'Rwanda ni nchi huru inayojitawala na ambayo ina uwezo wa kuchunguza wa kitu chochote'

Kizito Mihigo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kumekuwa na hisia mseto katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha ghafla cha msanii huyo

Rwanda imepinga shinikizo kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kutaka uchunguzi huru kufanywa kuhusu kifo cha msanii maarufu wa muziki wa kiinjili Kizito Mihigo, ambaye alipatikana akiwa amefariki katika kituo cha polisi Jumatatu asubuhi.

Alifariki siku tatu baaada ya kukamatwa karibu na mpaka wa Burundi, polisi wakimtuhumu kwa jaribio la kutaka kutoroka nchi na kujiunga na la waasi linalopigana dhidi ya serikali ya Rwanda.

Bw. Mihigo alipigwa marufuku kuondoka nchini Rwanda kutokana na mashitaka yaliyopita dhidi yake.

Msemaji wa shirika la upelelezi la Rwanda, Marie Michelle Umuhoza, ameiambia BBC kwamba "Rwanda ni nchi huru inayojitawala na ambayo ina uwezo wa kuchunguza wa kitu chochote".

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch, Amnesty International na Commonwealth Human Rights Initiative yamekuwa yakishinikiza kufanyika kwa uchunguzi huru wa kubaini mazingira yaliyosababisha kifo cha mwanamuziki huyo aliyekuwa na miaka 38- amabaye alizoa umaarufu kutokana na ujumbe wake wa amani na maridhiano.

Siku ya Jumatatu, polisi ya Rwanda ilitangaza kuwa alijitoa uhai akiwa kizuizini.

Afisa wa Human Rights Watch ameiambia BBC kwamba uchunguzi huru utaangalia kamera za siri katika eneo ambalo msanii huyo alikuwa anazuiliwa.

Lakini Umuhoza amesema Rwanda tayari inafanya uchunguzi kuhusu kifo chake.

"Sioni haja ya kufanyika kwa uchunguzi huru, katika nchi huru", alisema, bili kuangazia uchunguzi wao utakamilika lini.

Chanzo cha picha, Kizito Twitter

Maelezo ya picha,

Mwanamuziki maarufu kwa nyimbo za injili nchini Rwanda Kizito Mihigo

Pia amesema kwamba familia ya msanii huyo iko huru kumzika.

Baadhi ya marafiki zake na wanaharakati wa Rwanda wanaoishi nje ya nchi wametilia shaka mazingira ya kifo chake.

Wamesema kwamba mwanamuziki huyo hakutaka kujiunga na kundi la waasi nchini Burundi na kwamba alitaka kwenda Ubelgiji ambapo alikuwa akiishi.

Pia wanaamini kwamba hakujiua katika kituo cha polisi alipokuwa anazuiliwa na kwamba huenda aliuawa.

Muziki wa Kizito ndio chanzo cha matatizo yaliomkumba. Katika wimbo mmoja alipendekeza kwamba kila mtu aliyeuawa katika mauaji ya kimbari ya 1994 anapaswa kukumbukwa awe Mtutsi ama Mhutu.

Wanasema kwamba mamlaka imeliona hilo kama changamoto ya wazi dhidi yake na kwamba mauaji hayo yalitekelezwa na Watutsi.

Wakosoaji wa serikali wanaamini kwamba kutokana na hilo Kizito alilengwa.

Mwanamuziki huyo alikuwa ameanza kuchunguzwa kuhusiana na madai hayo pamoja na kutaka kuwahonga wananchi waliomkamata.

Mwaka uliopita aliachiwa huru kwa msamaha wa rais baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa hatia ya kutaka kumuua rais na kuhamasisha raia kupinga serikali.

Maelezo ya picha,

Mwaka 2015, Bwana Kizito alikutwa na hatia kwa kosa la jaribio la kutaka kumuua Rais Paul Kagame na kuhamasisha vurugu dhidi ya serikali na kufungwa lakini baadae alisamehewa

Kumekuwa na hisia mseto katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha ghafla cha msanii huyo wa muziki wa injili huku baadhi ya watu wakitaka majibu kutoka kwa serikali.

Kizito, aliyekuwa na miaka 38 alipata umaarufu kutokana na nyiimbo zake kama vile 'Inuma' unaomaanisha njiwa na 'Igisobanuri cy'urupfu' ambao unaelezea kifo ni nini.

Lakini baadhi ya watu wanaamini wimbo wake Igisobanuro cy'urupfu, ambayo tafsiri yake ni "maana ya kifo", aliyotoa mwaka 2014 siku kadhaa kabla ya kumbukizi ya 20 ya mauaji ya kimbara ya Rwanda, ndio iliyomtia mashakani- kwa kugusia kile kinachodaiwa kuwa uhalifu uliofanywa na chama tawala cha Rwanda Patriotic Front.

Mihigo, ambaye alikuwa aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 mwaka 2015 kwa kupanda njama ya kupindua serikali, na kuachiliwa baadaye kwa msamaha wa rais Septemba 15 mwaka 2018 pamoja na wafungwa wengine zaidi ya 2,000.