Mwanamke raia wa Afghanistan aliyefanya mazungumzo ya amani na wanamgambo wa Taliban

Fawzia Koofi akizungumza katika mahojiano mjini Kabul

Chanzo cha picha, AFP/Getty images

Maelezo ya picha,

Fawzia Koofi akizungumza katika mahojiano mjini Kabul

Ndoto ya Fawzia Koofi kuwa daktari alipokuwa mtoto ilizimwa baada ya wanamgambo wa Taliban kudhibiti Afghanistan.

Walimfunga mume wake. Alipata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu akiwa kizuizini na baada ya kuachiwa alifariki. Baadaye Fawzia alikuwa mwanasiasa na wanamgambo wa Taliban walitaka kumuua.

Pamoja na hilo alipata ujasiri wa kuzungumza nao.

''Nilikuwa nawakilisha nchi yangu. Nilikuwa nawawakilisha wanawake wa Afghanistan, '' aliieleza BBC.

Hatishwi

Mwezi Februari mwaka 2019, yeye, pamoja na wanaharakati wa haki za binaadamu, waliingia kwenye chumba cha hoteli jijini Moscow kilichokuwa na wanaume 70.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Asasi za kiraia, wanaharakati na mbunge Fawzia Koofi Afghan

Upande mmoja wa chumba hicho walikaa wanamgambo wa Taliban, wakiwa wamevalia vilemba na ndevu zao zikiwa zinaning'inia.

Kwa upande mwingine, wanawake wengine wawili walikuwa wamekaa miongoni mwa wanasiasa wa Afghanistan na wanaharakati, wote wanaume.

''Sikutishwa na hali ile. Kwangu ilikuwa muhimu kuwa jasiri.''

Koofi alikuwa mmoja kati ya wanawake waliokuwa kwenye ujumbe wa Afghanistan ambao ulifanya awamu nyingi za mazugumzo na Taliban.

Wakati wa mchakato mrefu wa amani, Taliban walikataa kujihusisha moja kwa moja na serikali ya Afghanistan, wakisema hawaitambui ''serikali ya vibaraka mjini Kabul''.

Lakini baada ya mashinikizo kutoka Marekani na Urusi, Taliban ilikubali kuzungumza na ujumbe usio mamlaka ya kiserikali.

Mazungumzo ya Moscow na Doha

Koofi alikuwa sehemu ya ujumbe katika awamu tatu na kukutana na wawakilishi wa Taliban mara mbili mjini Moscow na mara moja mjini Doha.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Fawzia Koofi says she was not afraid while talking to the Taliban

''Nilikuwa ninauheshimu upande mwingine. Niliwaambia kuwa Afghanistan sasa ilikuwa ikiwakilishwa na watu wenye maoni tofauti na kuwa nchi haikuwa ikifungwa na itikadi moja.''

Hayakuwa mazungumzo ya mezani. Hakukuwa na mawazo ya pamoja. Kila mmoja alipewa muda maalumu wa kuzungumza.

''Baadhi ya wajumbe wa Taliban walikuwa wakinitazama. Wachache walinakili. Baadhi walikuwa wakiangalia mahali pengine. Sikuona jambo lolote kuwa la ajabu.''

Aliwafanya Taliban wacheke

Chanzo cha picha, AFP/GettyImages

Maelezo ya picha,

Koofi

''Kwa kuwa upande wetu ulikuwa na wawakilishi wanawake, Nilipendekeza Taliban nao wawalete wanawake kama sehemu ya uwakilishi wao pia. Walicheka ghafla.''

Taliban hawakumpeleka mjumbe yeyote wa kike.

Wakati wa utawala wao mwaka 1996-2001 waliwapiga marufuku wanawake kutembea maeneo ya Umma na kuwakataza kupata elimu na ajira.

Taliban iliweka sheria zao kali za kiislamu na adhabu kali kama kupigwa mawe mpaka kufa na kuchapwa viboko.

