Vita vya Syria : Harakati za kijeshi za Uturuki mjini Idlib 'zinasubiri muda tu'

Turkish troops patrol the town of Atareb in Aleppo province, Syria (19 February 2020)

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Uturuki imekwishatuma maelfu ya wanajeshi wake kuimairisha kikosi cha wanajeshi wa uangalizi katika jimbo la Idlib

Rais wa Uturuki amesema kwamba "ni suala la muda tu " kabla ya nchi yake kuanza harakati za kijeshi kuzuwia mashambulio ya jeshi la Syria dhidi ya eneo linalodhibitiwa na upinzani katika jimbo la Idlib.

Recep Tayyip Erdogan ameonya kuwa anaazimia kufanya mabadiliko katika eneo la mpaka na kulifanya kuwa sehemu salama "kwa garama yoyote ile".

Serikali ya Syria na washirika wake Urusi wamekataa madai yake ya kurudisha nyuma majeshi yake hadi kwenye uzio wa eneo la usitishaji mapigano lililoafikiwa mwaka 2018.

Mapigano yamesababisha raia wapatao 900,000 wakiwemo watoto nusu milioni kuyakimbia makazi yao tangu Disemba 1.

Mamia wameuawa katika kipindi hicho, wengi wakiwa ni wahanga wa mashambulio ya wanajeshi wa serikali ya Syria na washirika wao kwa mujibu wa Umoja wa Matifa.

Watoto pia wanakufa kutokana na baridi, akiwemo mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja msichana na mtoto mchanga wa kiume aliyekuwa na miezi saba.

"Uhasama sasa umefikia maeneo yenye msongamano wa watu. Watu wanakimbilia maeneo ya barafu kutafuta usalama ambao umekuwa mgumu zaidi,'' kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa mataifa.

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa mapigano kusitishwa mara moja.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Zaidi ya watu 700,000, mkiwemo watoto 400,000 wamekimbia nyumba zao tangu mwezi Disemba

Idlib ni ngome ya mwisho ya waasi na wapiganaji wa jihadi ambao wamekua wakijaribu kumuondua madarakani rais wa Syria Bashar al-Assad tanga mwaka 2011.

Katika miaka ya hivi karibuni idadi ya watu waliosambaratishwa imeongezeka mara dufu hadi kufikia watu wapatao milioni tatu miongoni mwao watoto milioni moja.

Uturuki, ambayo inaunga mkono upinzani dhidi ya Bwana Assad na inaogopa kupokea wakimbizi wengi kutoka Syria, imepeleka wanajeshi wake katika vituo vya uangalizi mjini Idlib chini ya mkataba na Urusi ambao uliweka eneo lisilokuwa na mapigano- mkataba wa Sochi wa mwaka 2018.

Hata hivyo, imeshindwa kulizuwia jeshi la Syria kuchukua tena maeneo makubwa ya jimbo hilo kwa msaada wa mashambulio ya ndege za Urusi na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.

Mashambulizi ya hivi karibuni ya serikali na hakikisho la kuvuka kwa raia kwenye mpaka wa kuingia Uturuki vimeyachochea jeshi la Uturuki kuanza kujiimarisha katika maeneo yake ndani ya Idlib tangu Januari. Maelfu ya wanajeshi na maelfu ya vifaru vya kijeshi viliwasili tangu wakati huo.

Mapema mwezi huu, baada ya wanajeshi kadhaa wa Uturuki kuuawa katika mashambulio ya makombora ambayo maafisa wa Uturuki walisema yalirushwa na jeshi la Syria, Bwana Erdogan aliiambia serikali kurejea katika mstari wa uangalizi la sivyo wakabiliane na mashambulio ya kijeshi.

Jumanne, msemaji wa rais wa Uturuki alisema katika mazungumzo baina ya wajumbe wa Uturuki na Urusi mjini Moscow bado hajapata "matokeo ya kuridhisha".

Pendekezo la Urusi la "kuchora upya eneo salama halikukubalika na lilikua "halikua swali " kwa Uturuki kupeleka wanajeshi wake katika vituo vya ukaguzi, Ibrahim Kalinalielezea.

