Asayel Slay: Mwanamuziki wa kike Saudia kukamatwa kwa video aliotoa ya wasichana wa Mecca

Asayel Slay

Chanzo cha picha, Asayel Slay

Maafisa wa Saudia wameagiza kukamatwa kwa mwimbaji wa kike wa muziki wa 'rap' ambaye ametoa video ya muziki kwa jina Mecca ambayo ina sifu wanawake katika mji huo mtakatifu inayosema ni wenye "nguvu na wazuri".

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walionesha hasira yao na kusema kwamba mamlaka ina "unafiki".

Mwaka 2018, mwanamfalme mwenye msimamo mkali alianzisha pogramu ya kuendeleza mabadiliko.

Lakini wanaharakati wanasema kukandamizwa kumeongezeka na kumekuwa na msako wa kutishia uhuru wa kujieleza.

Video hiyo ilitolewa kupitia mtandao wa YouTube wiki jana na mwanamuziki huyo kijana ambaye anajiita Asayel Slay.

Muziki wa mwanadada huyo aina ya rap, unazungumzia wanawake wa mji wa Mecca, eneo takatifu kwa waumini wa Kiislamu ambao huenda mji huo kuhiji kila mwaka.

"Heshima yetu kwa wasichana wengine lakini wasichana wa Mecca ni wazuri sana," ameimba hivyo katika video yake huku wanaume na wanawake wakicheza densi katika mgahawa.

Video hiyo ilisambaa sana katika mitandao ya kijamii na watu wakitumia hashtag #Mecca_Girl_Represents_Me kuisifu.

Alhamisi gavana wa Mecca Khaled al-Faisal aliagiza wale wote waliofanikisha video hiyo wakamatwe na kuandika kupitia mtandao wa twitter kwamba "inatukana utamaduni wa Mecca" na kutumia hashtag" Hao si wasichana wa Mecca".

Akaunti ya mwanamuziki Asayel Slay imefungwa na video hiyo haipatikani tena kwenye mtandao wa Youtube.

Ujumbe uliosambaa sana kwenye twitter ulisema, "Ni wimbo pekee wa aina ya rap ambao hauna maneno machafu, matusi, picha za ngono, picha za kuonesha watu walio uchi, kuvuta sigara na muimbaji amevaa hijab.

"Msichana huyo anatakiwa kukamatwa kwasababu wimbo wenyewe hauendani na maadili ya Saudi Arabia ya zamani au hata ya sasa."

Watumiaji wa mitandao mingine ya kijamii wanasema kwamba kutolewa na agizo la kukamatwa kwa mwanamuziki huyo kunaonesha ubaguzi uliopo ukilinganisha vile wanaume wanavyochukuliwa tofauti na wanawake.

Pia walizungumzia kisa cha mwanamuziki wa Morocco Saad Lmjarred ambaye aliruhusiwa kufanya onyesho mji wa Riyadh baada ya kushtakiwa mara tatu kwa tuhuma za ubakaji ambazo alikanusha.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wameshutumu mamlaka kwa kuonyesha dunia kwamba inakumbatia usasa lakini kinachotokea ndani ya nchi ni tofauti kabisa - kamatakamata ya watu.

Mwanamfalme Prince Mohammed Bin Salman aendeleza taswira ya kwamba nchi hiyo imebadilika akiwa nje ya nchi kama sehemu ya ruwaza ya 2030 ya mpango wa mabadiliko.

Wasaniii kama vile Mariah Carey, Nicki Minaj na BTS wamekuwa wakialikwa kufanya maonesho Saudia Arabia.

Hata hivyo mwanamuziki Nicki Minaj alilazimika kuahirisha tamasha lake baada ya maneno aiyotoa yaliyoashiria kwamba anaunga mkono haki za wanawake na jamii ya mapenzi ya jinsia moja.

Katika tamasha la muziki la Desemba, raia 120 wa Saudi wanawake kwa wanaume walikamatwa kwa kuvaa mavazi yaliosemekana ni utovu wa maadili.