Ni kwanini kifo cha mlinzi wa William Ruto, Sajini Kenei kinaibua maswali?

Mkurugenzi wa Idara ya upelelezi, Goerge Kinoti amesema kwamba Sajini Kemei aliuawa kikatili, kinyume na habari za awali kwamba alijiua mwenyewe.

Chanzo cha picha, DCI/Twitter

Maelezo ya picha,

Mkurugenzi wa Idara ya upelelezi, Goerge Kinoti amesema kwamba Sajini Kemei aliuawa kikatili, kinyume na habari za awali kwamba alijiua mwenyewe.

Utata unaozingira kifo cha Sajini Kipyegon Kenei, aliyekuwa mkuu wa usalama katika ofisi ya Naibu Rais wa Kenya Dkt William Ruto unaendelea kuzua maswali mengi kuliko majibu baada ya idara inayochunguza uhalifu (DCI) kudai kwamba kuuawa kwa polisi huyo kunahusiana na matukio katika ofisi ya kiongozi huyo.

Mkurugenzi wa Idara ya upelelezi, Goerge Kinoti amesema kwamba Sajini Kemei aliuawa kikatili, kinyume na habari za awali kwamba alijiua mwenyewe.

Mwili wa Kenei ilipatikana nyumbani kwake

Mwili wa Sajini Kenei ulipatikana nyumbani kwake wiki mbili zilizopita ukiwa na jeraha la risasi. Kulingana na taarifa ya polisi, marehemu alijiua.

Kifo cha askari huyo kilitokea wakati ambapo alitakiwa kuandika taarifa ya maelezo kwa polisi kuhusu washukiwa wa sakata ya zabuni hewa ya ununuzi wa silaha za mamilioni ya pesa walipotembelea ofisi ya Dkt Ruto mjini Nairobi.

Kifo cha Sajini Kenei kimezua mjadala mkali nchini Kenya huku baadhi ya watu wakisema huenda mlinzi huyo aliuawa mahali tofauti na mwili wake ukapelekwa nyumbani kwake ili kwa lengo la kuficha ukweli juu ya uhalisi wa kilicho muua.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Naibu rais wa Kenya anakana kuhusika na madai ya ununuzi wa silaha hewa

Kabla ya mwili wa afisa huyo kupatikana, ofisi ya Dkt Ruto ilikuwa imetoa taarifa ikisema kwamba alikuwa ametoweka.

Mbali na kutilia shaka maelezo ya polisi, Wakenya mitandaoni hawakuridhishwa na hatua ambazo ofisi ya Dkt Ruto ilichukua pale Sajini Kenei alipokosa kufika kazini badaye na kujiwasilisha kwa wapelelezi kuandikisha taarifa.

Zabuni hewa ya silaha yalipuka

Mkuu wa DCI George Kinoti alisema awali kwamba, Sajini Kenei alitakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi kueleza jinsi aliyekuwa waziri wa michezo, Rashid Echesa na washukiwa wengine wanne walivyowaingiza raia wa kigeni katika ofisi ya Dkt Ruto, na hata kutia sahihi kandarasi feki ya kuuzia wizara ya ulinzi silaha.

Kwa mujibu wa Bwana Kinoti ambaye alionyesha wanahabri picha zilizochukuliwa na camera za kisiri yaani CCTV, Sajini Kenei anaonekana akiwafungulia mlango na kuwaelekeza Bw Echesa na ujumbe wake katika ofisi ya Naibu Rais.

Chanzo cha picha, ERashid Echesa /Twitter

Maelezo ya picha,

Rashid Echesa (kulia) akiwa na Naibu rais wa Kenya Dkt. William Ruto, anashutumiwa kupokea dola 395,442,000 kutoka kwa wafanyabiashara wa Poland akiwaahidi zabuni hewa

Bwana Echesa, mwandani wa karibu wa Dkt Ruto, ameshtakiwa kwa kujaribu kujipatia dola za Marekani 395, 442,000 kutoka kwa wafanyabiashara wa Poland kwa kuwaahidi zabuni ya kuiuzia idara ya ulinzi ya Kenya vifaa vya kijeshi.

Dkt Ruto ajitetea vikali

Dkt Ruto ameshutumiwa sana kufuatia kesi hiyo, huku viongozi wengine wakihoji vipi ulaghai wa hali ya juu unaweza kufanyika katika 0fisi yake bila yeye kujua.

Kwa upande mwingine, Naibu huyo wa rais Bwana Ruto ameshutumu ripoti hizo kama porojo zenye hila.

Dkt Ruto amejitetea vikali kwamba hakukutana na waziri huyo wa zamani wa michezo Bwana Echesa pamoja na wafanyabiashara wake waliotembelea ofisi yake na hakuhusika katika mkataba huo bandia uliodaiwa kugharimu dola milioni 397.

Ingawa inaonekana kifo cha aliyekuwa mkuu wa usalama katika ofisi ya Naibu Rais wa Kenya kinachukuwa mkondo wa kisiasa, wengi wanafuatilia sakata hiyo kwa umakini mkubwa wakitaraji kwamba ukweli utapatikana.