Rais wa Guinea-Bissau Cipriano Cassamá ajiuzulu baada ya 'kutishiwa kuuawa'

Cipriano Cassamá

Chanzo cha picha, Dan Sanha

Maelezo ya picha,

Cipriano Cassamá alikuwa spika wa bunge mpaka alipoteuliwa kuwa rais wa mpito

Mmoja kati ya wanaume aliyetangazwa kuwa rais wa Guinea-Bissau amejiuzulu kutoka kwenye nafasi hiyo baada ya kukaa madarakani kwa siku moja, akisema maisha yake yalikuwa hatarini

Cipriano Cassamá alichaguliwa na wabunge kuwa rais baada ya chaguzi zilizosusiwa mwezi mwezi Desemba.

Hatua hii ni pamoja na ukweli kuwa Jenerali wa jeshi wa zamani Umaro Cissoko Embaló tayari alikwisha apishwa kuwa rais katika hoteli mji mkuu wa nchi hiyo, Bissau.

Guinea-Bissau imekutwa na matukio tisa ya mapinduzi tangu mwaka 1980.

Koloni hilo la zamani la Ureno, pia limekuwa njia ya usafirishaji wa madawa ya kulevya kutoka Amerika Kusini yakielekea Ulaya.

Kwanini Guinea-Bissau ina marais wawili?

Kura zilikusudiwa kufuta kumbukumbu ya yaliyopita, lakini badala yake, zimesababisha mgogoro mpya wa kisiasa katika taifa ambalo Jeshi limekuwa na ushawishi wa kisiasa.

Tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza bwana Embaló kuwa amemshinda mpinzani wake, Domingos Simoes Pereira kwa asilimia 54% kwa 46% katika uchaguzi wa duru ya pili mwezi Desemba tarehe 29.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa bwana Embaló wakishangilia baada ya kutangazwa mshindi

Rais aliyeondoka madarakani José Mário Vaz alikabidhi madaraka kwa Bwana Embaló katika sherehe zilizofanyika katika hoteli ya kifahari siku ya Alhamisi.

Lakini Bwana Pereira wa chama cha PAIGC, kilichoiongoza Guinea-Bissau kupata uhuru wake na kilichokuwa pekee mpaka 1990, alikataa kuapishwa kwa Embaló, akisema uchaguzi ulitawaliwa na udanganyifu.

Kisha kikatumia wingi wa idadi ya wabunge kumuapisha bwana Cassamá, spika wa bunge kuwa rais wa mpito, mpaka Mahakama ya juu ilipotoa uamuzi kuhusu ombi la kubatilisha ushindi wa Embaló.

Cassamá amesema nini?

Bwana Cassamá amesema hakuwa na cha kufanya isipokuwa kuondoka madarakani kwa kuwa amekuwa akikabiliwa na vitisho vya kuuawa.

''Sina ulinzi... Maisha yangu yako hatarini, maisha ya familia yangu yako hatarini,maisha ya watu wa taifa hili yako hatarini. Siwezi kukubali hali hii, ndio sababu nikachukua uamuzi huu,'' aliwaambia waandishi wa habari.

Cassamá hakusema ni nani aliyemtishia maisha yake.

Mmoja wao, Aristides Gomes, alisema maafisa wa jeshi walivamia nyumbani kwake mjini Bissau ili kumshurutisha ajiuzulu.

''Walitishia kuwaua maafisa wa usalama ikiwa hawatajiuzulu, na kunitishia kuniua kama sitajiuzulu nafasi ambayo nilipatiwa kwa muibu wa sheria,'' alisema.

Jumuia ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika (Ecowas), imetoa wito wa kusitishwa mvutano huo.

Bwana Embaló amesema anataka kutatua mzozo na kuipatia maendeleo Guinea-Bissau, moja kati ya nchi masikini duniani, iliyo na watu ilioni 1.6.