Uchaguzi wa Marekani 2020: Sanders asema hana haja na juhudi za Urusi za kumsaidia kwenye kampeni'

Democratic US presidential candidate Senator Bernie Sanders speaks during a Get Out the Early Vote campaign rally in Santa Ana, California

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bernie Sanders ameionya Urusi "Kaa mbali na uchaguzi wa Marekani"

Anayetarajiwa kupeperusha bendera ya mgombea wa Urais wa Marekani kwa chama cha Democratic Bernie Sanders, ameshutumu taarifa za kwamba Urusi inajaribu kumsaidia katika kampeni, na kuiambia "Kaa mbali na uchaguzi wa Marekani".

Bwana Sanders amesema Ijumaa kwamba maafisa wa Marekani mwezi uliopita walimuarifu kuhusu juhudi za Urusi za kumsaidia katika kampeni.

Akizungumza katika eneo la Bakersfield, California, Bwana Sanders amesema bado haijafahamika vile Urusi imejipanga kuingilia uchaguzi.

Hata hivyo, Sanders, 78, seneta wa jimbo la Vermont alisema anapinga vikali majaribio yoyote ya aina hiyo.

Alimshutumu Rais wa Urusi, Vladimir Putin kama kiongozi wa kiimla muhuni, ambaye serikali yake imekuwa ikitumia propaganda ya intaneti kuhakikisha kwamba nchi hiyo imegawanyika.

"Tuwe wawazi, Urusi inataka kukandamiza demokrasia ya Marekani kwa kutugawanya, tofauti na rais wa sasa, mimi ninapinga vikali nguvu yoyote kutoka nje ambayo inataka kuingilia uchaguzi," Bwana Sanders amesema.

Bwana Sanders, kwa sasa anachukuliwa kama aliye mstari wa mbele katika uchaguzi wa mchujo kwa atakayepeperusha bendera ya chama cha Democrat kwenye kinyang'anyiro cha Urais.

Mtandao wa Facebook umesema haujaona ushahidi wowote unaoonyesha kwamba Urusi inasaidia katika kampeni ya bwana Sanders.

Ijumaa, gazeti la The Washington Post liliandika kwamba rais wa Marekani Donald Trump na wabunge wengine walikuwa wamefahamishwa kuhusu jaribio la Urusi la kumsaidia Bwana Sanders.

Maafisa waandamizi wa ujasusi pia wanaamini kwamba Urusi imekuwa ikitafuta njia za kuingilia uchaguzi utakaofanyika Novemba kwa mtazamo wa kutaka kumsaidia Trump.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Trump alidaiwa kukerwa kuhusu mkutano huo wa maswala ya uchaguzi

Kamati ya masuala ya kijasusi iliarifiwa kwamba Urusi inampendelea Trump katika mkutano wa siri uliofanyika Februari 13.

Rais Trump amezungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nevada Ijumaa, kwamba taarifa za kuwa Urusi inaingilia uchaguzi ni uvumi tu ulioanzishwa na wabunge wa chama cha Democrats.

"Nawaona hao waliotoa taarifa za uwongo, wabunge wa Democrats walisema kwamba Putin anataka kuhakikisha kuwa Trump anachaguliwa tena. Zimeanza tena," Bwana Trump alisema.

Sakata ya Trump na Urusi unahusu nini?

UMashirika ya kijasusi ya Marekani yalifikia hitimisho 2016, kwamba Urusi ilitumia mkakati wa mashambulio ya kimtandao na taarifa za uwongo katika juhudi za kubadilisha mweleko wa uchaguzi dhidi ya mgombea wa Democratic Hillary Clinton.

2017, aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Kijasusi, Robert Mueller, alichaguliwa kama mshauri maalum kuongoza jopo la idara ya sheria ya Marekani kuchunguza ikiwa wasaidizi wa Trump walishirikiana na maafisa wa Urusi wakati wa uchaguzi.

Bwana Mueller aliwasilisha ripoti ya kurasa 448 mwaka 2019, ambayo haikuthibitisha kuwa kampeni ya rais ilishirikiana na Urusi wakati wa uchaguzi, lakini ikaonyesha kwama Trump ameingilia uchunguzi wa jopo hilo.

Bwana Trump alitaja jopo hilo kama njama ya kisiasa na rais wa Urusi Vladimir Putin akakanusha kushirikiana na Marekani kwa namna yoyote ile.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Trump alidaiwa kukerwa kuhusu mkutano huo wa maswala ya uchaguzi

Ijumaa, Kremlin ilikanusha madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani. Msemaji Dmitry Peskov aliwaambia wanahabari kwamba taarifa hizo ni za kutia wasiwasi tu na kujenga dhana fulani isiyo na ukweli wowote, shirika la habari la Reuters limesema.

Hatua ya Urusi kukanusha taarifa hizo inakwenda kinyume na kile kilichosemwa na kaimu wa Shirika la Taifa la Kijasusi, Joseph Maguire, katika kikao na wabunge wiki iliyopita.

Bwana Trump alimkosoa bwana Maguire kwa kuarifu wabunge wa Democratic taarifa za kijasusi, na kumfuta kazi wiki moja baada ya kikao hicho.

Rais alitangaza wiki hii kwamba nafasi ya bwana Maguire itachukuliwa na Richard Grenell, balozi wa Marekani nchini Ujerumani ambaye anachukuliwa kuwa mwanifu kwa Trump.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Richard Grenell, balozi wa Marekani nchini Ujerumani, wiki hii ameteuliwa kuhudumu katika Shirika la Taifa la Kijasusi

Maafisa wawili katika utawala wa Trump wameliambia gazeti la New York Times kwamba kuondolewa kwa bwana Maguire ni jambo ambalo halikutarajiwa.

Democrats imeshutumu hatua ya rais ya kumteua bwana Grenell, ambaye awali alijaribu kunyamazia suala la ni kiwango gani Urusi iliingilia uchaguzi ulliopita.