Virusi vya corona: Shirika la fedha duniani kukabiliana na janga kiuchumi

International Monetary Fund Managing Director Kristalina Georgieva.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mkurugenzi wa shirika la fedha duniani, IMF Kristalina Georgieva

Shirika la fedha duniani (IMF) limetangaza kutoa dola bilioni 50 kuzisaidia nchi zilizoathirika na virusi vya corona.

Shirika hilo limetoa onyo kuwa mlipuko wa corona tayari umeathiri ukuaji wa kiuchumi wa mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana .

Hatua za dharura zimeanza baada ya virusi hivyo kusambaa nje ya China na kuzifikia zaidi ya nchi 70.

Wiki hii benki ya dunia imechukua hatua ya kupunguza makali ya matokeo ya virusi hivyo.

IMF ilisema kuwa inatoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia nchi maskini na kipato cha kati ambazo mifumo ya huduma zao za afya iko chini.

Wakati huohuo , ufadhili huo utasaidia kukabiliana na janga la kiuchumi kwa sababu kusambaa kwa virusi hivyo kumepelekea uchumi wa dunia kuyumba zaidi mwaka huu wakati janga hilo la kifedha lilianza kushuka taratibu tangu mwaka 2008.

Lakini mkurugenzi wa IMF Kristalina Georgieva ametoa onyo kuwa si rahisi kujua madhara yatakuwa makubwa kiasi gani: "Ukuaji wa kiuchumi duniani kwa mwaka 2020 utashuka ukilinganisha na mwaka jana".

Vilevile alikwepa kusema kuwa janga hili la kiafya linaweza kusababisha uchumi wa dunia kushuka.

Hizi ni hatua za sasa ambazo mashirika ya fedha yameamua kuchukua ili kulinda uchumi kutokana na matokeo ya mlipuko wa virusi vya corona.

Siku ya Jumanne benki kuu ya Marekani ilipunguza kiwango cha riba ikiwa ni hatua ya kupunguza mzigo wa athari za kiuchumi kutokana na virusi vya corona .

Hii ni hatua ya kwanza ya dharura ya kupunguza kiwango cha riba tangu janga la kifedha lianze mwaka 2008.

Siku hiyo hiyo Australia na Malaysia walipunguza kiasi cha riba kutokana na mlipuko huo.

Mawaziri wa fedha kutoka mataifa makubwa duniani ya G7 wamehaidi kuweka sera nzuri abazo zinaweza kukabiliana na athari hizi za kiuchumi zilizotokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Wiki hii pia ,benki ya dunia imehaidi kutoa msaada wa dola bilioni 12 kwa mataifa yanayoendelea kukabiliana na maambukizi ya corona.

Msaada huo wa dharura unajumuisha mikopo ya gharama za chini, ufadhili na msaada wa kiteknolojia.

"Tunataka kujaribu kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu," rais wa World Bank Group t David Malpass aliiambia BBC.

Maambukizi mapya barani Afrika kwa sasa ni watu 26:

Algeria yameongezeka na kufika watu 17

Senegal - watu wanne

Misri - watu wawili

Morocco - mtu mmoja

Nigeria - mtu mmoja

Tunisia - mtu mmoja