Erick Kabendera: Mwanahabari mpekuzi wa Tanzania aachiwa huru

  • Athuman Mtulya
  • BBCSwahili, Dar es Salaam
Eric kabendera na wenzake mahakamani

Mwandishi wa masuala ya uchunguzi nchini Tanzania Eric Kabendera ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa mahabusu kwa zaidi ya miezi sita.

Kuachiliwa huko kumekuja baada ya Kabendera kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Katika makubaliano hayo, Kabendera amekiri mashtaka mawili ya kukwepa kodi ya zaidi ya milioni 173 ya Tanzania na kutakatisha fedha ya kiwango hicho pia.

Kosa la kuongoza genge la uhalifu lilifutwa kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Katika shtaka la kukwepa kodi Kabendera amekubali kulipa kiasi cha shilingi za Tanzania milioni 172 kwa kipindi cha miezi sita.

Pili amelipa faini ya shilingi 250,000 za Tanzania kama faini, angeshindwa kulipa faini angepokea kifungo cha miezi 6 jela.

Katika kosa la pili la kutakatisha fedha Kabendera amelipa faini ya shilingi za Tanzania milioni 100.

Hatua hiyo inafuatia ombi la kutaka kuachiliwa huru alilowasilisha kwa mkurugenzi wa mashtaka katika mahakama ya kisutu jijini Dar es salaam.

Kabendera alikamatwa mwezi Julai 2019 , kwa tuhuma za kukwepa kulipa kodi, kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu.

Aliandika ripoti kali katika magazeti kama vile Independent,The Guardian na The Times mbali na katika magezeti mengine ya nyumbani ambayo yamekuwa yakiikosoa serikali.

Kumekuwa na ongezeko la ukosoaji dhidi ya jinsi serikali ya Tanzania inavyokabiliana na waandishi huru nchini humo.