Mwanamke hawezi kuwa Rais

Katika kuishi kwake kote nchini Afghanistan, Koofi aliwafahamu watu waliopewa adhabu za namna hiyo na alitaka kuzuia serikali ijayo kurejesha tena vitendo hivyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Koofi akiwa bungeni

Wakati wa zamu yao ya kuzungumza, mjumbe wa Taliban alijibu hoja ya Koofi kuhusu usawa wa wanawake na wanaume.

''Walisema mwanamke anaweza kuwa makamu wa Rais lakini hawezi kuwa rais. Pia alisema wanawake hawawezi kuwa majaji.''

Msimamo wa Taliban ulikuwa hivyo, chini ya sheria za kiislamu, wanawake pekee wanaweza kuwa majaji na wakuu wa nchi. Koofi hakufurahishwa na hilo.

Mtindo wa mazungumzo haukuruhusu majadiliano ya pande mbili: ''Sikukubaliana na hilo lakini sikubishana.''

Mipaka ya Uislamu

Mwezi mmoja baadae, Suhail Shaheen, msemaji wa ofisi ya kisiasa ya Taliban iliyo Qatar, aliiambia BBC idhaa ya Pashto kuwa : '' Tuna nia ya kuwapa wanawake haki zote wanazopaswa kupata kwa mujibu wa dini ya kiislamu. Tunakubali haki yao ya kupata elimu. Hii ni haki iliyowekwa kwa mujibu wa Uislamu.

Chanzo cha picha, Inayatulhaq Yasini

Maelezo ya picha,

Suhail Shaheen, Msemaji wa Taliban katika Ofisi ya Qatar

Uhakika ulikuja na mipaka.

''Wanawake wanaweza kufanya kazi na kupata elimu, lakini kwa mipaka ya sheria za kiislamu na utamaduni wa Afghanistan..'' aliongeza.

Kwa watu kama Koofi, hiki ndicho chanzo cha tatizo. Uislamu una kitabu kitakatifu kimoja, lakini kuna tafsiri nyingi za kithiolojia.

Chanzo cha picha, Media team of Fawzia Koofi

Maelezo ya picha,

Koofi akiwa ofisini kwake

''Nimesikia maoni tofauti kuhusu mafunzo ya dini ya Kiislamu kutoka kwa wanazuoni mbalimbali. Taliban wanafuata tafsiri iliyopitiliza kuhusu Koran.''

Koofi ameona namna sera za Taliban zilivyotekelezwa hapo zamani na kufanyiwa kazi. Kwa mara ya kwanza alimuona mpiganaji wa Taliban mwezi Septemba mwaka 1996.

''Nilikuwa ninasomea tiba ya dawa mjini Kabul wakati Taliban ilipoudhibiti mji. Niliwaona nikiwa ghorofa ya tano. Kulikuwa na mapigano mtaani chini na wanamgambo wakiwa wamebeba silaha.''

Ndoto iliharibiwa

Ndani ya siku kadhaa Taliban walichukua malengo yake ya utotoni alipooneshwa mlango wa kuingia chuoni, lakini ndoto ilizimwa na amri iliyowekwa na wanamgambo.

Alibaki Kabul akiwafundisha lugha ya Kiingereza wasichana walioondoshwa shuleni.

''Kilikuwa kipindi kigumu sana. ikiwa mtu anataka kukukandamiza na kusitisha fursa....iliuma sana.''

Taliban walitoa amri ya wanawake kuvaa mavazi ya kujifunika kuanzia kichwani mpaka miguuni. Hatimaye likawa jambo la lazima wanawake kuvaa buibui au burka.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Women wakiwa wamevaa burka

Vitendo vya kikaidi

''Sikununua burka kwasababu sifikirii kutumia pesa yangu kwa kitu ambacho sikioni kuwa sehemu ya utamaduni wetu.''

