Hamas yafanikiwa kudukua simu za wanajeshi wa Israel kupitia 'vipusa'

Mojawapo ya picha feki zilizodaiwa kutumika na Hamas

Chanzo cha picha, IDF

Maelezo ya picha,

Mojawapo ya picha feki zilizodaiwa kutumika na Hamas

Wapiganaji wa Hamas walidukua simu aina ya smartphone za wanajeshi wa Israel kwa kujifanya wanawake , limesema jeshi la Israel.

Msemaji wa wanajeshi alisema wanajeshi hao walitumiwa picha bandia za wasichana wadogo swala lililowavutia na kuwafanya kuzipakua picha hizo bila kujua kwamba zingeweza kudukua simu zao.

Amesema kuwa hatahivyo hakuna habari zozote muhimu zilizodukuliwa kabla ya kashfa hiyo kuzimwa. Hamas ambayo inadhibiti eneo la Gaza na Israel zinachukuliana kama maadui wakubwa.

Ni jaribio la tatu katika miaka ya hivi karibuni lililotekelezwa na Hamas ili kudukua simu za wanajeshi hao wa Israel, lakini pia ni la kiwango cha juu kulingana na luteni kanali Jonathan Conricus.

''Tunaona kwamba wanazidi kuimarika kiteknolojia'' , alisema.

Kanali Conricus alisema wadukuzi walijifanya kuwa wanawake wenye umri mdogo wakizungumza lugha ya Kihebrew, wakidai kuwa wahamiaji ama kuwa na tatizo la kusikia ili kuwashawishi wanajeshi hao.

Baada ya kujenga urafiki, wanawake hao walituma viunganishi ambavyo walisema vitasaidia kubadilishana picha, hatua iliowafanya wanajeshi hao kupakua programu ambazo zinaweza kushambulia simu aina ya smartphone ama hata tarakilishi.

Wanapofungua kiunganishi hicho , programu hiyo huweka kirusi kitakachompatia mdukuzi uwezo wa kuona data ikiwemo eneo , picha na mawasiliano.

Pia inaweza kudhibiti simu hiyo, kwa kuitumia kupiga picha na kurekodi video bila mmiliki wake kugundua.

Kanali Conricus alisema kwamba jeshi la Israel liligundua njama hiyo miezi kadhaa iliopita lakini likaiwacha iendelee chini ya uchunguzi hadi walipozima.

Jeshi la Israel liliwaonya wanajeshi kuhusu umuhimu wa kuwa makini wakati wanapotumia simu za smartphone na kutoa maelezo ya kujaribu kuzima majaribio ya udukuzi.