MRKH: Julian Peters ni mwanamke aliyezaliwa bila uke wala mfuko wa uzazi

Julian Peters
Maelezo ya picha,

Tatizo la Julian Peters halina tiba zaidi ya kukubali hali yake.

Julian Peters ni mwanamke wa miaka 29 aliyezaliwa na hali inayojulikana kama (MRKH) Mayer-Rokitansky-Küster-Hauser, hali inayoathiri sana wanawake na hasa kizazi cha mwanamke. katika hali hii muathiriwa huzaliwa bila mfuko wa kizazi.

"Hali hii ninayoishi nayo ina changamoto nyingi kwani kila siku ninakabiliana na hisia mseto, mbali na hayo jamii inayonizunguka pia wakati mwengine ina taswira tofauti kuhusu hali hii", anasema Bi Julian

Julian anasema kuwa maoni ya jamii yanatofautiana kuhusu hali yake kwani kuna wale ambao wanaamini kuwa hali anayoishi nayo sio ugonjwa bali ni jambo alilojiletea mwenyewe, pengine kwa dhana kuwa aliavya mimba nyingi au pengine aliwahi shiriki maswala ya ushirikina.

Julian anasema maoni hayo wakati mwengine yanakera lakini anavumilia na kuendelea na maisha yake.

Je aligundua lini ana matatizo ya ugonjwa wa MRKH.

Aligundua kuhusu ugonjwa huu akiwa kidato cha tatu, wakati huo alikuwa na miaka 17, anakumbuka alienda hospitalini kupata ushauri wa daktari kwa sababu alikuwa anaumwa na miguu yake. Alipofika hospitalini daktari alianza kwa kumuuliza baadhi ya maswali

"Daktari aliniuliza wakati wa mwisho wa kupata hedhi yangu ni lini? Jibi langu lilikuwa sikuwa nimepata hedhi zangu" Julian akasema.

Maelezo ya picha,

Kulingana na daktari Mutindi Kakuti wanawake wenye ugonjwa huu wanaweza kushiriki ngono endapo watafanyiwa upasuaji wa kurekebisha njia au sehemu siri ya kike

Baada ya daktari aliyekuwa anamtibu kufahamu kuwa kwa umri wake wa miaka 17 hakuwa na hedhi, daktari alitaka afanyiwe uchunguzi wa sehemu zake za uzazi, baada ya uchunguzi kufanywa ikiwa ni pamoja na kupigwa picha ya kizazi chake, hapo ndipo iligunduliwa kwamba alikuwa hana kizazi chote kama wanawake wengine na pia njia ya uke wake ilikuwa imeziba kutoka upande wa nje.

Japo alikuwa hana umri mkubwa sana hakuelewa mengi kuhusiana na hali hiyo, kwa hiyo alipoelezwa na dakatari kama binadamu hakuamini alichokuwa anaelezwa, Julian anasema.

"Wakati huo nilikuwa shuleni na nilikuwa tayari nasomea baiolojia, nilifahamu jinsi mwili wa mwanamke unavyopaswa kufanana, kwa hiyo nililia sana kwa kutambua kuwa sehemu ya kizazi changu zilikuwa na kasoro ila sikuwa na lingine la kufanya"

Madaktari wakati huo waliamua kuwa wangemfanyia upasuaji ili kufungua njia ya uke wake.

Japo katika suala la mfuko wa kizazi hakuwa na la kufanywa zaidi ya kukubali kuishi maisha yake yalivyo.

Juliana anasema kuwa "Nilikubali kuhusu hali yangu nikiwa na umri wa miaka 24. Baada ya kuelezwa ukweli wa mambo, nilirejea shuleni tu na kuamua kusoma kweli kweli. Nilipomaliza shule ya sekondari nilianza kufanya uchunguzi wangu vitabuni, na nikaanza kuelewa changamoto nilizokuwa napitia kama muathiriwa wa hali hii

Je alikuwa na uhusiano wa kimapenzi?

Maelezo ya picha,

Mwanamke mmoja kati ya 4000 ulimwenguni ana tatizo la kutokuwa na kizazi sawa na la Julian

Julian anasema ijapokuwa amekuwa na mahusiano ya kimapenzi, hajajihusisha na shughuli ya tendo la ndoa

Unaweza pia kusoma:

Licha ya kwamba anakiri kwamba hali hiyo huenda ikamuathiri maishani mwake hajakata tamaa ya kuwa na mtoto.

"Sio lazima uwe mama kwa njia ya kuzaa pekee yake unaweza kuamua kumrithi mtoto ambaye hana wazazi na kumlea kama wako." Julian amesema.

Je nini kinachosababisha ugonjwa huu wa MKHR?

Kulingana na daktari Mutindi Kakuti, maswala ya uzazi nchini Kenya, hali hii hutokea wakati mtoto wa kike anapokuwa tumboni mwa mama yake, na wakati mwengine huibuka kuwa viungo vya mwili hususan vya uzazi vya mtoto hukosa kujiunda kama inavyofaa au kama ilivyo kawaida.

Daktari Kakuti anasema kuwa kiini haswa sio kwamba huu ni ugonjwa wa kurithishwa kutoka kwa mama hadi mtoto au kutoka kwa ukoo, ila tu ni jambo ambalo linaweza kufanyika kwa yeyote na inasemekana kati ya wanawake 4000 ulimwenguni mmoja huenda akawa na tatizo hili.

Kulingana na daktari Kakuti wanawake wenye ugonjwa huu wanaweza kushiriki tendo la ndoa endapo watafanyiwa upasuaji wa kurekebisha sehemu ya siri ya kike.