu Wuhan pia amevuliwa majukumu yake.

Ni mabadiliko ya kwanza makubwa kufanyika yakiwahusisha maafisa wa chama jimboni Hubei tangu kutokea kwa mlipuko huo

Mapema wiki hii, idadi kubwa ya maafisa wa afya waliondolewa kazini.

Njia gani mpya ya utambuzi iliotumika?

Jimbo ambalo linachukua zaidi ya 80% ya maambukizi nchini China - sasa linajumuisha "visa vilivyogunduliwa kliniki" katika idadi ya visa vilivyothibitishwa.

Hii inamaanisha ni pamoja na zile zinazoonesha dalili, na kuwa na skani ya CT inayoonesha mapafu yaliyoathirika, badala ya kutegemea tu vipimo vya nucleic acid.

Kati ya vifo vipya 242 mjini Wuhan, 135 ni vile vilivyotambulika kwa vipimo vya kliniki.

Hii ina maanisha kuwa, hata bila njia mpya, idadi ya vifo Hubei siku ya Jumatano ilikuwa 107, ikiwa ni idadi kubwa kwa jimbo hilo.

Kwa ujumla jimbo la Hubei lina maambukizi ya watu 48,206 yaliyothibitishwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii