Hosni Mubarak alilazimika kuondoka madarakani baada ya kufanyika kwa maandamano makubwa

Hosni Mubarak

Chanzo cha picha, Getty Images

Aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak, atazikwa kwa mazishi ya kijeshi katika mji mkuu wa Misri, Cairo leo Jumatano.

Hosni Mubarak aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 91 Jumanne.

Ibada yake itafanyika katika msikiti wa Tantawy na kufuatiwa na mazishi yake katika makaburi ya familia mashariki mwa Cairo.

Serikali imetangaza siku tatu maombolezi ya kitaifa.

Bwana Mubarak alilazimika kuondoka madarakani mwaka 2011 baada ya kufanyika kwa maandamano makubwa miaka 30 baada ya kuwa rais kufuatia kifo cha Anwar el- Sadat.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alimpongeza Mubarak kwa kujitolea kwake kuhakikisha amani na usalama vinapatikana lakini jumuiya ya kimataifa kwa ujumla haijazungumzia lolote kuhusu na kifo chake.

Hosni Mubarak alikuwa mwanajeshi lakini alijitolea sana kwa nchi yake kuhakikisha inakuwa na Amani.

Chini ya utawala wake, Misri ilichukua jukumu ongozi kujaribu kufikia makubaliano kati ya Israel na Palestina.

Miongo yake mitatu ya kuwa madarakani ilifikia ukomo 2011 wakati wa vuguvugu la mageuzi katika nchi za kiarabu na kulazimika kung'atuka mamlakani.

Alikabiliwa na ukosoaji mkali kwa kutumia hali ya hatari kukamata wapinzani na miaka yake ya mwisho ya maisha alikuwa ana kabiliana na kesi za ufisadi.

Alikuwa mwanaanga

Muhammad Hosni Said Mubarak alizaliwa Mei 4, 1928 katika eneo la Kafr-El Meselha, kaskazini mwa Misri.

Licha ya kutoka katika familia maskini, alihitimu kutoka Chuo cha Jeshi cha Misri mwaka 1949. Baadae akahamia kikosi cha anga ambapo alipangiwa kufanyakazi mwaka 1950.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Hosni Mubarak akiwa mwanajeshi wa anga mwaka 1952

Kwa kipindi cha miaka miwili, alikuwa akiendesha ndege za kivita na kuwa mwelekezi wa ndege hizo. Alishuhudia kupinduliwa kwa Jenerali Gamal Abdel Nasser mwaka 1952 na vita vya Suez vilivyofuata.

Mwaka 1959, Mubarak alisafiri hadi Muungano wa Soviet - iliyokuwa msambazaji mkubwa wa silaha kwa serikali mpya ya Misri - ambapo alijifunza kuendesha ndege za mabomu.

Alimuona Suzanne akiwa na umri wa miaka 17, binti ya daktari na kupanda ngazi taratibu hadi kuwa kiongozi wa chuo cha jeshi la angani na kisha akawa mkuu wa wafanyakazi wa jeshi la angani mwaka 1972.

Shujaa wa Taifa

Lakini katika majukumu yake yaliofuata- kamanda wa jeshi la angani la Misri na naibu Waziri wa Ulinzi ndipo alipojenga jina lake.

Mubarak alikuwa muhimu sana katika upangaji wa shambulizi la kushtukiza kwa vikosi vya Israel mwanzoni mwa vita vya Waarabu na Waisrael mwaka 1973.

Shambulio hilo lilifanyika Yom Kippur, katika siku takatifu kwenye kalenda ya wayahudi. Mubarak alikuwa shujaa wakitaifa katika jukumu lililotekelezwa na jeshi la angani katika Mfereji wa Kanali

Urusi na Marekani walikaribia kuingia katika vita vya nchi zenye nguvu zaidi duniani na kukimbilia kusambazia washirika wao silaha.

Israel ilizuia uvamizi lakini ikasalimu amri katika vita vya Sinai kwa Msri.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wanajeshi wa Israeli wakindoka Ukingo wa Magharibi wa Mfereji wa Suez nchini Misri, 1973

Makamu wa Rais

Mafanikio yake alianza kuyashuhudia miaka miwili baadae baada ya Rais Anwar Sadat kumteua kama makamu wake.

