Coronavirus: Jinsi ugonjwa ulivyothibitisha chuki dhidi ya Wachina ama Sinophobia

Two women wearing protective facemasks stand inside a shopping mall in Bangkok on 5 February 2020.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mashaka dhidi ya wachina yameongezeka toka mlipuko wa virusi ulipoanza, hata barani Asia.

Sammi Yang awali aligundua kuwa kuna kitu hakipo sawa pale alipoenda kuonana na daktari jijini Berlin, Ujerumani.

Hali ilikuwa tofauti punde tu alipokatazwa kuingia ndani ya jengo.

Wagonjwa wengine walikuwa wakiharakishwa kuingia ndani, lakini Bi Yang ambaye ni mpambaji kutoka China ilimbidi asubiri nje na kupambana na baridi kali ya mwezi Januari .

Baada ya muda daktari wake akatoka. Akamweleza: "Haufanyiwi hivi wewe tu..."

"Kisha akasema: 'Haturuhusu wagonjwa wowote raia wa China kwa sasa kutokana na virusi vya Kichina'," Bi Yang ameieleza BBC. "Sikupata hata fursa ya kujieleza kuwa mimi nimzima."

Bi Yan amekuwa nje ya China kwa muda mrefu, lakini hata hilo nalo hakupata muda wa kulisema.

Toka kuibuka kwa virusi hivyo na kuanza kusambaa maeneo tofauti duniani, visa kadhaa vya ubaguzi vimeripotiwa kwa raia wa China ama watu wenye muonekano wa raia wa mataifa Mashariki ya Mbali.

Japo jumuiya ya kimataifa inaonesha huruma kwa China, jamii za Waasia na hususani Wachina ughaibuni wanasema kuwa ubaguzi dhidi yao umeongezeka.

Ubaguzi dhidi ya China na Wachina si kitu kigeni - Sinophobia - ni aina ya ubaguzi ambao umeelezwa kwa kina na umeendelea kwa karne kadhaa.

Lakini kinachoendelea kwa sasa kutokana na mlipuko wa coronavirus unathibitisha kuwa bado dunia ina husiana na China kwa namna ngumu kwa kiasi chake.

'Wachina wachafu, hawajastaarabika'

Milipuko ya virusi inatokea sehemu mbalimbali duniani, lakini muitikio huwa tofauti kulingana na eneo.

Katika maeneo ambayo jamii za Wachina ama Waasia zinaonekana japo kwa uchace kama Ulaya, Marekani na Australia, Sinophobia huchochewa na dhana kuwa Wachina ni wachafu na hawajastaarabika.

Kuitwa "kirusi", mathalani, ni jambo la kawaida kwa Waasia ambao pia hutengwa katika maeneo ya umma.

Ubaguzi huo hufikia hatua ya kuzaa mashambulizi.

Vichwa vya habari vya kibaguzi ikiwemo "Watoto wakichina wabaki nyumbani" vimeonekana kwenye vyombo vya habari Ufaransa na Australia.

Kutokana na taarifa kuwa virusi hivyo vimetokana na soko la kuuza wanyama, na kuwa kuna uwezekano vimewakumba binaadamu kutoka kwa popo kumefanya dhana ya kibaguzi kushamiri kuwa wachina wanakula kila mnyama ama mdudu anayetembea.

Nchini Singapore na Malaysia, maelfu ya watu wamesaini maombi ya mtandaoni ya kuzuia moja kwa moja raia wa China kuingia kwenye nchi hizo - na nchi hizo mbili zimeweka aina fulani ya ugumu kwa raia wa China kuingia.

Nchini Japani baadhi ya watu wanawalaumu Wachina kuwa "magaidi wa kibaiolojia" na dhana hasi kuwa serikali ya Uchina inawaambukiza kwa makusudi wakaazi, hususani Waislamu zimetapakaa nchini Indonesia na kwengineko.

"Katika nchi za Magharibi, China inaonekana kama ipo mbali a ilojitenga, na Sinophobia inazaliwa kwa kutojua ukweli. Lakini kwa nchi za eneo la karibuni ubaguzi unatokana na kuwajua saana wachina" ameeleza Profesa Donald Low, kutoka Hong Kong.

Hata katika maeneo ambayo kuna watu wa asili ya Uchina kama Hong Kong na Singapore, bado kuna ubaguzi, hususani kutokana na uhamiaji wa watu kutoka China Bara na kuingiliwa na serikali ya Beijing.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Ubaguzi katika picha Italia, mchoro huu unasema: Kuna mlipuko wa ujinga...inabidi tujikinge."

'Mshangao na dharau'

Baadhi wanaamini kuibuka upya kwa Sinophobia kunachangiwa zaidi na jinsi Uchina yenyewe, kwa namna iliyoshughulikia mlipuko wa virusi na sera zake nyengine dunianni.

Kwa mujibu wa Profesa Low watu wengi wanaiangalia China kwa "mshangao na dharau".

Baadhi wanaingalia China kwa namna ilivyopambana, "wengi wanastaajabia namna hospitali kubwa ilivyojengwa kwa siku chache tu. Lakini wegine wanaidharau kwa kushindwa kushughulikia vitu kama soko la wanyama, ama kushindwa kuwa wawazi".

Maelezo ya video,

Virusi vya Corona: Hospitali iliyojengwa ndani ya siku 10

"Wachina pia wanataka kupendwa na kuogopwa," anaeleza Profesa Low.

Pia uonekano wa Wachina katika nchi za nje upo juu kutokana na ongezeko la namba ya wanafunzi na watalii katika kila kona ya dunia. Ongezeko hilo limezaa pia ubaguzi katika kipindi hiki cha mlipuko wa coronavirus.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Kukua kwa watalii kutoka China kumefanya raia wa nchi hiyo kuonekana zaidi duniani.

Lakini pia wapinzani wa China wanalaumiwa na baadhi ya wachambuzi kwa kukua kwa Sinophobia.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikiongoza mashambulizi, husussani utawala wa rais Donald Trump anasema Profesa Barry Sautman, mwana soshiolojia kutoka chuo kikuu cha Syansi na Teknolojia cha Hong Kong.

Marekani pia ina historia mbaya na Sinophobia, mwaka 1882 ilipitishwa sheria ya kuwazuia wafanyakazi wa kichina katika machimbo ya dhahabu.