Uchaguzi wa Tanzania 2020: Ndoto ya urais ya Membe imeota mbawa?

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania
Bernard Membe

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bernard Membe aligombea tiketi ya urais ndani ya CCM 2015 mchakato ambao uliisha kwa John Magufuli kupata ridhaa ya chama.

Benard Camilius Membe amefukuzwa uanachama wa chama tawala CCM huku ndoto yake ya kugombea urais kupitia chama hicho ikitoweka.

Membe yuko huru kujiunga na chama kingine cha siasa endapo kutimiza ndoto yake ya kuwania urais kama walivyowahi kufanya waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyehamia Chadema wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 na waziri wa zamani wa mambo ya ndani na Naibu waziri Mkuu, Augustine Mrema aliyehamia chama cha NCCR-Mageuzi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Membe amefukuzwa baada ya kuhojiwa mwezi uliopita na Kamati ndogo ya Maadili, Udhibiti na Nidhamu ya CCM mjini Dodoma akituhumiwa utovu wa nidhamu,kumhujumu mwenyekiti wa CCM na nia ya kugombea urais mwaka 2020 kinyume cha utamaduni hali ambayo imeibua mjadala iwapo uamuzi wa chama hicho umebariki mwisho wake kisiasa au ataibuka kivingine.

Rekodi zinaonesha kuwa Membe amewahi kuadhibiwa na chama hicho tawala mwaka 2014 kwa makosa ya utovu wa nidhamu na kukiuka taratibu kuanza kampeni za urais ndani ya chama kabla ya wakati kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 sambamba na wanasiasa Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Aidha, mwanasiasa huyo mkongwe na waziri wa zamani wa mambo ya nje aliyedumu kwa kipindi cha miaka nane katika uongozi wa awamu ya nne chini ya rais mstaafu Kikwete, ametajwa kuwa si tishio kisiasa.

Lakini amepanda chati ya umaarufu siku za karibuni kutokana na makosa ya CCM ambao wamemgeuza kuwa ajenda katika mikutano mbalimbali ya hadhara ya shughuli za chama wakiongozwa na Katibu mkuu, Dk.

Bashiru Ally aliyebainisha kuwa Membe alikuwa na mwenendo wa kutia shaka ndani ya chama hicho na akaagiza afike ofisi za chama hicho jijini Dar es salaam kujitetea na tuhuma zinazomkabili.

Uamuzi wa CCM kumvua uanachama Membe umechochewa pia na matamshi aliyotoa baada ya kuvuja kwa sauti za mazungumzo yake katika mitandao ya kijamii na kukiri kuwa ni yeye, akishangazwa na kuporomoka kwa umaarufu wa Rais Magufuli, kudorora uhuru wa kujieleza na mahusiano ya kimataifa.

Je ni mwisho wa kisiasa wa Membe?

Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM na serikali, amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa, "Membe alishakwisha kisiasa tangu kumalizika kwa kura za maoni kuwania uteuzi ndani ya CCM mwaka 2015.

Alichokuwa anafanya sasa ni kutafuta relevancy au kiki ya kumfanya aonekane bado yumo na bahati mbaya akakanyaga waya. Kimsingi CCM ilifanya makosa kumpa jukwaa la kuonekana, isingevuja ile Clip ya mazungumzo wala kusingekuwa na mjadala wa Membe duniani kwa sasa.

Alikuwa ameshasahaulika, na sasa ameonesha dhahiri anahusudu kuonekana yupo kisiasa."

Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora anasema, "Simuoni Membe mwenye ushawishi kisiasa nje ya chama chake na bahati mbaya zaidi eneo analotoka halina mwamko wa siasa za upinzani.

Hivyo hata akijiunga na upinzani bado hana mtaji wake binafsi kuanzia eneo lake la nyumbani.

Anapaswa kukubali na kutulia tu astaafu kimya kimya lakini si kuhangaika na upinzani maana kwa mifumo yetu ya chama dola si rahisi kwa sasa CCM kupoteza nafasi ya urais.

Membe angekuwa na nafasi kama angebaki ndani ya CCM na hasa kama chama kingekuwa na nguvu kwa wanachama wake kiasi kwamba angeweza kuwatumia wenzake kadhaa kumkingia kifua lakini si kwa sasa ambapo hata uanachama hana."

Je ana nguvu kiasi gani ndani na nje ya CCM?

Wakati wa kinyang'anyiro cha kuwania uteuzi wa urais ndani ya CCM mwaka 2015, Membe alifanikiwa kutinga tano bora sambamba na Balozi Amina Salum, January Makamba, Dk. Asharose Migiro na John Magufuli. Hatua hiyo ilimjengea wafuasi wengi ndani na nje ya chama tawala.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema kutimuliwa kwa Membe na kuwa nje ya CCM kutaonesha iwapo mwanasiasa huyo ni tishio na ana nguvu kiasi gani au atakuwa amechimbiwa shimo la kutumbikia.

Hoja hiyo inashadadiwa kutokana na matamshi ya Membe kuwa anao watu wake serikalini, idara za usalama na ndani ya CCM.

Frank Banka, mchambuzi wa siasa na utawala bora nchini Tanzania, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Membe, hakuwahi kuwa mwanasiasa tishio ndani ya nchi hii bali ukubwa wake ulitokana na mambo makuu mawili.

"Moja, uamuzi wa Jakaya Kikwete kumpa nafasi katika uongozi, na zaidi ni ile propaganda ya kuonekana ndugu wa Kikwete ndio ilimpa nafasi ya kuwa maarufu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliokuwa na hekaheka nyingi ndani ya CCM.

