Waridi wa BBC: Simulizi ya mwanamke aliyetaka kutoa uhai wake na wa watu wengine

  • Anne Ngugi
  • BBC Swahili
Jackie Ruguru
Maelezo ya picha,

Jackie aliolewa akiwa na umri wa miaka 21 ,lakini miaka 7 baada ya kuishi na mumewe ambaye pia ni baba wa watoto wake wawili , ndoa yao iligonga mwamba.

Jackie Ruguru ni mwanamke wa miaka 37 na mama wa watoto wawili ambaye ndoa yake ilivunjika miaka saba iliopita.

Lakini licha ya changamoto ya kiafya inayomkabili amejizatiti kuwalea wanawe pekee yake, jambo ambalo anakiri sio rahisi.

Yeye ni mmoja wapo ya wanawake wachache nchini Kenya ambao wamejitokeza waziwazi kuzungumzia hali inayomuathiri mtu kiakili inayojulikana kama Bipolar 2, ambayo alizaliwa nayo.

Anasema kwamba ishara za hali hiyo zilianza kujitokeza bayana baada ya kujiunga na shule ya sekondari mbali na taasisi ya taaluma.

"Nakumbuka nikiwa shule ya upili nilikuwa msumbufu mno,kiasi kwamba wanafunzi na waalimu walikuwa wananiogopa kwani wakati mwingine ningekuwa na hasira za ghafla zinazonifanya kuonekana kama mtu aliyerukwa na akili "asema Jackie.

Historia yake ya bipolar 2 ilianzia wapi?

Chanzo cha picha, Jackie Ruguru

Maelezo ya picha,

Anadai kwamba alikuwa na tabia zisizo za kawaida hususan kukurupuka bila sababu, akiwa na hasira isiyoeleweka , mbali na tabia nyingine ambazo mtu hawezi kuzihimili .

Jackie aliolewa akiwa na umri wa miaka 21, lakini miaka saba baada ya kuishi na mumewe ambaye pia ni baba ya watoto wake wawili, ndoa yao iligonga mwamba.

Anasema kwamba ndoa yao ilikumbwa na vurugu na dhuluma za hapa na pale hadi ikafikia kikomo.

Anahisi kwamba yote hayo huenda yalichangiwa na hali yake ya kiakili licha ya kwamba yeye na mumewe hawakujua alikuwa na tatizo la kiakili kwa kiasi kikubwa.

Lakini siku moja akiwa katika Taasisi moja tatizo lake lilifichuliwa baada ya mwalimu mkuu kudai kwamba huenda mwanamke huyo alikuwa na tatizo la kiakili.

Mwalimu huyo alidai Jackie alikuwa na tabia zilizoashiria kwamba alikua na tatizo la kiakili kutokana na tabia zake zisizo za kawaida.

Kukutana na mwanasaikolojia

Hatua hiyo iliwafanya wazazi wake kumpeleka kwa mwanasaikolojia ambapo aligunduliwa kwamba alikuwa na bipolar 2 hali ambayo inaathiri akili.

Hatahivyo wazazi wake hawakutaka kumwelezea kilichojhiri baada ya ukaguzi huo wa kimatibabu uliosema kwamba ana tatizo la kiakili.

"Daktari mwanasaikolojia alisema kuwa nitameza dawa kila siku , lakini hawakunieleza ni kwanini nilikuwa nameza dawa. Kwa kipindi cha wiki moja nilizimeza taratibu lakini siku mmoja niliamka asubuhi na kuwaeleza wazazi wangu kuwa nilikuwa nimechoka kumeza dawa ambazo sikujua sababu yake "Jackie alisema

Kando na hayo mwanamke huyo anakumbuka kuwa mwaka wa 2012, 2011 kurudi nyuma maisha yake yalikuwa na kukurukakara kila upande.

Anasema kwamba maisha yake akiwa shule ya upili yalikuwa ya shida na usumbufu mwingi ambao hakuweza kuuelezea chanzo chake .

Anadai kwamba alikuwa na tabia zisizo za kawaida hususan kukurupuka bila sababu, akiwa na hasira isiyoeleweka, mbali na tabia nyengine ambazo mtu hawezi kuzihimili .

Chanzo cha picha, Jackie Ruguru

Maelezo ya picha,

La ajabu kabisa anasema kuwa aliwahi kuliteka nyara basi la shule ya upili na kuliendesha kwa kasi! .

Kwa mfano kila wakati alipokosana na walimu pamoja na wanafunzi wenzake anakumbuka alifukuzwa shuleni mara 14.

