Coronavirus: Kwanini ni marufuku kupeana mikono na busu?

Chanzo cha picha, AFP
Marufuku wachezaji kupeana mikono
Wachezaji nchini Tanzania wametakiwa kusalimiana kwa ishara badala ya kupeana mikono ili kujihadhari na maambukizi ya virusi vya corona.
Shirikisho la soka nchini humo, TFF limesema utekelezaji huo unaanza hii leo katika mechi za ligi kuu zitakazochezwa kwenye viwanja mbalimbali.
Ikulu ya Tanzania imetoa picha zikimuonesha rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli akisalimiana na viongozi wa upinzani bila kupeana mikono.
Hatua hiyo ni katika kuzingatia maelekezo ya wa Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu katika kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Magufuli na viongozi hao walisalimiana kwa ishara ya mikono na kugongeana miguu.
Watu pia wanaepuka kupigana mabusu mashavuni, kukumbatiana, kugongana mikono ili kuepuka maambukizi.
Mtaalamu wa afya Dokta Lindsay Broadbent anapinga vitendo vya kupeana mikono, akiiambia BBC kuwa kuna namna mbadala za kusalimiana ili kupunguza hatari ya maambukizi ya virusi.
Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Rais John Magufuli wa Tanzania akipeana ishara ya salamu na kiongozi wa chama cha NCCR MAGEUZI James Mbatia
Uganda
Rais wa Uganda Yoweri Museveni siku ya Jumamosi aliwataka raia wa Uganda kutoshikana mikono kuepuka maambukizi ya corona.
''Sasa kama wizara ilivyotuelekeza, tufanye maamuzi wenyewe kutoshikana mikono bila sababu au kujiweka katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa,'' Alisema kwenye taarifa yake.
Chanzo cha picha, Getty Images
Namna ya kuepuka maambukizi
China
Mjini Beijing, mji mkuu wa China ambako mlipuko ulianzia, mabango ya rangi nyekundu yakieleza watu wasishikane mikono isipokuwa kufunga mikono yao wenyewe kama ishara ya kusalimiana.
Matangazo ya vipaza sauti yamekuwa yakiwaeleza watu kutumia salamu ya utamaduni wa ishara ya kusalimiana iitwayo gong shou ( yaani kuweka ishara ya ngumi ya mkono mmoja juu ya mwingine)
Ufaransa
Magazeti yamejaa ushauri kuhusu mbadala wa salamu ya kushikana mikono, mazoea ya wakati wote ya utamaduni wa kubusu kwenye mashavu kwa watu ambao pia wanakutana kwa mara ya kwanza.
Mtaalamu wa masuala ya mitindo ya maisha Philippe Lichtfus, anasema kwa kumtazama mtu kwenye macho yake kunaweza kuwa ishara ya kumsalimia.
Australia
Brad Hazzard, Waziri mpya wa afya, aliwashauri watu kutopeana mikono, badala yake kumpigapiga mgongoni. ''Sisemi msipeane mabusu'' alisema, '' lakini muwe makini na mnayembusu.''
Brazil
Waziri wa afya ametaka raia kutopigana mabusu hata kama si kwa mdomo.
Chanzo cha picha, EPA
Tahahari dhidi ya virusi vya corona
Ujerumani
Waziri wa mambo ya ndani alijizuia kumpa mkono Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Uhispania
Mlipuko wa virusi vya corona pia huenda ukaiweka Uhispania katika tahadhari kubwa - utamaduni wa kubusu sanamu ya Bikira Maria wakati wa kipindi cha maajilio kuelekea Pasaka umeathirika.
''Ni moja kati ya hatua zilizo mezani,'' anasema afisa wa afya Fernando Simon.
Chanzo cha picha, AFP
Coronavirus
Romania
Tamasha la Martisor huashiria mwanzo wa majira ya kuchipua ambapo maua hutolewa, hasa kutoka kwa wanaume kwenda kwa wanawake.
Lakini sasa serikali imewataka watu watoe maua bila kupigana mabusu.
Poland
Poland ni moja ya nchi zinazofuata imani ya kikatoliki, wakati wa kukomunika, badala ya kulishwa mkate mdomoni, kila mtu ataupokea kwa mikono. Pia waumini wametakiwa kutochovya mikono yao kwenye
maji ya baraka wakati wa kuingia na kutoka na badala yake wapige tu ishara ya msalaba.