Ukaidi huu ulimfanya Koofi ajizuie kutembea ili awe salama.

''Idara ya maadili ilikuwa ikifanya doria mitaani na walikuwa wakiwapiga wanawake ambao hawavai burka.''

Haishangazi, watu walipata ahueni baada ya Taliban kuondoshwa wakati Marekani ilipofanya uvamizi kupambana nao.

''Tulitembea mitaani na kufanya manunuzi bila hofu ya kupigwa na Taliban.''

Baada ya kuangushwa kwa utawala wa Taliban mwaka 2001, alifanya kazi na Umoja wa Mataifa, akiwasaidia watoto wadogo waliokuwa wamesajiliwa jeshini.

Kifo cha mumewe

Kipindi cha mpito kutoka utawala wa Taliban hakikuwa chepesi kwa Koofi. Kipindi hicho mume wake alipoteza maisha baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu alipokuwa amefungwa jela na wanamgambo.

Chanzo cha picha, Media team of Fawzia Koofi

Maelezo ya picha,

Koofi akizungumza na vyombo vya habari

Hata hivyo, wakati wa uchaguzi wa wabunge ulipotangazwa mwaka 2005, aliamua kuingia kwenye kinyang'anyiro.

Baba yake, Abdulrahaman Koofi, alikuwa mbunge kabla ya kuibuka kwa wanamgambo wa Mujahideen, kisha Taliban.

Msingi wa msaada wake mpaka kifo chake akiwa mkononi mwa Mujahideen ulimpa nguvu.

''Heshima aliyoiacha ilinisaidia kushinda kwenye kura. Lakini changamoto muhimu ilikuwa kujenga mazingira ya mimi kufahamika mwenyewe.''

Aliendelea mbele na kuwa naibu spika wa bunge akiwa wa kwanza wakati wa awamu mbili za kuwa mbunge. Wakati akiwa katika ziara Kusini mwa nchi akiwa mbunge, alinusurika kuuawa na Taliban.

Kunusurika shambulio la Taliban

''Mwezi Machi mwaka 2010 nilikwenda katika jimbo Nangarhar kusheherekea siku kuu ya kimataifa ya wanawake. Nikiwa njiani na msafara wangu tulishambuliwa.''

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Fawzia Koofi

Risasi zilikuwa zikifyatuliwa kutoka upande wa pili wa mto na kutoka mlimani.

Koofi na mabinti zake waliokolewa na maafisa wake wa usalama, ambao waliwaondoa kwenye eneo hilo mpaka kwenye eneo la pango la mlimani, ambapo waliondoshwa kuelekea Kabul kwa helikopta.

Kofee ameona namna ambavyo kuangushwa kwa Taliban ambako hakujaleta amani. Kwa hakika ilichukua miaka michache kwa wanamgambo kujiunda tena na kurejea na kusababisha madhara makubwa.

Ripoti ya uchunguzi wa BBC mwaka 2018 ilibaini kuwa 70% ya nchi ya Afghanistan ilikuwa ikitishiwa na Taliban.

Chanzo cha picha, AFP/ Getty images

Maelezo ya picha,

Taliban ina uwezo wa kusababisha madhara makubwa

Haiwezi kuizima Taliban licha ya nguvu zao za kijeshi, Marekani sasa inatafuta la mazungumzo.

Vita nchini Afghanistan vimesababisha pigo kubwa kwa Marekani na washirika.

Zaidi ya wanajeshi 2,400 wa Marekani wameuawa nchini Afghanistan tangu 2001,na zaidi ya wanajeshi 1,100 kutoka nchi nyingine.

Idara ya Ulinzi ya Marekani inasema ilitumia dola bilioni 760 kwa jeshi la Marekani kati ya Oktoba 2001 na Machi 2019.

Makubaliano ya amani

Marekani na Taliban ziko karibu na kufikia mpango wa amani.

