William Ruto: Naibu wa rais Kenya adai idara ya jinai 'inatumiwa' kumkabili kisiasa

William Ruto

Chanzo cha picha, Afisi ya naibu rais

Maelezo ya picha,

Naibu wa rais nchini Kenya William Ruto akitoa heshima zake za mwisho kwa Sajenti Kenei aliyekuwa mlinzi wa afisi yake

Naibu wa rais wa Kenya William Ruto amesema kwamba Idara ya jinai nchini Kenya inatumika kumkabili kisiasa.

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya marehemu Kiyegon Kenei , Ruto alimtaka Mkurugenzi wa idara hiyo kuangazia maswala ya polisi na sio siasa.

"Nataka kumwambia mkurugenzi wa idara ya jinai DCI awachane na siasa, angazia kazi ya polisi na kupata chanzo cha ni nani aliyemuua afisa wa Polisi Kenei'', alisema.

Kiongozi huyo amesema kwamba yuko tayari kukabiliana na wale wanaopanga njama ya kumuangusha kisiasa.

Wakati huohuo , alijitenga na sakata ya shilingi bilioni 39 kuhusu vifaa vya kijeshi akisema kwamba vidole vinaelekezwa katika afisi yake huku washukiwa wa sakata hiyo wakiendelea kuwa huru.

"Afisi yangu haina uhusiano na Idara ya ulinzi DOD , hatununui bunduki katika ofisi yangu, hii ni njama ya kunikandamiza , hakuna anayewalenga wahusika kila kitu kimeelekezwa katika afisi yangu''.aliongezea.

Chanzo cha picha, Afisi ya naibu wa rais

Maelezo ya picha,

Naibu wa rais Dkt William Ruto akimpatia pole mjane wa marehemu wakati wa ibada ya mazishi ya sajenti Kenei

Aliahidi kawamba hatopumzika hadi wauawaji wa Kenei watakapokamatwa na kufunguliwa mashtaka.

''Wale waliomuua Kenei hawataona amani , tutawasaka na wale walio na njama dhidi yangu , pengine muniue lakini sitatishika'', alisema.

Naibu huyo wa rais pia alizungumzia kuhusu mazungumzo yao ya mwisho na Kenei akisema walizungumza siku tatu kabla ya afisa huyo kupatikana amefariki nyumbani kwake.

"Jumatatu hiyo wakati nilifika kwa ofisi, nikaita yule anayesimamia ulinzi katika ofisi ya majengo ya naibu wa rais Bw. Joseph Rop ambaye ni kamishna wa Police, na nikamuita yule ambaye anasimamia escort katika hiyo ofisi Bw. William Yampoi…wote wawili walikuja kwa ofisi yangu. Nilitaka kujua ni jambo gani lilitendeka Alhamisi iliyopita," alisema.

"Hawa wawili walikuja wakaniambia ilitokea hivi, mpaka wakaniletea CCTV. Mimi nikaita Kenei na wenzake wawili ambaye wanafanya kazi pamoja. Wakasimama mbele yangu pale ofisini," DP Ruto aliongezea.

Bwana Ruto pia aliongezea kwamba aliwahoji maafisa hao watatu kuelezea kile kilichotokea siku ambayo aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa alionekana katika ofisi yake na raia wawili wa kigeni;

"Kenei akaniambia ya kwamba ni kweli, yeye anajuana na Bw. Echesa…alikuwa amepigiwa simu na kuambiwa Echesa na wenzake waliokuja kwa ofisi yangu walikuwa na appointment…ndio akawaruhusu waje katika chumba cha kusubiri cha wageni," alisema Ruto.

Kulingana na naibu huyo wa rais , Kenei na wenzake walikubali kwenda kwa idara ya ujasusi ili kurekodi taarifa. Naibu huyo anasema kwamba hiyo ndio mara ya mwisho alizungumza na sajenti huyo.

Dkt. Ruto anasema kwamba alifanyia kazi zake nyumbani siku ya Jumanne na Jumatano.

Mwili wa Kenei ulipatikana nyumbani kwake

Mwili wa Sajini Kenei ulipatikana nyumbani kwake wiki mbili zilizopita ukiwa na jeraha la risasi. Kulingana na taarifa ya polisi, marehemu aliuawa

Kifo cha askari huyo kilitokea wakati ambapo alitakiwa kuandika taarifa ya maelezo kwa polisi kuhusu washukiwa wa sakata ya zabuni hewa ya ununuzi wa silaha za mamilioni ya pesa walipotembelea ofisi ya Dkt Ruto mjini Nairobi.