Makosa yake yalishirikisha kuwajibu walimu vibaya na kwa hasira mbali na kuanzisha fujo na wanafunzi wengine ambaohata mara nynegine alipigana nao .

La ajabu kabisa anasema kuwa aliwahi kuliteka nyara basi la shule ya upili na kuliendesha kwa kasi!.

Jingine la kushangaza ni kwamba kuna wakati mmoja alimfukuza mwalimu wake mbio za paka na panya huku akiwa na hasira nyingi chuoni humo.

Pia katika utu uzima wake alikuwa na matatizo mengi sana. Kwa mfano aliwahi kuchukua mkopo wa dola elfu nane na kuzitumia vibaya kwa anasa na baada ya siku tatu zilikuwa zimekwisha.

"Nakumbuka kuwa nilimpa mama aliyekuwa anaomba fedha barabarani 500 "alisimulia Jackie

Na sio hayo tu uhusiano wake na wenye nyumba kama mpangaji ulikuwa na tatizo kubwa. Anakiri kuwa wakati mwingi alikuwa anazua fujo kila inapofikia mwisho wa mwezi na hata kuwatia hofu wamiliki wa nyumba alizokodisha.

Je kwanini aliamua kutoa uhai wake na wa watu wengine?

Jackie anasema kuwa alikuwa anahisi kana kwamba maisha yalikuwa yameanza kumlemea akitizama msururu wa matukio ya maisha yake.

Anasema kuwa alikuwa haoni ladha ya kuishi tena na kwamba msongo wa kiakili na muelekeo wa maisha yake pia ulikuwa haumridhishi .

Ni wakati hupo ndiposa alianza mpango wa kile aliochokitaja kama kutaka kusitisha maisha yake .

"Mpango wangu ulikuwa nijitoe uhai kwa sababu sikuona raha ya maisha tena , nilikuwa msumbufu sana na watu waliokuwa karibu nami walikuwa wananiogopa sana " aliongezea Jackie

Chanzo cha picha, Jackie Ruguru

Lakini mpango wake wa kujitoa uhai haukufua dafu , kwani rafiki yake wa karibu alipiga simu wakati alipokuwa katika maandalizi ya kuchukua hatua hiyo.

Anasema kwamba licha ya kujuta hatua ya kupanga kujitoa uhai pamoja na watu waliokaribu naye, ni kutokana na fikra hizo ambapo maono ya kuunda shirika ambalo linawasaidia watu wanaoishi na ugonjwa wa kiakili yalianza .

Jackie sasa amekubali hali yake na anaitumia kama jukumu la kuhamasisha umma kuhusu magonjwa ya tofauti ya kiakili.

Anaongezea kuwa maisha ya kisasa yenye shughuli nyingi si haba ambayo hutukuza utajiri na fedha , yamewafanya watu kufanya mambo ya ajabu ili kujipatia sifa na utajiri na pindi hilo linapokosa kuafikiwa wengi hukosa tamaa ya kuishi tena .

Katika shirika ambalo Jacky analisimamia anasema kuwa washiriki wengi ni vijana kutoka vyuo vikuu ambao wanaendeleza elimu na pia kutoa nasaha kwa jamii kuelewa magonjwa ya kiakili .

Je bipolar 2 ni nini haswa?

Chanzo cha picha, Elvis Osimbi

Maelezo ya picha,

Mwanasaikolojia Elvis Osimbi

Kulingana na Mwanasaikolojia Elvis Osimbi , kutoka Nairobi Kenya, Bipolar ni ugonjwa sugu ambao huathiri jinsi akili ya binadamu inavyofanya kazi huku kukiwa na dalili nyingi tofauti, kwa mfano: -

Kuwa na tabia ambazo sio za kawaida kama vile hasira iliyopita kiasi , kuharibu vitu na kuzua fujo.

Mara nyengine wanaougua ugonjwa huo hupata ndoto au vitu ambavyo sio vya ukweli.

Dalili za Bipolar pia zinajumuisha furaha nyingi, msisimko na wakati mwengine kutokuwa na utulivu, kupata haja ndogo wakati wa kulala na kuwa na mawazo mengi kwa wakati mmoja.

Lakini pia kunazo dalili za unyogovu, kama vile huzuni, wasiwasi, kulia bila sababu hasira ya kupindukia na mawazo ya kujidhuru au kudhuru watu wengine .

Bipolar huweza kutibiwa tu kupitia mwanasaikolojia kulingana na mwanasaikolojia Elvis Osimbi na wakati mwingi wagonjwa uhitaji kunywa dawa kila siku huku wengine wakilazimika kutumia dawa hizo hadi mwisho wa maisha yao.