Nzige Afrika: Je, mataifa yanahitaji nini kukabiliana na tishio la wadudu hawa?

  • Na Reality Check
  • BBC News
Mwanamume akinyunyizia dawa Ethiopia

Chanzo cha picha, FAO/Petterik Wiggers

Maelezo ya picha,

Unyunyiziaji wa dawa umekuwa ukifanyika katika mataifa mengi, ikiwemo Ethiopia na Kenya

Umoja wa Mataifa umetoa ombi la kutolewa kwa fedha zaidi kukabiliana na nzige ambao wanatishia kuharibu mimea katika maeneo ya Afrika na Asia.

Je, kunahitajika nini na mataifa yaliyoathiriwa yana rasilimali za kutosha kukabiliana na tishio hili?

UN official Mark Lowcock
Getty Images
Ongezeko hili linatishia...upatikanaji wa chakula katika kanda ambayo tayari haina chakula cha kutosha. Hakuna muda wa kupoteza
Qu Dongyu
Mkurugenzi Mkuu wa FAO

Tishio ni kubwa kiasi gani?

Shirika la Chakula Duniani (FAO) linasema mzozo wa chakula huenda ukawa unanukia karibuni iwapo rasilimali zaidi hazitatolewa, na limewasilisha ombi la pesa za ziada $62m (£48m).

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa Qu Dongyu anasema wiki chache zijazo zitakuwa na umuhimu mkubwa.

Juhudi za kukabiliana na nzige zinaendelea katika mataifa 13, kuanzia India upande wa mashariki hadi Mauritania upande wa Afrika Magharibi.

Lakini tishio kuu lipo Afrika Mashariki na Yemen, pamoja na mataifa ya Ghuba, Iran, Pakistan na India.

Karibuni zaidi, nzige walionekana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na makundi makubwa ya nzige yamewasili pia Kuwait, Bahrain na Qatar, pamoja na pwani ya Iran.

FAO wameambia BBC kwamba katika mataifa matatu yaliyoathirika zaidi ambayo ni, Kenya, Ethiopia na Somalia, wanakadiria kwamba hekari 100,000 katika kila taifa zinahitaji kunyunyiziwa dawa za kuwaua nzige.

Kufikia mwisho wa mwezi Januari, maeneo yaliyonyunyiziwa dawa yalikuwa chini sana ya kiwango kilicholengwa katika mataifa hayo ya Afrika Mashariki.

  • Ethiopia hekari 22,550
  • Kenya hekari 20,000 (kadirio)
  • Somalia hekari 15,000 (kadirio)

Pesa zinazohitajika ni kiasi gani?

Januari, FAO walitoa ombi la kutolewa kwa $76m. Kiasi hicho sasa kimeongezwa hadi $138m.

Hata hivyo, kufikia sasa pesa zilizotolewa ni $33m, $10m kati ya hizo zilitolewa wiki hii na Wakfu wa Bill & Melinda Gates.

Umoja wa Mataifa unasema pesa hizi zinahitajika kusaidia mataifa kukabiliana na nzige kupitia kunyunyizia dawa ardhini na pia kutoka angani. Kadhalika, zinahitajika kuratibu juhudi za kukabiliana na nzige kwa pamoja maeneo ya mpakani.

Lakini fedha hizo zinatumiwa pia kutoa usaidizi wa sasa hizi na wa kipindi kirefu kuwasaidia wakulima ambao kipato chao kimeathiriwa na uvamizi huu wa nzige.

Wadudu hao waharibifu ambao huwa kiasi sawa na uzani wao kila siku wanazaana upesi kiasi kwamba idadi yao inaweza kuongezeka mara 400 kufikia Juni.

Mataifa yanahitaji nini?

Vifaa na watu wa kunyunyizia wanahitajika sana katika kukabiliana na nzige, lakini hivi vyote havipatikani kwa viwango vya kutosha.

Kunahitajika pia ndege, magari, vifaa vya kujikinga wakati wa kunyunyizia, redio za mawasiliano, mitambo ya kupima maeneo au GPS na vifaa vya kukita hema maeneo ambayo nzige wanahitaji kukabiliwa.

Unyunyiziaji wa dawa kutoka angani na ardhini pamoja na kuwafuatilia nzige kwa makini kila wanakoenda - nzige husonga na kuhama kwa kasi - vinatazamwa kama njia bora zaidi ya kukabiliana nao.

Dkt Stephen Njoka, mkuu wa Shirika la Kukabiliana na Nzige wa Jangwani Afrika Mashariki (DLCO-EA), shirika la kanda hii linaloratibu juhudi za kukabiliana na nzige alitwambia: "Tuna changamoto katika idadi ya ndege zilizopo - hazitoshi. Dawa za kuua wadudu pia hazitoshi."

Anasema kwa sasa Ethiopia inatumia ndege tano kunyunyizia, nayo Kenya inatumia sita kunyunyizia na nyingine nne kufanya upelelezi wa kutambua maeneo ambayo nzige wapo.

Serikali ya Kenya hivi majuzi ilisema inahitaji ndege 20 kukabiliana na nzige hao.

Aidha, kunahitajika pia kiasi cha kutosha cha dawa aina ya Fenitrothion ambayo inatumiwa kuwaua nzige.

Waziri wa Kilimo wa Kenya Peter Munya amesema dawa hiyo inanunuliwa kutoka Japan.

Mwezi mmoja uliopita, serikali ya Kenya ilisema ilikuwa imesambaza lita 4,700 za dawa ya kuua nzige maeneo yaliyoathiriwa na kwamba ilitangaza kusambaza lita 20,000 zaidi.

Bw Munya mapema wiki iliyopita alisema serikali ilikuwa imepokeza shehena ya kwanza ya lita 7,500 kutoka nje ya nchi, lakini ukilinganisha na hitaji hiyo ni theluthi moja tu ya dawa inayohitajika.

Somalia kwa sasa haifanyi unyunyiziaji wowote. Serikali ya taifa hilo - pamoja na afisi ya FAO Somalia - imetoa wito wa kuongezwa pakubwa kwa juhudi za kupeleleza walipo nzige na kukabiliana nao nchini humo.

FAO pia inasema nchini Yemen hakuna hatua kubwa zilizochukuliwa katika kupeleleza walipo nzige na kukabiliana nao.

Hii inatokana zaidi na vita vinavyoendelea nchini humo.

Na kutoa mafunzo kwa watu wa kukabiliana nazo?

FAO imesema hili ni suala muhimu sana kwa sasa kutokana na ukubwa wa uvamizi huu wa sasa wa nzige.

"Mengi ya mataifa haya hayajakabiliana na tatizo kama hili la znige katika kipindi cha miaka 25 na kwingine hata miaka 70, na kwa hivyo hakuna idadi kubwa ya wataalamu wenye ujuzi wa kukabiliana na nzige," FAO waliambia BBC.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Nzige walitoka Yemen ndipo wakaingia Ethiopia na maeneo mengine Afrika Mashariki

Kuna mipango ya kutoa mafunzo inayoendelea katika mataifa yaliyoathirika, na nchini Kenya kwa mfano zaidi ya maafisa 240 wa serikali wamefunzwa kuhusu njia za kufuatiliana na kukabiliana na nzige.

Lakini bado kunahitajika mafunzo zaidi.

Tayari hali ni mbaya kwa sasa, lakini hatua zaidi zisipochukuliwa kwa haraka hali itakuwa hata mbaya zaidi.