Sadat aliegemea zaidi katika kile alichokiita sera ya kigeni na kufurusha washauri wa Muungano wa Usoviet, alitembelea Jerusalem akiwa vitani na kufukuza viongozi wa Saudi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Sadat alimteua Hosni Mubarak kama naibu wake 1975

Mubarak alijikita katika masuala ya ndani ya nchi lakini akaanza kujenga mahusiano mazuri binafsi na viongozi wenzake wa Arabuni - hususan na mwana mfalme wa Saudi, Fahd.

Hakuwa mfuasi mkubwa aliyetambuliwa kuunga mkono Mkataba ya Amani wa Camp David 1979 - uliotiwa saini na Rais Sadat na Waziri Mkuu wa Israeli, Menachem Begin.

Mkataba huo uligawanya nchi za kiarabu. Mubarak alijutia kushindwa kwa Sadat kuzuia kuzorota kwa uhusiaono na washirika wake huku makundi yenye msimamo mkali yakichochewa na kile kilichoonekana kama usaliti.

Oktoba 1981, wanajeshi waliokuwa wanaunga mkono moja ya makundi hayo walimuua Sadat wakati wa gwaride la kukumbuka ushindi wake mwaka 1973 wakati wa vita vya Waarabu na Waisrael.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mubarak alijeruhiwa katika maujai ya rais Sadat, 1981

Wauawaji walijificha kwenye lori ambalo lilisimama mkabala na rais. Akiendelea kufikiria kwamba ni sehemu ya gwaride, alisongea mbele kidogo ili kuwapigia saluti.

Wakarusha gurunedi na kupiga risasi kila mmoja aliyekuwa karibu kwa kutumia bunduki aina ya AK-47. Sadat aliaga dunia hospitalini saa mbili baadaye; na Hosni Mubarak akawa miongoni mwa waliojeruhiwa.

'Amani Baridi'

Mubarak alimrithi rais kwa kupata asilimia 98 ya kura zilizopigwa kwenye kura ya maoni ambapo yeye alikuwa mgombea pekee.

Aliahidi kuendeleza mkataba wa Camp David lakini ikaonekana wazi kwamba uhusiano na Israel unaendelea kufifia kuliko ulivyokuwa chini ya Sadat.

Wachambuzi walianza kuelezea hali hiyo kama "Amani baridi".

Misri na Saudi Arabia mingoni mwa nchi tajiri za Uarabuni - pia ziliungana kupinga nguvu ya madaraka inayoongezeka ya Ayatollah Khomeini wa Iran.

Misri - ilioondolewa katika ligi ya Uarabuni 1979 - ikarejeshwa tena, na makao makuu yake yakarejeshwa mji wa nyumbani kwenye ukingo wa mto Nile.

Mubarak alisomea Chuo cha Jeshi cha Usovieti na kuzungumza Kirusi lakini alikuwa makini kuimarisha uhusiano na nchi za Magharibi.

Jukumu lake muhimu katika mchakato wa kutafuta Amani kati ya Israel na Palestina, kuliimarisha uhisiano wake na maraisi wa Marekani waliofuata, ambao walimpa msaada wa mabilioni ya madola.

Wakosoaji walimlaumu kwa kuwa kibaraka cha Marekani, kufunga na kuwatesa wapinzani wake na kufanya udanganyifu kwenye chaguzi.

Pia alitanua vikosi vya usalama wa ndani na kunusurika angalau majaribio sita ya kuuawa - akipata tu majera ya kisu katika bandari ya Said.

Vita vya Ghuba

Iraq kuvamia Kuwait mwaka 1991 kulikuwa pigo kubwa kwa Mubarak, ambaye alidai kwamba ameahidiwa na Saddam Hussein kuwa hakuna kitu kama hicho kilikuwa kinapangwa.