Maelezo ya picha,

Ramani inayoonyesha udhibiti wa eneo la kaskazini-magharibi mwa Syria(17 Februari 2020)

Katika hotuba kwa wabunge kutoka chama chake cha AK Party Jumatano, Bwana Erdogan alionya : "Tunaingia katika siku za mwisho kwa utawala wa Syria kusitisha mashambulio yake katika Idlib."

"Tunatoa onyo la mwisho," alisema. " Hatukupata matokeo tuliyoyataka katika mazungumzo yetu na Urusi. Mazungumzo yataendelea, lakini ukweli ni kwamba tuko mbali kufikia madai yetu tuliyoyatoa.

"Uturuki imefanya maandalizo ya kila kitu kutekeleza mipango yake ya harakati za kijeshi. Ninasema kwamba tunaweza kuja wakati wowote ule. Kwa maneno mengine , mashambulio ya Idlib tunangoja muda tu ," rais aliongeza.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Recep Tayyip Erdogan anataka jeshi la Syria kuondoka nyuma ya mstari wa ukaguzi wa Uturuki

Msemaji wa serikali ya Urusi mjini Kremlin alijibu haraka tisho hilo, akisema: "kama tunazungumzia harakati za kijeshi dhidi ya mamlaka halali kisheria za Jamuhuri ya Syria na vikosi vyenye silaha vya Jamuhuri ya Syria hii vitasababisha hali mbaya sana."

Lakini Dmitry Peskov aliongeza kuwa Urusi haitapinga kama jeshi la Uturuki litachukua hatua dhidi ya "makundi ya ugaidi ndani ya Idlib", kulingana na mkataba wa Sochi.

Vikosi vya Uturuki na washirika wao waasi wa Syria tayari wamefanya mashambulio matatu kaskazini mwa Syria tangu mwaka 2016, licha ya kwamba hayakuvilenga moja kwa moja vikosi vinavyoungwa mkono na serikali ya Urusi.

Mwezi Oktoba mwaka jana, walivifurusha vikosi vya wapiganaji wa Kikurdi vinavyoungwa mkono na Marekani kutoka kwenye eneo kati ya miji ya Tal Abyad na Ras al-Ain.

Watu wapatao 300,000 walismbaratishwa na raia 12 wakauawa katika makabiliano, kwa mujibu wa kikundi cha uangalizi.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Nusu ya milioni ya watoto wamesambaratishwa na mashambulio ya serikali

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet alielezea hali ya kutisha kwa kiwango cha mzozo wa kibinadamu katika eneo la Kaskazini-magharibi mwa Syria siku ya Jumanne, akisema kuwa ukatili alioushuhudia ulikua zaidi ya mtu anavyoweza kufikiria na kwamba raia wanaoishi katika mahema wanashambuliwa.

"Familia nzima, baadhi ya wamekimbilia eneo moja la Syria huku wengine wakikimbilia maeneo mengine na hivyo kutengana kwa muongo uliopita na inasikitisha kuwa vita vimekua ni sehemu ya maisha yao," aliwambia maripota Geneva.

Tangu Januari 1, Umoja wa Mataifa unasena umerekodi vifo vya raia 299. Vifo vyote hivyo vilisababishwa na Serikali ya Syria na washirika wake.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Miji inayoshikiliwa na upinzani kama Atareb yanakabiliwa na mashambulizi mazito

Bi Bachelet ametoa wito serikali ya Syria na washirika wake kuruhusu njia za wahudumu wa misaada ili wayafikie maeneo yenye mizozo, na kutoa njia salama kwa raia wanaotoroka mapigano.

Katika taarifa nyingine tofauti Jumatano, ndege ya kwanza ya abiria imesafiri kwa mara ya kwanza kutoka Damascus na Syria imefanya safari yake ya kwanza baada ya miaka minane baina ya mji wa Syria wa Damascus na mji wa pili kwa ukubwa wa Syria wa Allepo.