Shiekh Mohammed Al Maktoum: Je mtawala huyu wa Dubai ni mtu wa aina gani?

Sheikh Mohammed Al Maktoum (Disemba 10 2019)

Chanzo cha picha, AFP

Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum ni matawala wa Dubai ,bilionea na makamu wa rais wa milki za kiarabu UAE.

Katika eneo la mashariki ya kati anajulikana kwa kusimamia mabadiliko ya Dubai kuwa kituo kikuu cha biashara na utalii duniani.

Kwengineko anajulikana sana kwa kuhusika katika uendeshaji wa farasi na kuwa mmiliki wa Godolphin stables.

Amegonga vichwa vya habari baada ya kupatikana na mahakama kuu mjini London kuwateka nyara na kuwalazimisha watoto wake wa wawili wa kike kurudi Dubai, na kufanya kampeni ya vitisho dhidi ya mkewe wa zamani , bintimfalme Haya.

Sheikh Mohammed alizaliwa 1949 nyumbani kwao huko katika eneo la Shindagha, karibu na mkondo wa bahari wa Dubai.

Alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto wanne wa Sheikh Rashid Al Maktoum , ambaye aliitawala Dubai kwa miaka 32 tangu 1958.

Baada ya kumaliza shule ya upili 1965, Sheikh Mohammed alihamia Uingereza katika shule ya masomo ya lugha huko Cambridge.

Sheikh huyo aliyekuwa na umri mdogo baadaye alihudhuria mafunzo ya miezi sita katika jeshi la Uingereza kama kadeti mjini Hampshire.

Mwaka 1968, baada ya kurudi Dubai, Shekih Mohammed aliandamana na babake katika mkutano na mtawala wa wakati huo wa Abu Dhabi Sheikh Zayed Al Nahyan, ambapo walikubali kufanya muungano ambao ulipelekea kuundwa kwaMuungano wa milki za kiarbu.

Baada ya UAE kupata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1971, Sheikh Mohammed aliteuliwa kuwa waziri wa ulinzi - wadhfa ambao hadi wa leo anaushikilia.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Mamia ya majumba ya ghorofa Dubai

Sheikh Mohammed pia alihusishwa katika mpango wa babake wa kufidia upungufu wa hifadhi ya mafuta Dubai kupitia kuimarisha uchumi wake na kulifanya eneo hilo kuwa kituo cha biashara pamoja na utalii duniani.

Hii leo zaidi ya asilimia 95 ya mapato ya milki za kiarabu hayatokani na mafuta huku utalii ukichangia asilimia 20.

Idadi ya watu nchini Dubai imeongezeka kutoka 40,000 katika miaka ya sitini hadi milioni 3.3 , ikiwemo watu milioni 3.1 ambao hawatoki katika milki hiyo ya kiarabu, wengi ambao wanaishi katika mamia ya majumba marefu katika mji huo.

Mwaka 1990, Sheikh Rashid alifariki baada ya ugonjwa wa muuda mrefu uliotokana na kiharusi.

Alirithiwa na nduguye mkubwa Mohammed , Maktoum. Miaka mitano baadaye . Sheikh maktoum alitajwa kuwa mwanamfalme wa Dubai. Pia alijipatia kazi ya uendeshaji wa maswala ya kila siku ya Dubai.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Sheikh Mohammed alimrithi nduguye mkubwa Sheikh Maktoum (kushoto) kama mtawala wa Dubai 2006

Sheikh Mohammed alikuwa mtawala wa Dubai , makamu wa rais na waziri mkuu wa UAE 2006, baada ya nduguye aliyekuwa na umri wa miaka 62 kufariki wakati wa ziara yake Australia.

Chini ya uongozi wake Dubai iliendelea kuimarika. Mwaka 2008, Muungano wa Milki za kiarabu UAE ulizindua jumba refu zaidi duniani Burj Khalifa.

Miradi kama hiyo ya maendeleo , ilitegemea pakubwa mabilioni ya madola.

Mzozo wa kifedha ulifanya soko la nyumba Dubai kuanguka na mwaka 2009 kampuni zilizokuwa zikihusishwa na umilki wa serikali karibu zikatae kulipa madeni.

Abu Dhabi iliingilia kati na kuipatia mkopo serikali ya Dubai fedha ilizokuwa ikizitaka sana. Ujenzi wa Dubai pia ulitegemea wafanyakazi kutoka mataifa ya kigeni , ambapo wengi walilalamika walikuwa wakitumiwa vibaya.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Sheikh Mohammed alianzisha timu kubwa ya waendesha farasi duniani , Godolphin

Sheikh Mohammed pia amekuwa maarufu kwa kuhusika kwake katika mashindano ya kuendesha farasi ambapo pia anasifika kwa kuyabadilisha kuwa sekta kubwa duniani.

