Je mapigano ya Jubaland na serikali ya Somalia yanaweza kuwaingiza zaidi Alshabab Kenya?

Zaidi ya watu kumi walifariki kwenye makabiliano makali yaliyofanyika Jumatatu

Chanzo cha picha, JUBBALAND TV SHOW

Maelezo ya picha,

Zaidi ya watu kumi walifariki kwenye makabiliano makali yaliyofanyika Jumatatu

Hali ya utulivu imerejea katika eneo la Mandera kaskazini mwa Kenya baada ya mapigano makali yaliyotokea Jumatatu kati ya wanajeshi wa serikali ya Somalia na wale wa eneo la Jubaland.

Kwa mujibu wa mwandishi wa idhaa ya Somalia ya BBC aliye katika mji mkuu wa Mogadishu, zaidi ya watu kumi walifariki kwenye makabiliano hayo makali siku ya jumatatu.

Mapigano hayo yalivuruga shughuli za kawaida kwa wakaazi wa mji wa Mandera na kusababisha biashara na shule kufungwa huku wanajeshi wa Kenya wakipiga doria kwenye mpaka wa taifa hilo na Somalia.

Chimbuko la mapigano hayo

Inaaminika kwamba utawala wa rais Mohamed Abdullahi Framajo uliwatuma vikosi vya kijeshi karibu na mpaka wa Kenya katika harakati za kujaribu kumkamata waziri wa ulinzi wa eneo la Jubland aliyetoroka jela huko Mogadishu mapema mwaka huu, Abdirashid Janan. Mamlaka za Somalia zinaamini kwamba waziri huyo analindwa na kufichwa na serikali ya Kenya.

Duru za kiusalama zimeidokezea BBC kwamba, baada ya siku nzima ya makabiliano makali, majeshi ya serikali ya Somalia yalifanikiwa kuvifurusha vikosi vya Jubaland kutoka ngome yao ya Ghedo iliyoko karibu na mpaka wa Kenya.

Wakati walipolemewa na wanajeshi wa Somalia, wale wa Jubland walikimbilia Kenya ambako walipewa hifadhi katika kituo cha polisi cha Mandera mjini ambacho kilikuwa chini ya ulinzi wa vikosi vya Kenya.

Hata hivyo, haikubainika iwapo Bw Janan alisalia katika hifadhi yake mjini Mandera ama amefichwa na majeshi ya serikali ya Kenya.

Abdirashid Janan atoroka jela

Chanzo cha picha, Nation media Group

Maelezo ya picha,

Ujumbe kutoka Jukbaland unasemekana ulikua umeenda Mandera

Waziri wa ulinzi wa eneo la Jubaland Abdirashid Janan alikamatwa mjini Mogadishu mwezi Agosti mwaka jana akiwa njiani kuelekea Addis Ababa kwa tuhuma za ukikwaji wa haki za kibinadamu. Alikuwa amehudumu miezi mitano jela kabla ya kutoroka katika mazingira tatanishi mapema mwaka huu.

Tangu Bw Janan alipowasili Kenya, hali ya taharuki mjini Mandera imekuwa ikitanda na kuwalazimu baadhi ya wakazi kutoroka makwao wakihofia mapigano kuzuka.

Habari za kuwepo kwa Bwana Janan nchini Kenya zimezidisha uhasama wa kidiplomasia kati ya Mogadishu na Nairobi.

Waziri huyo amekuwa akijificha katika hoteli moja mjini Mandera tangu Januari 30 baada ya kukwepa kutoka jela alikokuwa akizuiliwa na serikali ya Somalia tangu Agosti 31, 2019.

Wabunge wa Kenya walimtembelea rais Farmajo.

Wiki jana, wabunge kumi na mmoja kutoka kaskazini mwa Kenya walifanya ziara ya kisiri mjini Mogadishu ambapo walikutana na rais Mohamed Farmajo. Ingawa baadaye wabunge hao walihojiwa na vyombo vya usalama baada ya kurudi Kenya kwa kufanya ziara Somalia bila idhini ya serikali, watunga sheria hao wanasema kwamba mazungmzo yao na rais Farmajo yalilenga kutokomeza kundi la wanagambo wa Al-shabaab.

Chanzo cha picha, JUBBALAND TV

Maelezo ya picha,

Habari za kuwepo kwa Bwana Janan nchini Kenya imezidisha uhasama wa kidiplomasia kati ya Mogadishu na Nairobi.

Wabunge hao walijitetea kwamba waliitikia wito wa hivi karibuni wa rais Uhuru Kenyatta wa kujaribu kupata suluhu la kudumu kuhusu ukosefu wa usalama katika eneo la Kaskazini mwa Kenya unaosababisha uvamizi na umwagaji damu wa mara kwa mara wa wapiganaji wa kundi la Al-shabaab wenye ngome yao nchini Somalia.

Je, Kenya imejitia kitanzi?

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba huenda hatua ya Kenya ya kumlinda waziri wa ulinzi wa eneo la Jubaland Abdirashid Janan huenda ikachochea uhasama zaidi wa kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili na kulemaza vita dhidi ya wanamgambo wa Al-shabaab.

Mchambuzi wa maswala ya kiusalama George Musamali anasema huenda utawala wa rais Farmajo ukasitisha ushirikiano wake na Kenya katika mikakati ya kupambana na wapiganaji wa Al-shabaab.

Inaaminika pia kwamba viongozi wengi wa Kaskazini mwa Kenya, wakiwemo wale wabunge waliokutana na Rais Farmajo, hawaungi mkono hatua ya serikali ya Kenya ya kumhifadhi na kumlinda Bwana Janan.

Sasa swali lilibaki kwenye vinywa vya wengi ni, je, Kenya imejitia kitanzi kwa kumficha bwana janan?