"Kila mtu anataka kuwa na amani. Tulizaliwa wakati wa vita na tulikua vitani. Kizazi changu chochote wala watoto wangu hawajui amani inamaanisha nini," anasema Fawzia Koofi.

Chanzo cha picha, Media team of Fawzia Koofi

Maelezo ya picha,

Koofi anasema kufunika uso wake si sehemu ya utamaduni wa Afghanistan

"Ikiwa mchakato wa amani utatoa nguvu zote kwa Taliban basi itakuwa kosa."

Ikiwa kila kitu kitaenda kwa kupanga, makubaliano ya Marekani naTaliban yatasainiwa mwishoni mwa mwezi huu.

Rais wa Marekani, Donald Trump, yuko tayari kumaliza vita virefu zaidi vya Washington na kuwarudisha nyumbani askari 13,000 waliowekwa hapo kabla ya uchaguzi wa baadae mwaka huu.

"Mapigano bado yanaendelea. Tunapaswa kuzingatia hali halisi ya Afghanistan. Changamoto kubwa ni jinsi ya kuvimaliza vita. Je! Tunamaliza kwa amani yenye heshima au kwa vita vingine?" anauliza Koofi.

"Amani inamaanisha uwezo wa kuishi na heshima, haki na uhuru."

Vikosi vya kigeni

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Vikosi vya muungano vimekuwa vikitoa msaada mkubwa kwa majeshi ya Afghanistan

Kuwepo kwa wanajeshi wa kigeni kunawapa askari wa Afghanistan msaada mkubwa . Pia hutuma ujumbe wazi wa kidiplomasia. Tunawahitaji kwa miaka mingine michache," anasema.

Koofi anasema kwamba masuala mengi kuanzia serikali ya siku zijazo yanahitaji kushughulikiwa kabla ya amani kupatikana. Anaangazia kupona kwa demokrasia na haki za wanawake.

"Hakuna mbadala wa demokrasia. Ni kwa demokrasia tu [kila mtu] atasema."

Afghanistan ni kati ya nchi masikini zaidi ulimwenguni. Kielelezo cha hivi karibuni cha Umoja wa Mataifa cha Maendeleo ya Binadamu kimeiweka kuwa nchi 170 kati ya 189.

Viwango vya elimu kwa wanawake vinakadiriwa kuwa chini kwa 16%, kulingana na ripoti za nchini humo.

Chanzo cha picha, AFP/Getty images

Maelezo ya picha,

Elimu kwa watoto wa kike ni changamoto nchini Afghanistan

Kuna gharama kubwa ya wanadamu kwa vita hivi vya muda mrefu.

Zaidi ya raia wa Afghanistan milioni moja waliuawa wakati wa vita vilivyohusisha muungano wa Kisovieti

Leo, raia milioni 2.5 wamesajiliwa kama wakimbizi nje ya nchi na wengine milioni mbili ni wakimbizi wa ndani. Wajane wanaokadiriwa kuwa milioni mbili wanajitahidi kupata riziki.

Utafiti wa mapato ya 2016-17 ulionesha kuwa zaidi ya nusu ya idadi ya watu walikuwa wanaishi chini ya kiwango cha umaskini.

Nini kilichobadilika?

''Wanawake wamepoteza sana, Tutapoteza kwa namna gani zaidi? Wanataka tulipe gharama kwa kiasi gani zaidi?'' anauliza Koofi.

Chanzo cha picha, AFP/Getty images

Maelezo ya picha,

Koofi na binti zake

Afghanistan imebadilika sana tangu uwepo wa Taliban.

Koofi anasema binti zake wote wamejiunga na vyuo vikuu vya Kabul. Haki ya kupata habari bila kikwazo kumeathiri tabia zao.

"Hakuna nguvu inayoweza kuzuia binti zangu na wasichana wengine wa rika lao kubaki majumbani mwao. Mtu yeyote anayetaka kutawala nchi lazima azingatie hilo."