Benki ya dunia yaitaka Tanzania kutowabagua wanafunzi wajawazito

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye pia anashughulikia masuala ya Afrika Mhe. Tibor Nagy mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Washington,Marekani
Maelezo ya picha,

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye pia anashughulikia masuala ya Afrika Mhe. Tibor Nagy mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Washington,Marekani

Benki ya dunia imeishinikiza serikali ya Tanzania kuanzisha mfumo wa elimu kwa wananfunzi wanaokatiza masomo yao kutokana na sababau kama vile uja uzito.

Ikuzungumza katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya benki hiyo na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi, benki hiyo imesema kwamba inafuatilia kwa karibu maswala yote yanayoendelea nchini Tanzania na kwamba itaendelea kushirikiana na taifa hilo katika maswala ya elimu.

Akizungumza katika mkutano huo mkurugenzi wa benki ya dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist amesema benki hiyo inavutiwa na mambo ya maendeleo yanayofanywa na serikali ya Magufuli katika utoaji wa elimu ya bure kwa shule za msingi na sekondari.

Hatua hiyo inajiri siku chache tu baada ya Benki ya Dunia kuahirisha kupiga kura kuhusu mkopo wa dola milioni 500 kwa Tanzania zilizokuwa zikilenga miradi mbalimbali ya elimu.

Kura hiyo ilikuwa inatarajiwa kupigwa tarehe 28 mwezi Januari , lakini tayari kulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa maoni juu ya benki hiyo iidhinishe mkopo huo kwa Tanzania ama la.

Taarifa za kuahirishwa kwa kura hiyo zilijiri siku chache baada ya shinikizo kutoka kwa wanaharakati wa Tanzania na wa kimataifa waliokuwa wakiitaka benki hiyo isitoe mkopo huo kwa serikali kutokana na kile walichokiita kuwa ni sera na sheria ya elimu ya kibaguzi.

Maelezo ya picha,

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akikabidhi ujumbe maalum wa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwenda kwa Rais wa Marekani Doland Trump. Anayeshuhudia ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi

Kwa mujibu wa nyaraka za Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine, mkopo huo ulikusudiwa kwenda kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi waliokuwa wanarudi shule baada ya kuwa wamepata ujauzito.

Lakini Katika mkutano viongozi hao pia walizungumzia masuala mbalimbali ya miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu mbali na maeneo ambayo Benki hiyo imeisaidia Tanzania aidha kwa mikopo ya masharti nafuu au misaada ikiwa ni pamoja na ujenzi na uendelezaji wa shule za msingi na sekondari.

Maelezo ya picha,

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa na Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist katika makao makuu ya Benki ya Dunia Washington,Marekani.Nyuma ya Prof. Kabudi ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi

Mkurugenzi Mtendaji mbadala wa Kanda Namba 1 ya Afrika kutoka Benki ya Dunia Bw. Taufila Nyamadzabo amesema mazungumzo baina ya Tanzania na benki ya dunia yamekuwa ni ya manufaa kwa kuwa yameondoa sintofahamu iliyokuwepo kati ya pande hizo mbili na kwamba mradi huo utapitishwa na bodi ya benki ya dunia hivi karibuni.

Mkopo huo uliotarajiwa kutolewa na Benki ya Dunia ulitarajiwa pia kugharamika wanafunzi wajawazito kupitia elimu mbadala na si katika mfumo rasmi.

Swala hilo lilizua utata na kuwasukuma wanaharakati wa Tanzania kuiandikia bodi ya utendaji ya Benki ya Dunia ikiwa benki hiyo itaipa Tanzania mkopo huo, kabla ya nchi hiyo haijaahidi kuondoa sera na kipengele cha sheria kinachowakataza wanafunzi wa kike kurudi shuleni baada ya kujifungua.

Maelezo ya picha,

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Donald Wright (aliyevaa tai nyekundu) Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi

Kwa mujibu wa shirika la habari la CNN la nchini Marekani, hakuna sababu rasmi iliyotolewa kuhusu kuahirishwa kwa kura hiyo japo inaripotiwa kuwa uongozi wa benki hiyo ulifanya kikao cha dharura na wanaharakati wa haki za binaadamu kutoka Tanzania na mashirika ya kimataifa .

Sheria ya elimu ya Tanzania imebeba kipengele cha nidhamu ambacho kinaipa mamlaka uwezo wa kuwafukuza shuleni wasichana wanafunzi wanaogundulika kuwa na ujauzito.

Hatahivyo hatua yetu ya kumtafuta mwakilishi wa benki hiyo nchini Tanzania kutoa tamko lake haikufua dafu.