Zitto Kabwe: Mahakama yamkuta na kesi ya kujibu kiongozi wa ACT-Wazalendo

Zitto Kabwe

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe amekutwa na kesi ya kujibu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kuyatenda Oktoba 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Hayo yanajiri siku moja tu baada ya Zitto ambaye ni rejea nchini baada ya kumaliza ziara yake katika mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani na Uingereza.

Ziara hiyo imezua gumzo nchini Tanzania hususani baada ya Zitto kubainisha wazi kuiandikia barua Benki ya Dunia kusitisha mkopo wa elimu kwa Tanzania.

Baadhi ya wanansiasa kutoka Chama tawala walitoa kauli za kutishia uhai wa mwanasiasa huyo huku yeye mwenyewe akidai kuwa kumekuwa na mipango ya "kumbambikia kesi ya uhujumu uchumi."

Kesi ya uchochezi

Leo Jumanne Februari 18, Mahakama ya Kisutu chini ya hakimu mwandamizi Huruma Shaidi imemkuta mwanasiasa huyo na kesi ya kujibu.

Zitto sasa anatarajiwa kujitetea kwa siku nne mfululizo mwezi ujao kutoka Machi 17 mpaka 20.

Mashahidi 10 wanatarajiwa kumtetea Zitto kwenye kesi hiyo.

Mashtaka ya Zitto yanatokana na kauli zake za kulitaka jeshi la polisi kutolea maelezo kile alichokiita mauaji ya polisi na raia yaliyotokea kwenye Kijiji cha Mpeta, Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma.

Safari ya ughaibuni

Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jumatatu usiku, Zittoamedai kuwa pamoja na kupewa vitisho lakini bado hana hofu ndio mana maana amerudi nchini.

"Sina hofu na ndio maana nimerudi bila shida yoyote kwa sababu hamna kosa lolote nimefanyana nimetekeleza wajibu wangu kama kiongozi wa kisiasa kama mbunge na sina hofu kabisa, nitaendeea kufanya shughuli zangu kawaida,." amesema na kuongeza: "Ziara ilikuwa na mafanikio makubwa sana na ndio maana watawala wanahangaika na kuendelea na vitisho kwa sababu ya mafanikio ya ziara niliyokuwa nayo."

Katika kikao cha bunge kilichopita spika Job Ndugai alitaja barua ya bwana Kabwe kuwa uhaini mkubwa na kuifananisha na vitendo vilivyopelekea rais Donald Trump kushtakiwa bungeni , makosa anayokana.

Maelezo ya video,

Zitto Kabwe aeleza kwanini anataka Benki ya Dunia isiikopeshe Tanzania kwa sasa

''Yeye Bwana Trump ameshtakiwa kwa sababu alikuwa anakula njama na mataifa ya kigeni ili kuingilia maswala ya ndani ya Marekani . Tuna mbunge ambaye amekuwa akifanya vitendo kama vya bwana Trump - kuna swala la uhani hapo'' , alisema.

Abdallah Bulembo, kutoka chama cha mapinduzi CCM alitoa wito wa kuuawa kwa bwana.

''Kuna mtu mmoja aliyechukua maswala yetu ya ndani na kuyapeleka nje ya taifa , hafai kuruhusiwa kurudi na anafaa kuuawa pale alipo .Uhaini! kile ambacho bwana Zitto Kabwe amekuwa akilifanyia taifa hili ni uhaini''.