Marufuku yawekwa ya uhusiano wa mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi, Uingereza

UCL building on Gower Street

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Chuo Kikuu cha London chaanzisha sera ya kupiga marufuku uhusiano wa mapenzi chuoni

Marufuku ya kuwa na uhusiano wa mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha London ni mwamko mpya kwa vyuo vikuu, wachambuzi wamesema.

Makundi ya wanafunzi yamesema kwamba ni imani yao kuwa sera sawia na hiyo zitaanza kutekelezwa na vyuo vingine.

Chuo Kikuu cha London kinaaminika kuwa cha tatu nchini Uingereza kuanzisha marufuku hiyo.

Inasemekana kwamba sera hiyo inalenga kuzuia unyanyasaji kwa walio na madaraka na vitendo vya ngono.

Kelsey Paske, maneja wa kitengo kinachoangazia tabia ya utamaduni, amesema sera hiyo pia inalenga kutatua migogoro ambayo huenda ikazuka kutokana na mahusiano "huenda yakawa na athari mbaya katika mazingira ya kwenye taasisi za masomo".

Sera mpya ya mahusiano katika Chuo Kikuu cha London kwa wafanyakazi, kulingana na gazeti la the Guardian, inakataa "mahusiano ya karibu na ya mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi pale ambapo kuna usimamizi wa moja kwa moja".

Uhusiano wa mapenzi kati ya mfanyakazi na mwanafunzi ambaye hamsimamii kimasomo moja kwa moja ni lazima uwekwe wazi na mfanyakazi.

Sera hiyo pia inakataza mahusiano ya mapenzi na wafanyakazi au wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka 18 au watu wazima ambao wako katika hatari mfano, yule ambaye atahitaji usaidizi maalumu kwasababu nya ulemavu.

Kukiuka sera hiyo kutachunguzwa na kitengo cha kukabiliana na utovu wa nidhamu chuoni, ambao ni pamoja na uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua kuanzia kupewa onyo rasmi hadi kufutwa kazi au kufukuzwa chuoni.

Dr Anna Bull, wa shirika moja linalopinga vitendo dhidi ya tabia zinazoendeleza ngono katika taassi za shule za juu, amesema kwamba shirika lake linaunga mkono kikamilifu sera hiyo mpya na ni matumaini yao kwamba vyuo vingine vikuu vitafuata mkondo huo.

Alisema kuwa sera hiyo ni moja ya sheria kali Uingereza ambayo pia inatekelezwa na vyuo vikuu vingine viwili vya Greenwich na Roehampton.

Dr Bull ameongeza kuwa vyuo vingi vina sera ambazo zinakemea vikali uhusiano wa mapenzi kati ya wahadhiri na wanafunzi lakini sheria kama hiyo bado huenda ikatoa mwanya kwa wafanyakazi wanaotaka kuwa na uhusiano na wanafunzi ambapo wafanyakazi wanaweza kuitisha vikao nje ya jengo la chuo au hata kuzungumza na mwanafunzi kwa namna inayoashiria kuwa anatafuta uhusiano wa mapenzi.

"Tunaona kwamba huu ni mwito kwa sekta hii kuanza kuwajibika kwa kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya wahadhiri kutumia vibaya madaraka yao," amesema.

'Aliniomba nikutane naye kwenye baa'

Emma anasema ukosefu wa sera imara ya uhisiano kati ya wanafunzi na wahudumu kama wahadhiri katika chuo alichosomea awali lakini sio Chuo Kikuu cha London, kulimfanya asiwe na ujasiri na kusema kwamba msimamizi wake alikuwa na tabia ya ukosefu wa nidhamu ya aina hiyo.

"Tulikuwa tukikutana ana chukulia kama vile tuna mahusiano ya mapenzi na kunilazimisha tuonane kwenye baa wala sio katika ofisi yake na hatimaye akawa anachukulia eti kila mmoja wetu anaridhia uhusiano huo," anasema.

Msimamizi wa Emma alitaka kukutana naye baada ya kuwasilisha kazi yake, akakubali akidhani kwamba alikuwa anataka kumpongeza.

"Badala yake akanipeleka kwenye baa, na mara moja akaanza kuonyesha tabia kama vile tumekubaliana, kunishika mkono, kuninunulia kinywaji, na kutoa matamshi ambayo yalikuwa yanakashifu wahadhiri wangu na wanafunzi wenzangu," akaongeza.

Emma ambaye sio jina lake kamili, wakati huo alikuwa na miaka 20 na anasema kwamba iwapo kungekuwa na sera iliyowazi kama hiyo ingempatia fursa ya kukata kukutana na msimamizi wake nje ya jengo la chuo kikuu.

Kwa mfano, sera ya Chuo Kikuu cha London, inaonesha kwamba wahudumu wenye jukumu la msingi kama kusimamia, kufundisha, au kutoa huduma kwa wanafunzi, wanastahili kuhakikisha vikao kati yao na wanafunzi vinafanyika tu ndani ya jengo na wanastahili kutumia akaunti ya barua pepe au simu za chuoni kuwasiliana na wanafunzi.

"Nilijua kwamba kitendo kile si sahihi lakini sikutaka kutengeneza mazingira mabaya kati yetu kwa kusema kwamba sifurahii kile anachokifanya," Emma amesema.

Hata hivyo, wanafunzi wengine waliiambia BBC kwamba walikuwa na makubaliano ya kuwa na uhusiano na wahadhiri wao wakati wakiwa vyuo vikuu na wala hawaungi mkono marufuku hiyo.

Jen amesema alikuwa na uhusiano wa mapenzi na mhadhiri wake kwa miezi kadhaa alipokuwa na umri wa miaka 21.

Wawili hao walikutana wakati wote wawili wakiwa wanashirikiana katika kitengo cha kusaidia wanafunzi na mhadhiri huyo, 31, hakuwahi kuwa mhadhiri wake wa moja kwa moja katika somo lolote lile.

"Tulikuwa watu wazima wenye uwelewa wa kile tunachofanya na sikuwa na tatizo nalo wala hakuna ambaye alionyesha kukereka," amesema.

Chama cha Taifa cha Wanafunzi pia kimefurahishwa na sera mpya iliyoanzishwa katika Chuo Kikuu cha London.

Afisa mwanamke wa chama hicho Rachel Watters amesema: Ukiangazia suala la mahusiano ya mapenzi katika taasisi za elimu za juu na kwengineko, tunatarajia vyuo vingi zaidi kupitia tena sera zao kwa namna sawa na hiyo."

Msemaji wa Vyuo Vikuu Uingereza, anayewakilisha sekta hiyo amesema: "Wanafunzi wote na wafanyakazi ni haki yao kuwa salama na kupata tajriba nzuri, na vyuo vikuu vimejitolea kuwa sehemu salama kuishi, kufanyakazi na kusomea."

Shirika hilo limesema litachapisha mwongozo wake kwa vyuo vikuu kuhusu kudhibiti tabia zisizokubalika za mahusiano ya mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi msimu ujao.