Erick Kabendera: Amnesty Inernational, CPJ wakosoa namna mwandishi wa Tanzania alivyopata uhuru wake

Kabendera

Chanzo cha picha, Reuters

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International pamoja na Kamati ya Kulinda Wanahabari (CPJ) wamekosoa namna mwandishi wa habari za uchunguzi wa Tanzania alivyoachiwa na kudai kuwa hajatendewa haki.

Amnesty na CPJ wamelalamikia zaidi Kabendera kulipishwa faini kubwa ili kupata uhuru wake.

"Mama yake Kabendera alifariki siku chache tu baada ya kumuomba rais John Magufuli amwachie mtoto wake. Tayari ameshapitia mateso mengi kwa kufanya tu kazi yake, na alitakiwa aachiliwe bila masharti yoyote. Kwa kifupi hakukuwa na haki yeyote kutoka mahakamani" ameeleza Bi Deprose Muchena, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa bi Muchena ni jambo la "kufedhehesha kwa Kabendera kulipa faini kubwa kupata uhuru wake baada ya kukaa takribani jela miezi saba kwa kutekeleza uhuru wake wa kujieleza."

Naye mwakilishi wa CPJ kwa kanda ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Muthoki Mumo amesema: "Tunakaribisha kuachiwa kwa Kabendera baada ya takribani miezi saba jela, kwa mashtaka ambayo wazi kabisa yalikuwa ni kujibu mapigo kwa uandishi wake wa ukosoaji''.

''Lakini tunasikitishwa sana licha ya kuzuiliwa jela bila uwezekano wa dhamana ambapo aliumwa na kumpoteza mama yake, bado mkasa huu haujakwisha kwa Kabendera kutokana na faini kubwa ambazo zinaendelea kumuelemea."

Katika taarifa yao pia Amnesty imeitaka serkali ya Tanzania "kuacha kutumia vibaya sheria kwa kukandamiza uhuru wa raia."

"(Tanzania) inapaswa iahidi hadharani kuwa italinda uhuru wa watu kutekeleza haki zao za kibinadamu na kuacha kuwashitaki kisiasa wakosoaji na wanahabari kama Erick Kabendera."

Hata hivyo, serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha kubana uhuru wa watu na haki za binaadamu. Waziri wa Habari wa Tanzania Harrison Mwakyembe aliieleza BBC hivi karibuni kuwa Tanzania inafuata utawala wa sheria.

"...kuwa mwandishi wa habari hakumfanyi Kabendera kuwa juu ya sheria, kama ilivyo kwa wengine wote itakapoonekana kuna kosa iwe mwandishi ama raia mwingine hatua za kisheria zitafuatwa," alisistiza Mwakyembe.

Kabendera ameachiwaje?

Chanzo cha picha, Reuters

Kuachiliwa kwa Kabendera kumekuja baada ya kuingia makubaliano ya kukiri makosa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika mfumo ambao kwa Kiingereza unaitambulika kama 'plea bargaining'.

Katika makubaliano hayo, Kabendera amekiri mashtaka mawili ya kukwepa kodi ya zaidi ya milioni 173 ya Tanzania na kutakatisha fedha ya kiwango hicho pia.

Shtaka la tatu lilokuwa linamkabili hapo awali la kuongoza genge la uhalifu lilifutwa kama sehemu ya makubaliano hayo.

Baada ya kukiri makosa hayo, alitakiwa pia kukubali kulipa faini na fidia za jumla ya Shilingi za Tanzania milioni 273.

Katika shtaka la kukwepa kodi Kabendera amekubali kulipa kiasi cha shilingi za Tanzania milioni 172 kwa kipindi cha miezi sita.

Pili amelipa faini ya shilingi 250,000 za Tanzania kama faini, angeshindwa kulipa faini angepokea kifungo cha miezi 6 jela.

Katika kosa la pili la kutakatisha fedha Kabendera amelipa faini ya shilingi za Tanzania milioni 100.

Kabendera alikamatwa mwezi Julai 2019 , kwa tuhuma za kukwepa kulipa kodi, kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu.

Aliandika ripoti zake katika magazeti kama vile Independent, The Guardian na The Times mbali na katika magezeti mengine ya nyumbani. Baadhi ya taarifa zake ni za kuikosoa serikali.