Coronavirus: Wezi waliokuwa wamejihami waiba mamia ya karatasi za chooni Hong Kong

Uhitaji wa karatasi za chooni ni mkubwa Hong Kong

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Uhitaji wa karatasi za chooni ni mkubwa Hong Kong

Wezi waliokuwa na silaha Hong Kong wameiba mamia ya karatasi za chooni zenye tahamani ya $130 sawa na £98.

Kwa sasa Hong Kong inakabiliwa na upungufu mkubwa wa karatasi hizo za kwendea chooni kwasababu ya wasiwasi uliopo wakati mlipuko wa virusi vya corona ukiendelea.

Wezi hao waliokuwa na visu walimuibia mwanamume mmoja aliyekuwa anawasilisha karatasi hizo nje ya duka moja, polisi imesema.

Maafisa wa polisi wamewakamata wanaume wawili na kupata baadhi ya bidhaa zilizokuwa zimeibwa, kulingana na vyombo ya habari katika eneo hilo

Wizi huo ulifanyika katika eneo la Mong Kok, mji wa Hong Kong jumatatu asubihi.

Kulingana na taarifa za eneo, wahalifu walimtishia mwanamume wakati anashukisha karatasi hizo ili kuziwasilisha katika duka kubwa la kufanyia manunuzi la Wellcome Supermarket.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Karatasi za chooni

Kulingana na taarifa iliyotolewa karatasi 600 za chooni zimeibwa.

Maduka ya maeneo yamekuwa yakishuhudia foleni ndefu za wateja punde tu bidhaa zinapowasilishwa kwa hofu ya kutokea kwa virusi vya corona ambako kutalazimisha watu kusalia majumbani.

Licha ya kwamba serikali imetoa hakikisho kwamba maeneo ambayo virusi vya corona bado havijatokea, yataendelea kupata huduma zao kama kawaida, wananchi wamekuwa wakinunua bidhaa kwa wingi ili kuzihifadhi.

Bidhaa nyingine za nyumbani kama vile mchele, tambi na vifaa vya kufanya usafi uhitaji wake umeongezeka maradufu.

Barakoa (Maski) na sabuni za kunawa mikono ni baadhi ya bidhaa ambazo kwa sasa ni nadra sana kupatikana wakati watu wanajaribu kujilinda dhidi ya virusi vya corona ambavyo tayari vimesababisha vifo kwa zaidi ya watu 1,700.

Hata hivyo mamlaka imelaumu taarifa za uzushi mitandaoni ambazo zimesababisha foleni za watu madukani na kusema kwamba usambazaji wa bidhaa hizo bado haujaathirika.

Hali kama hiyo pia imeshuhudiwa Singapore ambapo watu wamekuwa wakinunua karatasi hizo kwa wingi tu ambako tayari visa 75 vya corona vimethibitishwa.