India: Gumzo la mwanamke anapokuwa kwenye hedhi limerudi tena mitandaoni

A wall painting about menstruation in Guwahati on May 28, 2019

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Hamasisho kuhusu hedhi ambayo imekuwa mwiko kwa miaka mingi nchini India

Gumzo la mwanamke anapokuwa kwenye hedhi limerudi tena mitandaoni.

Wanafunzi wa chuo wanaoishi katika vyumba maalum vya kulala magharibi mwa India jimbo la Gujarat wamelalamika kwamba walilazimika kuvua nguo na kuonesha suruali zao za ndani kwa walimu wao wa kike ili kuhakikisha kwamba hawako kwenye siku zao za hedhi.

Wasichana,68, walitolewa darasani na kupelekwa chooni ambapo waliamriwa wavue nguo zao ili wakaguliwe.

Hilo limetokea katika mji wa Bhuj Jumanne. Wasichana hao ni wanafunzi wanasomea masomo ya shahada ya kwanza katika chuo kikuu cha wasichana cha Shree Sahajanand, yenye kushikilia msimamo mkali wa dini ya Kihindu.

Afisa wa shule anayesimamia vyumba vya kulala alilalamika kwa mkuu wa chuo Jumatatu kwamba baadhi ya wanafunzi walikuwa wanavunja sheria ambayo wanawake walio kwenye hedhi wanatakiwa kufuata.

Kulingana na sheria, wanawake hawaruhusiwi kuingia kwenye hekalu wala jikoni na pia hawaruhusiwi kugusa wanafunzi wengine wakati wakiwa kwenye hedhi zao.

Wakati wa kula chakula, wanafunzi walio kwenye hedhi wanahitajika kukaa mbali na wanafunzi wengine, waoshe vyombo na madarasani wanatarajiwa kuketi kwenye viti vya nyuma.

Chanzo cha picha, BBC Gujarati

Maelezo ya picha,

Wanafunzi wa kike wakikusanyika nje ya chuo cha wasichana cha Shree Sahajanand Girls Institute (SSGI)

Mmoja wa wanafunzi hao, alimwambia mwanahabari wa BBC Prashant Gupta kwamba kwenye vyumba vyao vya kulala kuna sajili ambapo wanahitajika kuweka majina yao wakati wanapokuwa kwenye hedhi na kusaidia mamlaka kuwabaini.

Lakini kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, hakuna hata mwanafunzi mmoja ambaye alikuwa ameweka jina lake kwenye sajili pengine hilo limetokana na yale ambayo wanalazimika kuyapitia punde tu baada ya kufanya hivyo.

Kwahiyo, siku ya Jumatatu afisa anyesimamia vyumba vya kulala alilalamika kwa mkuu wa chuo kikuu kwamba wanafunzi ambao wako kwenye hedhi wanaingia jikoni, wanakaribia hekalu na kutangamana na watu wengine.

Inasemekana kwamba siku iliyofuata, wanafunzi walirushiwa maneno makali na mkuu wa chuo kabla ya kulazimishwa kwenda kuvua nguo kukaguliwa.

Walielezea kile kilichowatokea kama tajriba mbaya zaidi iliyowaacha na mfadhaiko wa akili sawa na mateso ya kiakili.

Wanafunzi wanalia kwa mshutuko

Baba ya mwanafunzi mmoja anasema alipowasili chuoni, binti yake na wengine kadhaa walimkimbilia na kuanza kulia. "wako kwenye mshutuko," alisema.

Alhamisi, kundi la wanafunzi walifanya maandamano katika chuo hicho wakitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa chuo ambao waliwasababishia fedheha.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa chuo hicho alisema inasikitisha kutokea kwa tukio kama hilo na kuongeza kwamba kumetolewa agizo la kufanywa kwa uchunguzi na hatua kuchukuliwa dhidi ya watakaopatikana na makosa.

Hata hivyo, Darshana Dholakia, makamu wa Chansela wa chuo hicho alitupiwa kidole cha lawama wanafunzi.

Alisema kwamba wanafunzi wamevunja sheria na kwamba baadhi yao wameomba msamaha.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi wameiambia BBC kwamba kwa sasa wanapata shinikizo kubwa kutoka kwa mamlaka ya shule kutupilia mbali suala hilo na wasilizungumzie popote.

Ijumaa, mkuu wa jimbo la Gujarat aliagiza uchunguzi ufanywe kuhusiana na kitendo hicho cha aibu na kutaka wanafunzi wajitokeze na kuzungumza bila ya uoga wowote kuhusu kile walichopitia.

Polisi imewasilisha malalamiko.

Unyanyapaa dhidi ya wanawake umesambaa

Hii sio mara ya kwanza wanafunzi wa kike kudhalilishwa kwasababu ya hedhi.

Katika visa kama hivyo, wanafunzi 70 walilazimishwa kuvua nguo miaka mitatu iliyopita katika shule moja kaskazini mwa India na msimamizi wa kike baada ya kuona damu kwenye mlango wa bafu.

Unyanyapaa dhidi ya wanawake kwasababu ya hedhi ni jambo ambalo limeenea sana nchini India, ambapo kwa muda mrefu mwanamke kuwa kwenye hedhi ni mwiko na wakati huwa huchuliwa kuwa wachafu.

Mara nyingi hawajumuishwi katika shughuli za kijamii na kidini, na pia hawaruhusiwi kuingia kwenye mahekali wala jikono.

Pia, wanawake wa mijini waliopata elimu wamekuwa wakipinga vikali desturi hizo. Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kumekuwa na juhudia za kuhakisha kuwa hedhi inachukuliwa kama jambo kawaida tu.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Maandamano katika hekalu la Sabarimala baada ya mahakama kutoa umauzi kwamba wanawake waruhusiwe kuingia hekaluni

Hata hivyo mafanikio katika vita hivyo yamekuwa finyu.

2018, mahakama ya juu zaidi iliagiza hekalu la Sabarimala lifungue milango yake na wanawake wa kila rika waruhusiwe kuingia na kusema kwamba wanawake kukatazwa kuingia kwenye hekalu hilo la kusini mwa Kerala ni ubaguzi wa rangi.

Lakini mwaka uliofuata, mahakimu walikubaliana kupitia tena uamuzi huo baada ya kufanyika kwa maandamano makubwa.

La kushangaza, maandamano hayo yalijumuisha idadi kubw aya wanawake na kuashiria vile uzito wa unyanyapaa dhidi ya hedhi.