Aliendesha farasi katika fukwe za bahari mjini Dubai akiwa mtoto na alizinduliwa katika mchezo huo 1967 nchini Uingereza.

Miaka kumi baadaye alisherehekea ufanisi wake kama mmiliki. Kiongozi huyo alizindua kundi kubwa zaidi la waendesha farasi duniani Godolphin , pamoja na shirika la uzalishaji wa farasi aina ya Stalion , Darley.

Godolphoin ambayo ina vifaa katika UAE , England , Jamhuri ya Ireland , Australia, Japan na Marekani ilishinda michezo 6000 kote duniani tangu 1992.

Sheikh Mohammed mara kwa mara uhudhuria mashindano ya kundesha farasi kama vile yale ya Royal Ascot, ambapo amepigwa picha na malkia Elizabeth wa pili.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bintimfalme Haya na Sheikh Mohammed walihudhuria mara kwa mara mashindano ya farasi ya Royal Ascot

Sheikh Mohammed waligawana farasi na mkewe wa sita na mdogo kabisa bintimfalme Haya bint- al -Hussein , mwana wa aliyekuwa mfalme wa Jordan na dadake wa kambo mfalme Abdullah wa pili.

Wawili hao walifunga ndoa 2004 na walikuwa na watoto wawili, Al Jalila na Zayed.

Katika mahojino yake bintimfalme Haya alionyesha kwamba maisha yao yalikuwa mazuri, lakini mgawanyiko ulianza kuonekana 2018 wakati Sheikha Latifa mmoja ya watoto wakubwa wa Sheikh Mohammed aliomzaa na mke mwengine , alijaribu kutoroka UAE kwa usaidizi wa aliyekuwa mpepelezi wa zamani wa Ufaransa na mkufunzi wa mazoezi ya kimwili.

Boti iliokuwa ikiwabeba ilizuiwa baharini katika pwani ya India na Sheikha Latifa alirudishwa Dubai.

Katika kanda ya video , alidai kwamba alikuwa amefungwa kwa zaidi ya miaka mitatu na kunyanyaswa baada ya jaribio jingine la kutoka 2002 kugonga mwamba.

Washirika wa Sheikha Latifa walisema kwamba anazuiliwa chini ya kifungo cha nyumbani . Lakini serikali ya Dubai ilisisitiza Sheikha Latifa amekuwa akinyanyaswa na sasa alikuwa salama.

Makhtoum hakutoa tamko la kuvunjika kwa ndoa yake , lakini aliandika shairi kali akimshutumu mwanamke asiyejulikana kwa usaliti na kuchapisha katika mtandao wake wa instagram.

Mwezi Julai, bintimfalme Haya aliwasilisha ombi la kutaka kulindwa kutokana na ndoa ya lazima katika mahakama kuu ya London - pamoja na ulinzi wa watoto wake .

Sheikh Mohammed naye aliwasilisha ombi la kutaka watoto wake warudishwe Dubai. .

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bintimfalme Haya alitoroka Uingereza mwaka uliopita na watoto wao wawili

Miezi minane baadaye , mahakama kuu ilitoa msururu wa maamuzi yaliosema kwamba Sheikh Mohammed aliagiza na kupanga njama ya kurudishwa kwa lazima kwa Sheikha Latifa 2002 na 2018 pamoja na kutekwa nyara kinyume na sheria kwa dadake mkubwa Sheikha Shamsa 2000.

Sheikha Shamsa aliitoroka mali ya familia hiyo huko Surrey mwaka huo lakini baadaye alikamatwa katika eneo la Cambridgeshire na maajenti wa kiongozi huyo na kurudishwa Dubai kwa lazima.

Ombi la polisi wa Cambridgeshire kuzuru Dubai ili kufanya uchunguzi lilikataliwa.

Mahakama ilibaini kwamba Sheikh Mohammed anaendelea kuendesha utawala ambapo wanawake wote wawili wanayimwa haki yao ya kuwa na uhuru.

Pia inasema kwamba bintimfalme Haya ambaye alikuwa na uhusiano wa nje ya ndoa na mlinzi mmoja , kwa sasa alikuwa anaishi kwa hofu ya maisha yake baada ya kupata vitisho kadhaa vya kifo huko Dubai na London .

Hii ni baada ya bunduki kuwekwa katika mto wake wa kulalia.

Sheikh Mohamed alipinga uamuzi uliotolewa na akawasilisha ombi la kukataa rufaa ya kuweka faragha maswala yao.