Yevgeniy Fedorov: Muendesha baiskeli wa Kazakhstan ashinda Tour de Rwanda

  • Yve Bucyanna
  • BBC Swahili
Yevgeniy Fedorov ,wa timu ya Vino-Astana Motors ya Kazakistan ndiye aliyeshinda mkondo wa kwanza wa mashindano ya mbio za baiskeli maarufu Tour du Rwanda

Yevgeniy Fedorov ,wa timu ya Vino-Astana Motors ya Kazakhstan ndiye aliyeshinda mkondo wa kwanza wa mashindano ya mbio za baiskeli maarufu Tour du Rwanda ambayo yameanza leo.

Fedorov kijana wa mwenye umri wa miaka 20 ,ametumia saa 2 dakika 44 na sekunde 59 kumaliza mbio hizo za umbali wa kilomita 114.

Amemuacha nyuma kwa sekunde 15 mwendesha baiskeli wa pili Mulueberhan Henok kutoka timu ya Eritrea.

Mbio za mkondo wa kwanza zimeanzia mjini Kigali hadi katika mji wa Rwamagana ,mashariki mwa Rwanda na kurudi Kigali tena. Mshindi wa kila mkondo katika mbio hizi hujishindia dola 1200.

Timu 16 zinashiriki mashindano ya Tour du Rwanda 2020.

Baadhi ya timu zilizo na waendesha baiskeli wakali zaidi ni pamoja na Vino-Astana Israel Start up Nation ,Total Direct Energy ya Ufaransa na Team Novo Nordisk kutoka Marekani, lakini pia waendesha baiskeli kutoka Rwanda na Eritrea ambao wanajua vyema barabara za sehemu nyingi watakazozunguka nchini Rwanda.

Maelezo ya picha,

Ushindani mkali ukionekana miongoni mwa timu zilizoshiriki katika Tour de Rwanda 2020

Timu kutoka barani Afrika zinazoshiriki ni wenyeji Rwanda walio na timu 3, Eritrea pamoja na Afrika kusini.

Hata hivyo waendesha baiskeli wengi hasa kutoka Eritrea wanapatikana katika timu kadhaa za Ulaya zinazoshiriki mashindano haya.

Leo washindani wanatoka mjini Kigali kwenda mji wa kusini wa Huye ,barabara yenye umbali wa kilomita 120.

Ni kwa mara ya pili shindano la Tour du Rwanda kuchezwa likiwa kwa kiwango cha juu cha 2.1

Kiwango hiki ndicho cha juu zaidi barani Afrika katika mashindano yaliyoko kwenye kalenda ya shirikisho la mbio za baiskeli duniani UCI.