Coronavirus: Je, ni taarifa gani feki zinazoenezwa Afrika kuhusu virusi vya corona?

  • Na Reality Check
  • BBC
Mtoto akipimwa joto uwanja wa ndege wa Lagos, Nigeria

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kufikia sasa nchi 33 kati ya 47 Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara zina vifaa vya kupima virusi hivyo, ukilinganisha na mataifa mawili pekee Januari

Visa vya maambukizi ya coronavirus vinapoendelea kuongezeka duniani, kumekuwa na ongezeko la taarifa za uzushi na za kupotosha pia kuhusu ugonjwa huo.

Visa vilivyoripotiwa Afrika bado si vingi mno ukilinganisha na maeneo mengine duniani lakini serikali zinalazimika kukabiliana na mafuriko ya taarifa feki. Tumeangazia baadhi ya zilizoenezwa sana hapa:

1. Huhitaji kunyoa ndevu zako kujikinga

Picha ya zamani iliyotolewa na Idara ya Kukabiliana na Magonjwa Marekani (CDC) kuhusu ndevu na masharafa imekuwa ikitumika kimakosa kushauri kwamba wanaume wanafaa kunyoa ndevu zao kujikinga na virusi hivyo.

Gazeti la Punch la Nigeria lilichapisha habari yenye kichwa: "Ili kuwa sala kutoka kwa coronavirusi, nyoa ndevu zako, CDC yatahadharisha."

*Tumeweka viashiria kwenye picha kubainisha iwapo taarifa ni "feki" au imetumia "picha ya zamani".

Picha hizo ya CDC ina picha nyingi za mifano ya mitindo ya kunyoa ndevu na masharubu ambayo mtu anafaa kujiepusha nayo anapovalia barakoa za kutumiwa wakati wa kupumua. Miitndo ya ndevu kama vile 'Ndevu za Mashavuni' na Zappa zilikubalika lakini kuna mitindo mingine ambayo inaweza kuzuia mask hizo za kupumua zisifanye kazi vyema.

Picha hiyo ya michoro ni halisi lakini ilitengenezwa 2017 (kabla ya mlipuko wa sasa wa voronavirus) kwa ajili ya kutumiwa na wafanyakazi wanaohitajika kuvalia mask za kupumulia zinazobana. Kinyume na taarifa zinazoenezwa, CDC haijatoa ushauri wa karibuni kuhusu mask hizo na haishauri watu kunyoa ndevu zao au sharafa au hata kuzinyoa kwa mtindo fulani.

Vichwa vya habari sawia na hivyo vimechapishwa katika mitandao mataifa mengi na kuenezwa sana. Mtandao wa habari wa 7News nchini Australia uliandika kwenye Twitter: "Jinsi ndevu zako zinavyoweza kukuongezea hatari ya kupata coronavirus."

Ushauri wa sasa wa serikali ya Uingereza kuhusu afya ni kwamba ingawa mask zina umuhimu kwa wahudumu hospitalini, "kuna ushahidi finyu kwamba zina manufaa makubwa kwa umma."

2. Nabii wa Nigeria anayepigana na coronavirus

Mhubiri nchini Nigeria ambaye amekuwa akijiita nabii na kudai kwamba anaweza kutibu virusi hivyo pia amekuwa mwathiriwa wa taarifa feki.

Taarifa kumhusu David Kingleo Elijah, wa kanisa la Glorious Mount of Possibility Church zilianza kuenea mitandaoni baada ya video yake akisema kwamba atakwenda China "kuangamiza" virusi hivyo kupakiwa kwenye YouTube na kuenezwa kwenye mitandao mingine ya kijamii.

"Nitakwenda kuangamiza coronavirus kwa unabii. Nitakwenda China, ninataka kuangamiza coronavirus," anasema kwenye video hiyo.

Siku chache baadaye hata hivyo, taarifa ziliibuka kwenye mablogu zikidai kwamba alikuwa amesafiri hadi Uchina lakini akaambukizwa virusi hivyo akijaribu kuwaombea wagonjwa na akalazwa hospitalini.

Blogu zilimbandika jina - Elija Emeka Chibuke.

Picha zilizotumiwa kumuonyesha akiwa hospitalini zilikuwa ni picha za zamani, na aliyekuwa pichani ni Adeshina Adesanya, mwigizaji kutoka Nigeria maarufu kama Pasta Ajidara, aliyefariki hospitalini mwaka 2017.

3. Taarifa za uongo kuhusu dereva wa teksi

Taarifa kuhusu dereva wa teksi aliyemsafirisha Mwitaliano aliyegunduliwa kuwa na virusi vya corona nchini Nigeria zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye WhatsApp lakini hazikuwa za kweli.