Maelezo ya picha,

Magufuli (kushoto) na Membe (kulia) walikuwa ni miongoni mwa makada wa CCM waliochuana kuwania tiketi ya urais 2015

"Pili, alizidi kukua baada ya uchaguzi mkuu 2015 kwa baadhi ya wanachama wa CCM waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa, sasa baada ya huyo kuhamia Chadema wale waliobaki walikosa mtu wa kumuunga mkono hivyo kuamua kujiunga na siasa za kumkuza Membe.

Amenufaika na upepo wa kisiasa kutoka kundi kinzani na ambalo lilikuwa linaamini kwa kufanya hivyo kutampunguzia nguvu Rais Magufuli,"

Anaongeza kwa kusema, "Huu ndiyo mwisho wa Membe kisiasa hata kama ataamua kujiunga chama cha upinzani bado hatakuwa na nguvu kisiasa kwani nguvu yake ilitengenezwa na upepo wa kisiasa ulioamua kuvuma kwake kwa wakati huu na upepo huu ulikuwa kwa wale wanaoamini ndio muarobaini wa kumpa misukosuko kisiasa Magufuli,"

Je, Membe atafuata nyayo za Lowassa, Mrema?

Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi, ulitawaliwa na hekaheka nyingi za kisiasa huku jina la Augustine Lyatonga Mrema likitawala vyombo vya habari, siasa, mitaani na kote nchini tangu kutangaza kuhama CCM.

Kwa mujibu wa Profesa T.L Maliyamkono kwenye kitabu chake cha "The Race for the Presidency: The first multiparty democracy in Tanzania (1995), ameeleza kuwa Mrema alikuwa tishio la ndani na nje ya CCM.

Mara baada ya rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri ikiwemo kumwondoa waziri mkuu John Malecela na kumteua Cleopa Msuya, ambayo yalimwathiri pakubwa Mrema.

Anaongeza kuwa, ndani ya CCM Mrema alitengwa na baadaye kuonekana ni tatizo licha ya juhudi zake za kupambana na rushwa pamoja na kuikosoa serikali ili irekebishe matatizo, hivyo akawa hana chaguo jingine zaidi ya kujitoa na kujiunga upinzani.

Chanzo cha picha, IKULU, TANZANIA

Maelezo ya picha,

Baada ya Lowassa (kulia) kukatwa kwenye kinyang'anyiro cha CCM alihamia Chadema na kushindana tena na Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa 2015.

Tishio la Mrema linathibitishwa na matokeo rasmi ya NEC, ambapo mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa alishinda uchaguzi huo kwa jumla ya kura 4,026,422 sawa na asilimia 61.82.

Naye Agustine Mrema (NCCR-Mageuzi) alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,808,516 sawa na asilimia 27.77.

Msuguano wa Mrema na viongozi wenzake wa CCM na serikalini ni sawa na wa Lowassa na CCM ambapo hakuridhika na uamuzi wa chama hicho kukata jina lake hatua za awali kuwania kuteuliwa kugombea urais.

Aidha, migogoro hiyo ndiyo ilichochea Mrema na Lowassa kwa nyakati tofauti kukihama CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, NCCR-Mageuzi na Chadema.

Wanasiasa wote wawili wameweka rekodi ya kuwa wagombea wa urais wa upinzani waliopata kura nyingi zaidi.

Lowassa alipata takribani kura Milioni 6 na Mrema kura milioni moja na laki nane na mia tano kumi na sita kwa kigezo cha uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Wachambuzi wa siasa wanauliza swali moja kuu; Je, kwa mazingira hayo Membe ataamua kutumia uzoefu wa wanasiasa wenzake waliohamia upinzani na kuichachafya CCM?

Vilevile, Membe pia anaweza kuziba pengo lililoachwa wazi na Lowassa ndani ya upinzani?

Ikumbukwe, waziri mkuu mstafau mwingine Frederick Sumaye naye alikihama CCM na kujiunga na upinzani mwaka 2015 kabla ya mwaka huu 2020 kurejea chama hicho.

Je, Membe ataweza kuomba radhi CCM?

Sophia Simba ni miongoni mwa wanachama wa daraja la juu CCM ambaye alifukuzwa uanachama chini ya uenyekiti wa Magufuli kutokana na madai ya kukihujumu chama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Sophia alifukuzwa pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Mary Msambatavandu.

Hata hivyo Sophia Simba aliomba msamaha, na kuomba kurudishiwa uanachama wake wa CCM.

Kiongozi mwandamizi wa CCM na serikalini amesema, "Vinginevyo tukubali CCM ni kubwa kuliko mwanachama wake yeyote.

Hivyo kwa sasa Membe akiomba msamaha na kurudishiwa uanachama anayo miezi 48 ya matazamio.

Asipofanya hivyo ataishia kama walikoishia akina Agustine Mrema na wengineo waliotoka CCM,"

CCM kufukuza wanachama wanaompinga rais?

Kadiri miaka inavyokwenda ndivyo wanasiasa ndani ya CCM wamekuwa wakiibuka kila mara kutamani kupambana na Rais anayetakiwa kupitishwa bila kupingwa mara baada ya kutumikia miaka mitano.

Wenye matamanio kama Bernard Membe wanashindwa kunyukana na mwenyekiti wao kwakuwa 'utamaduni' wa CCM unasema hapingwi.

Je ni wakati wa CCM kubadili utaratibu kuwaruhusu wanachama wake kupambana na rais anayeomba ngwe ya pili?