Je, kitumbua cha Diamond Platinumz na Tanasha Dona kimeingia mchanga ama ni kiki za kibiashara?

  • Abdalla Seif Dzungu
  • BBC Swahili
Tanasha Donna na mpenzi wake Diamond Platinumz

Chanzo cha picha, TANASHA DONNA/FACEBOOK

Maelezo ya picha,

Tanasha Donna na mpenzi wake Diamond Platinumz

Juma hili lilianza na uvumi kwamba wapenzi walio na umaarufu mkubwa katika eneo la Afrika Mashariki Tanasha Donna na Diamond wameachana.

Hatua hiyo ilijiri baada ya Tanasha kuchapisha ujumbe katika mtandao wake wa Instagram akiwaonya wanawake wenzake kutovumilia wapenzi 'wanaojihusudu'.

Katika msururu wa machapisho ya mtandaoni, Tanasha alitoa dalili kwamba mambo sio shuari katika uhusiano wake na msanii maarufu katika eneo la Afrika Mashariki Diamond Platinumz.

Aliandika: Watu kama hawa hawana roho na ubinaadamu uliosalia ndani mwao. Ushetani mtupu ni kama kucheza densi na shetani. Tuwasamehe, wawacheni na kumwacha Mungu kukabiliana nao. Watu kama hao kila mara huamini kwamba majuto hayatawafikia hadi yanapowafikia. Mara nyengine unahitaji uzoefu ili kujifunza, ombeni kila siku mara tano kwa siku iwapo itawezekana. Kwasababu kukabiliana na baradhuli ni sawa na kukabiliana na shetani mwenyewe. Lindeni roho zenu, alisema Tanasha.

Chanzo cha picha, DIAMOND PLATINUMZ/FACEBOOK

Maelezo ya picha,

Msanii maarufu Afrika mashariki Diamond Platinumz

Kulingana na uvumi ulioenea katika baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania ni kwamba mtangazaji huyo aliyebadilika na kuwa msanii alilumbana na mamake Diamond alipojaribu kuondoka Tanzania na mwanawe.

''Mungu huwaondoa watu fulani katika maisha yako kwasababu alisikia mazungumzo ambayo hakuyasikia na kuona vitu ambavyo hukuviona''...alichapisha.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao pia wamedai kwamba Tanasha alimuondoa baba ya mwanawe, dadake na mamake miongoni mwa wafuasi wake katika mtandao wa Instagram.

Lakini hata naye Tanasha hakusazwa baada ya baadhi ya watumiaji wa mitandao kudai kwamba walimuonya kutoingia katika uhusiano na Diamond Platimuz.

Lakini cha kushangaza ni kwamba malalamishi yaliochapishwa na Tanasha yanajiri chini ya wiki mbili baada ya wawili hao kutoa kibao cha ushirikiano kwa jina Gere.

Katika kibao hicho kilichotazamwa na zaidi ya watu milioni tano, wawili hao wanaonekana wakiwazomea wale wanaoonea wivu uhusiano wao huku Tanasha akimwambia mpenzi wake kutomdanganya.

Wawili hao hatahivyo hawajaucheza wimbo huo kwa pamoja katika majukwaa na wengi wanahisi kwamba huenda Diamond na Donna wanatumia kiki ya 'kuachana kwao' ili kuweza kuuza muziki huo hata zaidi.

Uchunguzi wetu umebaini kwamba licha ya madai kwamba bi Tanasha alifutilia mbali picha zote za mpenziwe si kweli kwani bado kuna picha za Diamond katika mitandao yake ya kijamii.

Vilevile licha ya machapisho yake chungu nzima, hakuna chapisho la moja kwa moja linaloonesha wazi kwamba Tanasha ametengana na Diamond ama Diamond ametengana na Tanasha.

Ni kutokana na fikra hizo ambapo tunauliza swali Je, Tanasha Dona ameachana na Diamond Platinumz ama ni 'kiki' za kibiashara.

Katika mojawapo ya masuala ambayo yamekuwa yakitumiwa na wasanii kujiuza ama hata kuuza muziki wao ni suala la kutumia kiki.

Kiki ni ugonjwa mbaya sana na kwa bahati mbaya kila msanii anaamini ataweza kufanya vizuri kupitia kiki.

Upande mwengine mashabiki pia wamejengwa kwenye njia ya matamanio ya kusikia habari za familia na matukio binafsi kuliko kazi zao.

Sio kwamba hawatoi kazi nzuri, bali habari za maisha binafsi zina nguvu kuliko uzito wa nyimbo mpya.

Kwa mfano baadhi ya wanamuziki maarufu wamekuwa wakitumia skendo ili mradi kuvutia ufuasi.

Wengine wametumia hata vifo kujipatia wafuasi kama ilivyotokea na msanii raia wa Tanzania Meja Kunta ambaye licha ya kutangazwa kufariki alitoa kibao siku chache baadaye.

Je unakuwaje kwamba siku chache tu baada ya kudai kwamba watu wanawaonea Gere hadharani muwachane?

Maswali yalianza kuulizwa kuhusu uhusiano wao baada ya ndoa yao kuahirishwa mara kwa mara hadi ikawa sio gumzo tena.

Kulingana na dadake Diamond Platinumz , Queen Darleen ambaye alizungumzia kuhusu ndoa hiyo iliokuwa ikisubiriwa na wengi, Diamond hakuwa tayari kufunga ndoa hivi karibuni

Kabla ya uhusiano wake na Tanasha Diamond Platinumz alichumbiana na Zari Hassan mfanyabiashara wa Uganda ambapo walipata watoto wawili.

Wawili hao waliachana siku ya Valentines ambapo zari alituma ujumbe katika mtandao wake wa Instagram akitangaza kuachana na mpenzi wake Diamond.