Taarifa hizo zilidai kwamba mwanamume huyo alikuwa ametengwa na serikali ya jimbo la Ogun na akagunduliwa kuwa na ugonjwa huo lakini akatoroka hospitalini.

Taarifa hizo zilidai kwamba mwanamume huyo alikuwa anatishia kueneza virusi hivyo iwapo familia yake haingelipwa naira 100m ($274,000).

Serikali ya jimbo la Ogun limepuuzilia mbali taarifa hizo.

Serikali hiyo ya jimbo imesema hakuna mgonjwa yeyote aliyetoweka kutoka kwa kituo cha kuwatenga watu waliotangamana na watu wenye ugonjwa huo..

Taarifa hizo mara ya kwanza zilichapishwa kwenye ukurasa bandia uliojidai kuwa wa shirika la habari la Africa Independent Television (AIT). Shirika hilo limetoa taarifa kuukana ukurasa huo na taarifa hizo.

Taarifa hizo ilikuwa na picha ya dereva huyo ambaye jina lake lilitajwa kuwa Adewale Isaac Olorogun. Hata hivyo, picha iliyotumiwa ni picha iliyotumiwa kwenye taarifa nyingine ya Buzzfeed kwenye taarifa kuhusu utumwa Libya. Picha hiyo ilikuwa ya - Jude Ikuenobe.

Bw Ikuenobe aliambia mwandishi wa BBC Yemisi Adegoke kwamba alishangaa sana kusikia akitajwa kwenye taarifa hizo na kwamba alijawa na hofu kutokana na vitisho vilivyokuwa vinatolewa na watu wakichangia maoni kwenye taarifa hizo.

"Sijakuwa nikisafiriki pekee yangu tena [kwa sababu ya wasiwasi]. Kila niendapo, nakwenda na marafiki au jamaa.

"Tangu wakati huo [picha iliposambazwa] haijakuwa rahisi."

Nigeria ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kuripoti kisa cha coronavirus, mwathiriwa akiwa mwanamume Mwitaliano aliyefika nchini humo kutoka Lagos 25 Februari.

Serikali imesema imefanikiwa kuwafikia watu 100 ambao huenda walitangamana na mwanamume huyo.

4. Sauti ya mazoezi ya kutangaza corona Kenya

Nchini Kenya, serikali ililazimika kutoa taarifa kupuuzilia mbali "taarifa za uzushi" kuhusu kuripotiwa kwa visa vya corona nchini humo.

Hii ilitokana na kanda ya sauti iliyorekodiwa ambayo ilisambaa sana kupitia WhatsApp ikidaiwa kuwa ya afisa akihutubia kikao cha wanahabari kutangaza kutokea kwa virusi hivyo..

Kanda hiyo ilidai kulikuwa na visa 63 vya corona nchini humo, jambo ambalo si la kweli. Kufikia sasa bado hakuna kisa kilichothibitishwa cha corona nchini Kenya.

Wizara ya afya ilisema kanda hiyo ilirekodiwa wakati wa kikao cha mazoezi ya kutoa mafunzo kwa maafisa wa mawasiliano mjini Machakos. Hata hivyo, haikueleza ni vipi kanda hiyo ilirekodiwa na kuanza kusambaa.

Chini ya sheria za Kenya, mtu anaweza kupigwa faini ya $50,000 (£39,000) au kufungwa jela miaka miwili kwa kueneza habari za uzushi mitandaoni.

5. Tiba

Nchini Nigeria, mhubiri aliweka video na bango mitandaoni akidai kwamba supu ya pilipili kali inaweza kutibu corona. Madai hayo yalienezwa pia kupitia WhatsApp.

Kufikia sasa, bado hakuna dawa ya kutibu wala chanjo ya kujikinga dhidi ya corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema lipuko wa sasa umesbabaisha kuenea sana kwa taarifa za uzushi na za kupotosha kuhusu virusi hivyo.

Nchini Cape Verde, taifa la visiwani Afrika Magharibi, ujumbe umekuwa ukienea kwamba daktari mmoja kutoka Brazil amependekeza watu wanywe chai ya shamari kama tiba ya corona. Hii ilisababisha watu wengi kukimbia sokoni kununua shamari, ambayo ni kiungo cha jamii ya karoti, kwa mujibu wa AFP.

Wizara ya afya nchini Brazil imewatahadharisha watu dhidi ya kusambaza taarifa hizo.

WHO inasema kunawa mikono vyema ni muhimu katika kusaidia kuzuia maambukizi.