Israel Habimana: Raia wa Rwanda aliyeuza mali yake kutengeneza bwawa la umeme kwa wanakijiji

Mtambo unatumika kuzalisha umeme
Maelezo ya picha,

Mtambo unatumika kuzalisha umeme

Shughuli ya usambazaji nishati ya umeme katika mataifa yanayoendelea bado ni changamoto kubwa hususan maeneo ya vijijini.

Rwanda ni miongoni mwa mataifa hayo ingawa takwimu zinasema kuwa asilimia 52 ya wakazi wake wanahuduma ya umeme wengi wao wakiwa wakaazi wa maeneo ya mijini.

Pamoja na hayo baadhi ya wananchi vijijini wameanza kulivalia njuga tatizo la kutokuwa na umeme.

Bwana Israel Habimana aliweza kutengeneza bwawa dogo la umeme na kusambazia vijiji vinavyomzunguka eneo la mashariki mwa Rwanda kulingana na mwandishi wa BBC, Yves Bucyana.

''Niliweza kuzalisha umeme kutokana na haya maporomoko ya maji. Hili bwawa dogo lina uwezo wa kutoa kilowati 13 lakini pia utafiti niliofanya baadae niligundua kwamba zinaweza kuongezeka hadi kilowati 23 ingawa itategemea kama nitapata udhamini'' amesema Habimana.

Israel Habimana alitengenza bwawa dogo la umeme na kusambazia huduma hiyo familia zipatazo 200 za vijiji vinavyomzunguka wilayani Kirehe mashariki mwa Rwanda.

''Mfano mnamo wakati huu tunatumia kilowati mbili tu kwani wananchi wako katika shughuli za kilimo. Ukiangalia katika mtambo huu unaona mabadiliko ya kiwango cha matumizi ya nishati''.

Maelezo ya picha,

Bwawa dogo linalosambaza umeme kwa familia za mashariki mwa Rwanda

Kinachotumika kubaini kiwango cha umeme unaohitajika ni sauti ya mashine na inapobadilika inamaanisha kwamba tayari wananchi wameanza kutumia kiwango kikubwa cha umeme na fundi anayekuwepo huongeza hadi kiwango kinachohitajka na wananchi.

''Sauti ya mashine hii ikibadilika, inamaanisha wakulima wengi wamerejea makwaona kuanza shughuli zengine mfano saluni zimeanza kufanya kazi, karakana pamoja na wanaosaga nafaka.''

Licha ya hayo, Bwana Israel hakusomea taaluma hiyo kwani anavyosema mwenyewe alikomea katika elimu ya msingi.

Hata hivyo anasema aliandaliwa warsha maalum ya miezi kadhaa na shirika la nishati kuhusu utengenezaji wa mabwawa madogo ya umeme.

Israel Habimana ameiambia BBC kwamba alianza mradi wake mnamo mwaka 2012 na kumgharimu franga milioni 48 sawa na dolla zaidi ya elfu 50.

Mwanzoni wananchi wengi walimuona kama kichaa kwani alilazimika kuuza mali yake yote ikiwemo mashamba, nyumba na gari na isitoshe bado anadaiwa na wananchi pesa nyingi. Ila pamoja na hayo Bwana Habimana hajahisi kupata hasara yoyote.

''Sitambui hii kama hasara kubwa kwani ndoto yangu ilikuwa kuwaondoa gizani wanakijiji wenzangu. Sasa imetimia na sina shaka matunda yako mbele. Ni kweli mwanzoni watu waliniona kama kichaa lakini sasa najisikia fahari mno nikiwa na matarajio ya kuwa pole pole nitaanza kukusanya mapato kwa maslahi yangu. Na kizazi changu kitanufaika na mapato hayo ambapo nitakuwa nikikusanya kiasi cha asilimia 57 ya makusanyo ya malipo ya nishati iliyotumiwa na wananchi.'' amesema bwana Habimana

Lakini vipi wananchi kama vile wanaofanya kazi ya karakana wameanza kunufaika na huduma hii ya nishati?

Maelezo ya picha,

Seremala anayetumia umeme unaozalishwa kutoka kwa bawa dogo

Sindikubwabo umubaji fundi wa karakana moja anasema, ''mimi ni fundi seremala. Natumia nishati kwa kuwasha taa, kusikiliza redio na kuchaji simu, hayo ndiyo matumizi yangu nyumbani. Lakini mradi mkubwa ni huu wa useramara. Karibu vijiji vyote 10 majirani wanategemea karakana yangu na mimi huingiza pesa.''

Kila mwananchi mwenye umeme anatakiwa kulipa faranga elfu mbili kwa wakati huu wakiwa hawajapewa mtambo wa kuhesabu kiwango cha nishati kilichotumiwa.

Israel Habimana anasema kwamba ameshapata idhini kutoka kwa serikali kumruhusu kusambaza zaidi umeme huo katika vijiji vingine viwili vyenye wakaazi zaidi ya 200 na hivyo kuanza kupata faida.

Mamala ya nishati ya Rwanda inasema kuwa watu walio na umeme ni zaidi ya milioni 1.5 na malengo ni kwamba kila mwananchi atakuwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2024.