Unaweza kuelezea vipi uhalifu kama ubaguzi wa rangi?

Nelson Mandela and FW de Klerk receive Nobel Peace Prize

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Nelson Mandela (kushoto) na FW de Klerk wote wawili wakipokea Tuzo ya Amani ya Nobeli 1993

FW de Klerk mzungu wa mwisho kutawala Afrika Kusini ameomba msamaha kwa kuhoji kuhusu ikiwa ubaguzi wa rangi ni uhalifu dhidi ya binadamu au la lakini hatua hiyo imetonesha kidonda kulingana na mwandishi wa BBC Andrew Harding.

Enzi za wakati wa ukoloni bado ni swala nyeti Afrika Kusini

Msamaha wa bwana de Klerk ulikuwa ni jaribio la kutuliza mjadala ambao umekuwepo kwa wiki mbili baada ya kutoa maoni yake ambayo wengi waliyachukulia kama jaribio la kubadilisha historia na kuonyesha kuwa ubaguzi wa rangi haukuwa kitu kibaya vile.

Katika taarifa iliyotolewa kupitia wakfu wa De Klerk, 83, alionyesha kusikitishwa na hasira, machungu na kuchanganyikiwa ambako huenda kulisababishwa na maoni yake.

Wiki mbili katika mahojiano na kituo cha runinga SABC kinachomilikiwa na serikali, aliyekuwa raisi alisema kwamba hakubaliani na mtangazaji aliyemtaka kuthibitisha kuwa ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi ulikuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mwaka 1992, FW de Klerk alishiriki kampeni ya wazungu pekee kupiga kura ya maoni ili kupata uungwaji mkono wa kufanyika kwa mabadiliko ya kumaliza ubaguzi w rangi

Bwana de Klerk alikubali kwamba ulikuwa uhalifu na kuomba msamaha kwa mchango wake katika hilo, lakini akasisitiza kuwa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini ulisababisha idadi ndogo tu ya vifo na haustahili kulinganishwa na ''mauaji ya kimbari'' au ''uhalifu dhidi ya binadamu".

Awali, Afrika Kusini ilionekana kupuuza maneno yake.

Bwana de Klerk, ambaye alipokea Tuzo ya Amani ya Nobel na Nelson Mandela baada ya kuchangia pakubwa katika majadiliano ya kumaliza ubaguzi wa rangi, ni mtu ambaye siku hizi hana umaarufu sana Afrika Kusini na matamshi yake tatanishi huwa hayatiliwi maanani sana na raia.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Julius Malema aliongoza wabunge wa EFF wakitaka Bwana de Klerk aondolewe bungeni

Lakini hilo lilibadilika Alhamisi iliyopita wakati ambapo Bwana de Klerk, kama aliyewahi kuongoza taifa hilo, alihudhuria kikao cha bunge cha kila mwaka ambapo rais Cyril Ramaphosa hutoa hotuba kwa taifa.

Wabunge wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) walikatiza hotuba ya rais na wakitaka Bwana de Klerk aondolewe bungeni.

"Tuna muuaji humu bungeni," alisema kiongozi wa chama cha EFF Julius Malema. Alisema kwamba Bwana de Klerk ni mtu anayeomba msamaha kwa ubaguzi wa rangi … wakati yeye ni muuaji".

Saa moja na nusu baadae, rais Ramaphosa akafanikiwa kuanza hotuba yake huku msimamo mkali wa chama cha EFF ukilaumiwa vikali na chama tawala cha ANC na vyama vingine vya kisiasa kama wenye kuibua hasira na aibu.

Pia unaweza kusoma:

Kwa mara nyingine tena, ilionekana kana kwamba maneno ya kwamba Bwana de Klerk yalikuwa yamepuuzwa.

Lakini hilo halikuendelea kwa muda mrefu.

Siku zilizofuata baada ya tukio hilo, raia walianza kumkosoa de Klerk kwa kutoa maneno yaliyosababisha ghadhabu kali kote nchi humo na kutonesha vidonda.

Hasira hiyo ilijitokeza hata kwenye mitandao ya kijamii na ajenda zingine za kisiasa kutoka kwa upinzani lakini pia kutokana na jaribio lake la kujaribu kutetea matamshi yake.

Awali, wakfu wake unaosaidia watu ulitoa taarifa kali kuelezea kwanini wanaamini Bwana de Klerk alikuwa sawa na kusisitiza kwamba ubaguzi wa rangi haukuwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Pia taarifa hiyo ilielezea kwamba kuelezea ubaguzi wa rangi kwa namna hiyo ilikuwa ni "propaganda iliyoanzishwa na Muungano wa Sovieti", na kwamba ilikuwa inaonesha historia yenye kuumiza moyo ya Afrika Kusini peupe, kuonyesha wazi uovu na mazuri yaliyotendeka.

Wakfu wa Bwana de Klerk, ulisisitiza kuwa yeye hakuwa na hatia kupitia maonevu na unyanyasaji wa chama cha EFF ambao walisema meneno yenye kuzua chuki na kuita vingozi wao madikteta.

