Manusura wa shambulio la tindikali: 'Kuna watu wengi wazuri duniani kuliko wabaya'

  • Na Hailu Sahle
  • BBC Tigrinya
Menbe Aklilu na Atsede iwakiwa hospitali

Chanzo cha picha, Menbere Aklilu

Maelezo ya picha,

Menbere Aklilu alimsaidia Atsede Nguse kupata matibabu nchini Marekani

Mwanamke wa Ethiopia aliyeshambuliwa kwa tindikali na mumewe mwaka 2017 anasema licha ya hali ngumu anayopitia baada ya shambulio hilo ana kila sababu ya kuwashukuru watu waliomsaidia.

"Kuna watu wengi wazuri duniani kuliko watu wabaya," Atsede Nguse aliaambia BBC kwa njia ya simu kutoka makao yake mapya nchini Marekani.

"Nimeguswa na ukarimu na upendo niliopewa na watu baada ya tukio hilo," mama huyo wa miaka 29 amesema.

Tindikali aliyomwagiwa ilimchoma vibaya na kumharibu uso na na sehemu zingine za mwili wake.

Hakuweza kupata matibabu katika hospitali za Ethiopia na hakuwa na uwezo wa kifedha wa kutafuta matibabu mahali kwengine kokote.

Chanzo cha picha, Menbere Aklilu/Facebook

Maelezo ya picha,

Uso wa Atsede uliungua vibaya kwa tindikali iliyomuathiri pia kifua, mikono na mguu wake mmoja

Waliposikia masaibu yaliyomkuta, marafiki zake na wahisani walichangisha fedha za kugharamia matibabu yake nchini Thailand.

Lakini fedha hizo ziliisha kabla ya Bi Atsede kukamilisha matibabu yake hali iliyomfanya kurudi nyumbani akiwa hajapona.

Kwa mara ya pili, mtu mwingine akajitokeza kumsaidia.

'Moyo wangu uliguswa'

Menbere Aklilu, mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake nchini Ethiopia ambaye anaishi Marekani, alisoma kuhusu kisa cha Bi Atsede katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Yeye mwenyewe kama muathirika wa unyanyasaji wa kinyumbani, anasema alitaka kumsaidia.

"Niliposoma kisa chake, nilisikitika sana sawa na watu wengine. Lakini sikutaka yaishie hapo, nilifahamu kuwa ni mama, nikajiuliza: 'Hali ingelikuaje ikiwa mwanangu angelikutwa katika hali ya mtoto wake kwa sasa?'

"Hili liliugusa sana moyo wangu."

Shirika la kimataifa la kuwahudumia manusura wa mashambulio ya tindikali ambalo sio la kiserikali na lenye makao yake nchini Uingereza linakadiria kuwa kati ya wanawake 50 na 75 hushambuliwa kwa tindikali nchini Ethiopia kila mwaka.

Idadi hiyo inaashiria jinsi mzozo wa kinyumbani kiwango ulivyofikia viwango hatari.

Mwaka 2016 ripoti ya serikali ilibainisha kuwa zaidi ya theluthi moja ya wanawake ambao wako katika mahusiano au walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi waliwahi kudhulumiwa kwa njia moja au nyingine kimwili, kingongo au kuhisia mikononi mwa wapenzi wao.

Shambulio dhidi ya Bi Atsede linaweza kutumiwa kama mfano wa kuelezea hali ni mbaya kwa kiasi gani.

Onyo la majirani

Mume wake, aliyemuoa mwaka 2012, angelimpiga wakitofautiana kitu kidogo.

"Majirani zetu walikuwa na hofu, na walikuwa wakinionya kuwa siku moja huenda akaniua. Licha ya hayo yote, niliendelea kuishi naye kwa maslahi ya mtoto wangu. Sikutaka aishi bila malezi ya baba yake, kama nilivyosema."

