Je hatua ya Serikali kuu kuchukua majukumu ya utawala wa kaunti ya Nairobi ina maana gani?

  • Na Hezron Mogambi
  • Muhadhiri Chuo Kikuu cha Nairobi
Serikali kuu ya Kenya imemuondolea Gavana wa Nairobi Mike Sonko mamlaka ya utawala, anayekabiliwa na tuhuma zikiwemo za ufisadi
Maelezo ya picha,

Serikali kuu ya Kenya imemuondolea Gavana wa Nairobi Mike Sonko mamlaka ya utawala, anayekabiliwa na tuhuma zikiwemo za ufisadi

Hatua ya kuyahamisha majukumu muhimu kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi hadi kwa Serikali Jumanne ni hatua ambayo imewapata wengi nchini Kenya kwa mshangao.

Hii ni kwa kuwa hatua hii inatokea wakati mjadala wa kumwondoa Gavana wa Nairobi Mike Sonko mamlakani ukisubiriwa juma hili katika Bunge la Kaunti ya Nairobi baada ya mwakilishi wodi wa Makongeni jijini Nairobi ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika bunge la Kaunti ya Nairobi, Peter Imwatok, kutoa notisi juma lililopita, ya kutaka kumwondoa Gavana Sonko mamlakani.

Kulinga na sheria na taratibu za bunge hilo la kaunti, mjadala na uamuzi wa Bunge la Kaunti utafikiwa baada ya siku kumi za kutoa notisi hiyo.

Hii ndiyo sababu hatua ya jana ya kuwepo makubaliano yaliyotiwa saini kati ya serikali kuu ya Kenya ikiongozwa na waziri wa ugatuzi, Eugene Wamalwa na Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko ambayo pia yalishuhudiwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi jana mchana yamewashangaza wengi.

Je, ni kwa nini pawepo makubaliano na pande hizi mbili ilhali kuna mjadala unaotarajiwa katika Bunge la Kaunti ya Nairobi kuhusiana na kumwondoa mamlakani gavana Sonko juma hili?.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Kenya

Maelezo ya picha,

Rais Uhuru Kenyatta amechukua majukumu muhimu ya serikali ya kaunti ya Nairobi katika kile ambacho ofisi yake imeelezea ni "makubaliano ya kihistoria ".

Ingawa hili ni swali lenye uzito, lazima ikumbukwe kuwa iwapo hatua hii itaendelea na Gavana Sonko kuondolewa mamlakani, basi jiji la Nairobi lingebaki bila usimamizi wowote na wakaazi wangetatizika pakubwa.

Kulingana na taarifa kutoka kwa ikulu ya Rais, serikali ya kitaifa itaanza kusimamia huduma za afya, uchukuzi, ujenzi na mipango, na shughuli za kimaendeleo.Itakumbukwa kuwa Gavana Sonko ana kesi mahakamani inayomzuia kufika afisini mwake kulingana na agizo la mahakama.

Aidha, Kaunti ya Nairobi hana Naibu Gavana kwa kuwa aliyekuwa Naibu Gavana, Polycarp Igathe, alijiuzulu mnamo Januari mwaka wa 2018 kutokana na kile alichokiita, "kukosa kuelewana na Gavana Sonko kuhusu usimamizi wa jiji la Nairobi."

Katika hatua ambayo wachanganuzi wengi wameitilia doa, Gavana Sonko hakumteua Naibu wake kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili hali ambayo ilitatiza utoaji huduma katika jiji kuu la Nairobi.

Zaidi ya haya, msumari ulitiwa kwenye kidonda pale Gavana Sonko mwenyewe alipofikishwa mahakamani mnamo Disemba mwaka uliopita akishtakiwa kwa makosa ya ufisadi, uvujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya mamlaka.

Chanzo cha picha, SONKO/FACEBOOK

Maelezo ya picha,

Makubaliano yaliyompokonya Bwana Mike Mbuvi Sonko kati ya serikali ya Kaunti ya Nairobi yamefanywa kulingana kipengele cha 187 cha katiba ya Kenya.

Zaidi, mahakama ilimzuia asifike afisini ili kutovuruga ushahidi. Hali hii ya kukosa kuwepo kwa gavana na naibu wake katika usimamizi wa jiji la Nairobi kuliweka jiji la Nairobi katika hali ya ati ati huku wakaazi wakilalamikia hali duni ya utoaji huduma.

Hatua yake ya hivi karibuni ya kutaka kumteua Naibu Gavana ili kuhakikisha kuwa jiji la Nairobi halikosi uongozi ipasavyo iligonga mwamba pale mahakama kuu ya Kenya ilipolikataza bunge la Kaunti ya Nairobi kumpiga msasa Bi Anne Kananu, ambaye Gavana Sonko alikuwa amteua kama naibu wake.

Hapo awali, bunge la Kaunti ya Nairobi lilikuwa limeiomba serikali ya kitaifa kutoa usaidizi kwa serikali ya kaunti ya Nairobi katika kuhakikisha kuwa wakaazi wa jiji la Nairobi wanapata huduma ipasavyo kwa sababu ya ukosefu wa Gavana na Naibu wake kwenye usimamizi wa Kaunti.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Tuhuma dhidi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike sonko na hatua ya mahakama mahakama kumzuwia asifike ofisini ili kutovuruga ushahidi vilizorotesha huduma za jiji kwa raia

Makubaliano kati ya jana serikali ya Kaunti ya Nairobi na Serikali ya kitaifa yamefanywa kulingana kipengele cha 187 cha katiba ya Kenya ambacho kinahusu uhamishaji wa majukumu kati na baina ya viwango mbali mbali vya serikali nchini Kenya. 

Kulingana na makubaliano hayo yaliyotiwa saini jana katika ikulu ya Nairobi ambayo BBC iliweza kuyaona, usimamizi wa kaunti ya Nairobi ukiongozwa na Gavana Mike Sonko ulikiri kutokuwa na uwezo na kuetekeleza majuku fulani pamoja na migongano ya ndani kwa ndani ambayo imepelekea utoaji huduma kwa wakaazi wa Nairobi kutofikiwa ipasavyo.

Aidha, serikali ya Kaunti imekiri kushindwa kuwajibika kutekeleza baadhi ya majukumu ambayo sasa yatatekelezwa na Serikali ya kitaifa