Waziri mkuu wa Lesotho Thomas Thabane kushtakiwa kwa mauaji ya mkewe

Thomas Thabane (katikati) katika siku ya kuapishwa kwake 2017 akiwa na mkewe Maesaiah Thabane, pembeni ni Mfalme Letsie III

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Thomas Thabane (katikati) katika siku ya kuapishwa kwake 2017 akiwa na mkewe Maesaiah Thabane, pembeni ni Mfalme Letsie III

Waziri Mkuu wa Lesotho Thomas Thabane, 80, atashtakiwa kwa mauaji ya mkewe wa kwanza Lipolelo Thabane, Polisi wameeleza.

Bwana Thabane alitangaza kuwa atajiuzulu mwezi Julai kutokana na umri wake, bila kuzungumzia shutuma dhidi yake.

Mkewe wa sasa Maesaiah Thabane tayari ameshtakiwa kwa mauaji.

Atakuwa kiongozi wa kwanza kusini mwa Afrika kushtakiwa kwa mauaji akiwa madarakani, katika kesi ambayo imeishitua nchi hiyo.

Lipelo 58, alipigwa risasi na kufa siku mbili kabla bwana Thabane kuwa waziri mkuu mwaka 2017.

Wakati huo, alieleza kuwa kitendo cha mauaji ya mkewe wa zamani ''hakina maana'' lakini sasa polisi wanamshutumu kuhusika kwenye mauaji hayo.

Chanzo cha picha, The Post

Maelezo ya picha,

Thabane alimuoa Maesaiah mwaka 2017

''Waziri mkuu atashtakiwa kwa mauaji'', Kaimu kamishna wa polisi Paseka Mokete alinukuliwa na shirika la habari la Uingereza, Reuters.

''Polisi wanaandaa miongozo na pengine atashtakiwa kesho,'' aliongeza.

Waziri Mkuu anasemaje?

Thabane alisema kwenye redio ya taifa kuwa amelitumikia taifa kwa ''bidii'' na kuwa atajiuzulu mwishoni mwa mwezi Julai, Reuters imeripoti.

''Nimefanya kazi kwa ajili ya Lesotho. Leo...kwa umri huu, nimepoteza nguvu zangu nyingi,'' alinukuliwa akisema.

Thabane amepewa mpaka siku ya Alhamisi kujiuzulu.

Mauaji yalitokeaje?

Chanzo cha picha, Lesotho Times

Maelezo ya picha,

Lipolelo Thabane

Mkewe wa zamani Lipoleo Thabane alipigwa risasi na kufariki nje ya nyumba yake katika mji mkuu wa Maseru siku mbili kabla ya kuapishwa kuwa waziri mkuu 2017.

Wanandoa hao walikuwa wakikabiliwa na mchakato wa kutalakiana.

Shambulio hilo lilidaiwa kutekelezwa na watu wasiojulikana , lakini stakahabadhi zilizowasilishwa mahakamani hivi karibuni na kamishana wa polisi , Holomo Molibeli zimezua maswali chungu nzima.

Agizo la kumkamata Maesaiah Thabane mwenye umri wa miaka 42 lilitolewa mnamo mwezi Januari baada ya kutoweka.

Alikamatwa katika eneo moja la mpakani na Afrika Kusini siku ya Jumanne baada ya makubaliano kati ya mawakili wake na maafisa wa polisi , alisema msemaji wa polisi Mpiti Mopeli akizungumza na chombo cha habari cha AFP.