Mazungumzo ya amani: Kagame na Museveni wakubaliana kukabidhiana wahalifu

Kagame na Museveni wakutana mpakani Gatuna
Maelezo ya picha,

Kagame na Museveni wakutana mpakani Gatuna

Mawaziri wa maswala ya kigeni wa Rwanda na Uganda wametia saini makubaliano ya kukabidhiana wahalifu wanaotafutwa na mataifa yote mawili katika mkutano uliofanyika katika mpaka ukisimamiwa na marais wa mataifa hayo mawili.

Mkutano huo uliunga mkono kuachiliwa kwa makumi ya raia waliokuwa wakizuiliwa kutoka pande zote mbili katika kipindi cha wiki chache zilizopita.

Hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili imekuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja na kusababisha mpaka wa Gakuna upande wa Rwanda kufungwa hatua ilioathiri raia na biashara.

Sababu moja ya hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili imekuwa lawama zinazohusiana na maswala ya kiusalama.

Rwanda imeshutumu Uganda kwa kuwahifadhi waasi wanaokabiliana na serikali ya taifa hilo huku Uganda ikimlaumu jirani yake wa kusini kuingilia vikosi vyake vya usalama.

Uganda sasa imekubali kuchunguza na kubaini madai ya Rwanda kwamba waaasi wa Rwanda wamekuwa wakisajili na kufanya mafunzo ndani ya Uganda.

Pia imekubali kuzuia tatizo kama hilo kufanyika tena ndani ya ardhi yake.

Mkutano huo ulikubali kwamba wakati hilo litakapoangaziwa , mkutano mwengine utafanyika katika kipindi cha siku 15 ili kuufungua mpaka huo.

Hali ya wasiwasi kati ya viongozi hao wawili inaonekana kupungua.

Rais Paul Kagame na Yoweri Museveni walionekana wakisaliamana kwa mkono na kutabasamu wakati walipowasili kwa mkutano huo.

Hii ni mara ya nne viongozi hao wawili walikutana kwa mazungumzo yaliosimamiwa na marais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na mwenzake wa Angola.

Uganda na Rwanda zina uhusiano wa karibu , huku idadi kubwa ya raia wakiishi katika mataifa yote mawili.

Rais wa Angola Joao Lourenco na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo pia walikuwepo kusaidia kuweka makubaliano.

Mkutano huo unajiri baada ya serikali ya Rwanda kuwaachilia raia 20 wa Uganda ambao walikamilisha vifungo vyao kuhusu mashtaka mbalimbali ikiwemo kuvuka na kuingia taifa jirani bila kibali.

Wiki hii Uganda pia liwaachilia raia 13 wa Rwanda ambao walikuwa wakizuiliwa kwa makosa ya upelelezi na makosa mengine yanayohusishwa na usalama.