Chanzo cha picha, Menbere Aklilu/Facebook

Maelezo ya picha,

Bi Atsede anasikitika sana jinsi shambulio hilo lilivyomuathiri mtoto wake

Hatimaye, mwaka 2015, baada ya kupigwa vibaya hadi meno yake yakang'oka na uso wake kuvimba aliondoka Gambella, magharibi mwa Ethiopia, na kurudi kwao.

"Baada ya kuenda Adigrat, mama yangu na dada yangu wanaoishi Saudi Arabia walinisaidia kuanzisha biashara ndogo ya kuuza manukato. Kwa kweli nilikua nikiendelea vizuri na maisha."

Lakini mwezi Juni mwaka 2017, mume wake alipata nambari yake ya simu, na kuanza kumpigia simu akijidai yuko nje ya nchi.

"Alikuwa akijifanya kama yuko Saudi Arabia. Lakini nikasikia sauti za watoto wakizungumza kwa lugha yetu ya nyumbani, Tigrinya."

Mwezi uliofuata, alikuja hadi nyumbani kwa mama yangu katika kijiji cha Adigrat.

"Alikuwa amejificha [kwenye kichaka karibu na hapo]. Nilimuona akija karibu na mimi. Akanimwagilia kitu kichwani mwangu na mwili wangu mzima," Bi Atsede anakumbuka, jinsi alivyopiga mayowe hadi sauti yake ikapotea.

Tindikali hiyo ilimchoma moja kwa moja.

"Nililia na kuomba msaada. Ndugu zangu walikimbia na kuja kunisaidia. Lakini alitoroka na kuingia kwenyegari lililokuwa likimsubiri."

Bi Atsede aungua vibaya mikono, uso, kifua, masikio, na mguu wake mmoja pia alipoteza uwezo wa kuona.

Hospitali nchini Ethiopia hazikuweza kumsaidia.

Lakini kile kilichomvunja moyo zaidi ni jinsi shambulio hilo lilivyomuathiri mwanawe wa miaka mitano.

"Baada ya shambulio hilo, familia yangu ilimleta mtoto wangu kuja kuniona. Alipoingia katika chumba na kufika mahali nilipokuwa, walimwambia anisalimie, wakisema, 'Ni mama yako.'

"Aliniangalia ana kusema: 'La, huyu sio mama yangu; mama yangu ni mrembo.'"

Baada ya Bi Atsede kurejea nyumbani kutoka Thailand, aliishi katika kituo cha wahanga wa mizozo ya nyumbani mjini Addis Ababa.

Upasuaji wa macho

Bi Menbere alifanikiwa kuwasiliana naye katika kituo hicho, baada ya kupambana na mchakato wa uhamiaji kumwezesha, kumpeleka Marekani.

Alichangisha fedha kwa ushirikiano na marafiki na jamaa zake - na hata watu wasiomjua walijitolea kumsaidia Bi Atsede waliposikia kisa chake.

Mwanaharakati huyo anasema kuwa anamchukulia Bi Atsede kama dada yake: "Tunaishi pamoja. Tunaliwazana kwa kuelezana tuliopitia maishani''

"Nawasidia wanawake kwasababu najipenda. Kila wakati unapomsaidia mtu, makovu yako yanapona. Pia, Naamini naweza kuwapa motisha watu wengine kusaidiana."

Bi Atsede kwa sasa anasaidiwa na wataalamu wa matibabu mjini California ambao wamejitolea kumsaidia aishi maisha ya kawaida.

"Nimefanikiwa kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kopo la jicho. Sikuwa na makopo ya macho.nilikuwa siwezi kufungua na kufunga macho," akisema, anatumai siku moja nitafaniwa kuona tena.

"Pia nimekamilisha somo la watu wasio kuwa na uwezo wa kuona (Braille) na kujifunza kompyuta. Nina ndoto kubwa, na amini nitazifikia ndoto zangu.''

Mume wake hajawahi kupatikana , lakini amehukumiwa kifungo cha maisha jela bila kufika mahakamani .

"Nikipatana naye, Nitamuuliza swali moja tu: 'Mbona umenifanyia hivi?"

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video,

Manusura wa mashambulio ya tindikali Uganda wazungumza