Wakati anaunga mkono vikwazo kama hatua iliyochukuliwa na jumuiya ya kimataifa, Mubarak aliahidi kutoa usaidizi wa jeshi kwa muungano dhidi ya kiongozi wa Iraqi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Mubarak aliungana na Jumuiya ya Kimataifa dhidi ya Iraq iliyovamia Kuwait. Wakosoaji wake walimshutumu kwa kuwa kibaraka wa Marekani.

Saddam alitoa wito wa kupinduliwa kwa serikali ya Misri lakini mabilioni ya madola kama deni yalifutiliwa mbali na Marekani na wakopeshaji wa kimataifa.

Mwongo mmoja baadae, Mubarak alijiondoa katika nchi zinazounga mkono uvamizi wa Iraq kulikoongozwa na Marekani 2003. Alisema kwamba hatua hiyo itapelekea kuundwa kwa mamia ya makundi ya Bin Laden na kuelezea Imani yake kwamba azimio la mgogoro kati ya Israel na Palestina ilikuwa ndio kipaumbele kwa eneo hilo.

Alichaguliwa tena bila kupingwa katika kura ya maoni 1987, 1993, na 1999.

Kulikuwa na uchaguzi wa vyama vingi mwaka 2005, lakini vyombo vya usalama wa ndani na mfumo wa uchaguzi uliendelea kuwa dhabiti chini ya udhibiti wa Mubarak.

Alifanikiwa kuvutia uwekezaji wa kigeni, ingawa matokeo yake mara nyingi yalishindwa kufikia wale waliokuwa katika hitaji zaidi.

Kulikuwa na ripoti kwamba utajiri wa familia ya Mubarak ulikuwa zaidi ya £50 billion.

Vuguvugu la Mageuzi katika nchi za Kiarabu

January 2011, Misri kukawaka moto. Kulikuwa na maandamano ambapo waandamanaji walikuwa wameghadhabishwa na umaskini, ufisadi, ukosefu wa ajira na utawala wa kidikteta.

Aliahidi kutogombea urais katika uchaguzi uliofuata lakini hilo halikutosha.

Baada ya siku 18 za maandamano, alisalimu amri na kutangaza kwamba anajiuzulu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Waandamanaji waliandamana dhidi ya Mubarak, 2011, na kulazimika kujiuzulu

Miezi minne badaae, Mubarak ambaye alikuwa mgonjwa alifikishwa mahakama. Akiwa hospitalini, alikabiliwa na kesi ya ufisadi na maandamano yaliyopangwa ambayo yalisababisha mauaji.

Timu yake ya ulinzi awali ilidai kwamba bado yeye alikuwa ni rais halali wa Misri na hivyo basi hakustahli kufikishwa mahakamani.

Juni 2012, Mubarak alipatikana na makosa na kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kushindwa kuzuia mauaji ya waandamanaji lakini akaondolewa mashtaka mengine.

Umamuzi wa mahakama ulisababisha maandamano katika maeneo mbalimbali mjini Misri.

Miezi sita baadae, hukumu yake ilibadilishwa na kuamuriwa kesi kusikilizwa tena. Alihukumiwa kifungo cha nyumbani akiwa hospitali ya jeshi mjini Cairo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mubarak aalifikishwa mahakamani 2014

Baada ya mahakama kutoa uamuzi mara kadhaa, Mubarak alifutiliwa mbali makosa ya ufisadi lakini akahukumiwa kwa ubadhirifu wa pesa.

2017, mahakama ya juu zaidi ya Misri hatimaye ilimuondolea shtaka la yeye kusababisha vifo vya waandamanaji na kuachiliwa huru.

Hosni Mubarak aliahidi kuendelea kuhudumia Misri hadi siku ya mwisho maishani.

Katika kipindi chake cha miongo mitatu madarakani, Misri ilisalia kuwa thabiti. Lakini wengi walifungwa bila kufunguliwa mashtaka na kuteswa.

Kimataifa, Mubarak aliendeleza sera ya kimataifa ambayo ililenga kumaliza migogoro ya ndani lakini nyumbani alitawala kimabavu.