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha,

FW De Klerk, akiwa na Nelson Mandela, 1994, alisaidia pwakubwa katika kumaliza ubaguzi wa rangi

Katika mahojiano na BBC Ijumaa iliyopita, de Klerk alisema matamshi yake kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu yaliendana na Baraza la Usalama wakati huo.

Yalirejelelea ukweli wa kwamba ingawa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ilitangaza ubaguzi wa rangi Afrika Kusini kama uhalifu dhdi ya bnadamu, Marekani na Uingereza ambao wote ni wanachama wa Baraza hilo walipiga kura kupinga kuthibitisha hilo.

Lakini hatua hiyo haiwezi kuzuia hatua ya Umoja wa Mataifa ya kushutumu ubaguzi huo wa rangi na kuanzishwa kwa vikwazo vingi tu dhidi ya Afrika Kusini.

Ubaguzi huo wa rangi pia ulijumuishwa kama uhalifu dhidi ya binadamu katika sheria ya Roma iliyoanzisha Mamakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita

Matamshi ya Bwana de Klerk yazua mshutuko

"Ni jambo lenye kukatisha tamaa na kukosesha matumaini hii leo, kuanza kudai kwamba ubaguzi wa rangi ulikuwa au haujawahi kuwa uhalifu dhidi ya binadamu,'" amesema Philippe Sands, QC, profesa na mtalamu wa sheria za kimataifa

Ili kuweka mambo sawa, mwengine aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, alitangaza kwamba atamtumia Bwana de Klerk nakala ya Umoja wa Mataifa kuhusu mkutano huo, na kushtushwa kwamba mtangulizi wake hakuwa na ufahamu wa hilo.

Baadhi ya watu - hususan lakini sio kwa ukamilifu, wazungu waliopo Afrika Kusini walijibu matamshi ya Bwana de Klerk kwa kutaka watu kusonga mbele na kuweka angalizo kwa mambo ya msingi kama vile kupiga vita ufisadi, umasikini na kufufua uchumi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Watu wapanga foleni ndefu kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia Afrika Kusini 1994

Watu hao hao walisema kwamba mjadala unaoendelea umekusudiwa, na kutumiwa vibaya na chama cha ANC na wengine ili kuondoa angalizo kwa kushindwa kwao kuendeleza nchi na kutupia lawama wazungu walio wachache.

Hakuna shaka kwamba katika miaka ya hivi karibuni, chini ya rais Jacob Zuma, na kwa shinikizo la chama cha EFF, hali ya kisiasa nchini Afrika Kusini imekuwa ya kibaguzi.

Wakulima wazungu na ukiritimba umekuwa ukilaumiwa kwa mabadiliko ya kiuchumi yanayofanyika kwa kasi ndogo.

Aliyekuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance, Helen Zille, mara nyingi amekuwa akionyesha masikito yake juu ya ubaguzi unaoendelea kushuhudiwa na siasa ambako kumekuwa kukisababisha msuguano ndani ya nchi yake.

Lakini kwa wengine ama hata pengine kwa walio wengi matamshi ya Bwana de Klerk yanaonekana kuendeleza dhana ya kwamba wazungu wengi hawajawahi kuwajibika katika kukubali maovu yaliyotendeka nyakati za nyuma.

Pengine hili ni kwasababu ubaguzi wa rangu ulimalizika kupitia majadiliano wala sio ushindi wa jeshi.

"Kwa raia wengi wazungu Afrika Kusini…kuendelea kukanusha madhila ya enzi ya ubaguzi wa rangi," aliandika mtaalamu wa katiba Pierre de Vos. "Wanakataa kukubali kwamba wao au wazazi wao walianzisha mfumo huo ama kwa kukusudia au kwa mbinu za kijanja janja na kunufaika nao."

'De Klerk anastahili kuomba msamaha'

"Cha kusikitisha, wakfu wa FW de Klerk, na tabia ya baadhi ya raia wazungu ya kujaribu kujitetea kutokana na mfumo huo uliokandamiza maisha ya watu weusi kwa ya vizazi kadhaa, yamezua gumzo wakati ambapo wengi wanahoji matunda ya demokrasia na uhuru," ameandika mchambuzi wa siasa Somadoda Fikeni katika Twitter.

"De Klerk alifaidika na mapesa na kujionea fahari katika mjadala unaendelea wakati ambapo anastahili kutubu kila siku," aliandika kupitia Twitter mwanahabari Carol Paton.

Chama cha ANC kilitoa taarifa yake, ikishutumu matamshi ya Bwana de Klerk kama uwongo mtupu ambao unajitokeza wakati wa kujitolea kwao kuendeleza maridhiano na kujenga taifa".

Desomnd Tutu
Getty Images
It is incumbent on former leaders of the white community... to demonstrate the courage... necessary to contribute to societal healing"
Desmond & Leah Tutu Foundation

Punde tu baada ya hilo, wakfu wa Askofu Mkuu Desmond Tutu ulitoa wito kwa wakfu wa De Klerk kufuta taarifa yake.