Coronavirus: Kwanini Uganda imewafurusha raia 22 wa kigeni waliowasili kwa kongamano la kibiashara

Baadhi ya raia wa kigeni waliowasili katika uwanja wa Entebbe nchini Uganda wakipiga foleni ya kukaguliwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Baadhi ya raia wa kigeni waliowasili katika uwanja wa Entebbe nchini Uganda wakipiga foleni ya kukaguliwa

Maafisa wa wizara ya afya nchini Uganda siku ya Jumapili wamesema kwamba takriban raia 22 wa kigeni watarudi katika mataifa yao huku hofu ya maambukizi ya virusi vya corona ikiendelea.

Uganda ndio mwenyeji wa kongamano la kimataifa kuhusu biashara linaloanza nchini humo hii leo.

Kulingana na waziri ya afya nchini humo raia hao walikataa kwenda karantini kwa siku 14 walipowasili katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

''Siku ya Jumapili tulipokea abiria 22 kutoka mataifa yanayoorodheshwa katika Shirika la Afya Duniani WHO kuwa katika orodha ya kwanza ya maambukizi ya corona katika uwanja wa ndege.

Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na dalili ama ishara za COVID19. Tuliwaambia kuhusu hatua zetu za kujiweka katika karantini kwa siku 14 . Hatahivyo hawakuwa tayari kufuata maagizo yetu .Hii leo watarudi nyumbani kwao'', waziri wa afya Dkt. Ruth Aceng alisema sikjuya Jumapili. ''

Kufikia sasa Uganda haijathibitisha ama kuwa na shuku ya kisa chochote cha ugonjwa wa COVID19.

Hatua hiyo ya Uganda inajiri saa chache tu baada ya mtalii kutoka Ujerumani kufariki kutokana na virusi vya corona katika eneo la kitalii la Sinai mashariki mwa Misri, ikiwa ndio kifo cha kwanza kurekodiwa Afrika.

Raia huyo wa Ujerumani aliyekuwa na mwenye umri wa miaka 60 alionesha dalili za joto mwilini na kulazwa katika hospitali ya Hurghada tarehe 6 mwezi Machi , kabla ya kupatikana na ugonjwa huo , ilisema ripoti ya wizara ya afya.

Mtalii huyo aliyewasili kutoka Ujerumani wiki moja iliopita , alifariki baada ya kukataa kuhamishwa hadi katika eneo lililotengwa baada ya kuugua ugonjwa mbaya wa mapafu.

Siku ya Jumamosi , wizara ya afya ilitangaza kuhusu visa 45 vya raia wa Misri na wale wa mataifa ya kigeni waliodaiwa kuambukizwa virusi hivyo katika meli moja mto Nile.

''Boti hilo lilikuwa likibeba watu 171 -ikiwemo wageni 101 na wafanyakazi 70 wa Misri'', alisema Waziri Mkuu Mostafa Madbouli.

Mbali na visa hivyo vya meli ya watalii, Misri imegundua visa vingine vitatu vya maambukizi ya virusi hivyo huku kisa cha kwanza kikiwa kilitangazwa tarehe 14 mwezi Februari.

Wizara ya afya ilisema wiki iliopita kwamba mgonjwa wa kwanza , raia wa China alipona na kuachiliwa.

Visa vingine viwili , raia wa Canada aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya mafuta na raia mmoja wa Misri aliyekuwa amerudi kutoka Serbia kupitia Ufaransa walikuwa wanaendelea na matibabu.

Mataifa mengine matatu ikiwemo Ufaransa yametangaza kwamba abiria sita waliokuwa wakirudi kutoka Misri waligunduliwa kuwa na virusi hivyo.

Jinsi ya kujizuia na maambukizi ya virusi vya corona

Wataalam wa afya ya Umma wamekuwa wakitoa ushauri ili kujaribu kuzuia maambukizi ya virusi hivi.

Je nitajilinda vipi?

Je dalili ni zipi?

Nifanyeje iwapo sijisikii vyema?