Diane Gashumba: Ni waziri wa tatu kujiuzulu nchini Rwanda

Dkt. Diane Gashumba: Ni waziri wa tatu kujiuzulu nchini Rwanda Haki miliki ya picha CYRIL NDEGEYA
Image caption Dkt. Diane Gashumba: Ni waziri wa tatu kujiuzulu nchini Rwanda

Waziri wa Afya nchini Rwanda Dkt. Diane Gashumba amejiuzulu kulingana na afisi ya waziri mkuu nchini humo.

Katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa Twitter, afisi hiyo imesema kwamba kujiuzulu kwake kunatokana na makosa ya kawaida na mapungufu yake ya uongozi.

Hatahivyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu sababu zilizomlazimu kujiuzulu.

Dr Gashumba ambaye kazi yake inashirikisha kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola kuingia nchini Rwanda kutoka taifa jirani la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekuwa afisini tangu mwezi Oktoba 2016.

Kujiuzulu kwake kunajiri wiki moja tu baada ya mawaziri wengine wawili kutangaza kujiuzulu.

Evode Uwizeyima, ambaye alikuwa akisimamia maswala ya kisheria alikiri kumpiga mlinzi mmoja. Isaac Munyakazi alijiuzulu kama waziri anayesimamia elimu ya msingi na ile ya upili.

Evode Uwizeyimana alijiuzulu baada ya kumsukuma mlinzi wa kike hadi chini.

Kisa hicho kilichofanyika siku ya Jumatatu iliopita , kilifichuliwa baada ya shahidi mmoja kutuma ujumbe katika twitter.

''Haingepaswa kufanyika kwangu kama kiongozi na afisa wa umma, tayari nilikua nimeomba msamaha kwa kampuni ya walinzi hao na sasa naomba msamaha hadharani na kwa umma'',alisema.

Waziri huyo baadaye alimtembelea mlinzi huyo na kumuomba msamaha kabla ya kupiga picha naye.

Lakini raia wengi wa Rwanda katika mitandao ya kijamii waliendeleza wito wa kumtaka kujiuzulu na ilipofikia siku ya Alhamisi , afisi ya waziri mkuu ilitangaza kuwa bwana Ewiziyimana amejiuzulu.

Katika ujumbe wa twitter afisi hiyo pia ilisema kwamba waziri anayesimamia elimu ya msingi na ile ya upili Issac Munyakazi pia amejiuzulu.

Mada zinazohusiana