Jimbo la Kano Nigeria lampata Amir mpya baada ya kutimuliwa kwa mtangulizi wake kwa 'kukosa heshima'

The Emir of Kano, Muhammadu Sanusi II

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Muhammadu Sanusi wa II ni gavana wa zamani wa Benki kuu ya Nigeria

Serikali ya jimbo la Kano lililoko Kaskazini mwa Nigeria imemteua Amir mpya wa Kano. Kiti cha Amir ni kiti chenye ushawishi mkubwa zaidi cha kitamaduni nchini humo

Uteuzi huo umefuatia kufutwa kazi kwa Amir Muhammadu Sanusi wa II ambaye amekua katika mzozo wa muda mrefu na gavana wa jimbo hilo.

Amir mpya Aminu Ado Bayero -ambaye ni mwana wa mtangulizi wa Sanusi ambaye aliliongoza jimbo la Kano kwa zaidi ya nusu karne hadi kifo chake kilipotokea mwaka 2014.

Amir mpya alikua amegombea kiti ufalme huo na Amir Muhammadu Sanusi baada ya kifo cha baba yake .

Muhammadu Sanusi wa II, alitolewa uongozini baada ya kutenda " kinyume kabisa na maagizo ya sheria katika za ofisi ya gavana wa jimbo," imesema serikali ya jimbo la Kano.

Maelezo ya picha,

Amir mpya wa Kano, Aminu Ado Bayero ni mtoto wa mtangulizi wa Sanusi

Bwana Sanusi, ambaye ni gavana wa zamani wa Benki kuu ya Nigeria amekua na uhusiano mbaya na gavana wa jimbo la Kano Abdullahi Ganduje, tangu mwaka 2017.

Je ni kwanini amefutwa kazi?

Serikali imesema kuwa alifutwa kazi "ili kulinda utakatifu, utamaduni, mila, dini na ufahari wa ufalme wa Kano," akimshutumu Amir kwa " kukosa kabisa heshima" kwa taasisi na ofisi ya gavana.

Tangu Amir na gavana walipokosana, Bwana Sanusi hajahudhuria sherehe na mikutano rasmi, ambayo serikali inasema ilikua ni "ukosefu wa utiifu".

Mwandishi wa BBC aliyeko Kano Mansur Abubakar anasema kukataa kwa Amir kufika mbele ya jopo la uchunguzi wa madai ya ufisadi dhidi yake ni jambo ambalo halikuifurahisha serikali.

Anashutumiwa kuuza ardhi na matumizi mabaya ya pesa la ufalme lakini alipata agizo la mahakama la kusitisha uchunguzi dhidi yake.

Kulingana na Mhariri mkuu wa gazeti la Nigeria Daily Trust Mannir Dan Ali, hizi ndizo sababu jimbo liliamua kuchukua hatua dhidi ya kiongozi mwanye ushawishi wa kidini na kitamaduni katika jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu la Kaskazini. Katika barua za BBC kutoka kwa waandishi wa habari mwandishi Mannir Dan Ali anasema:

Bwana Sanusi alitumia nafasi yake kama Amir kuzungumzia masuala ambayo si ya kawaida kwa eneo la kaskazini mwa Nigeri na uzungumzaji wake wa wazi uliwaudhi baadhi ya wanasiasa.

Maelezo ya picha,

Gavana Abdullahi Ganduje aliugawanya ufalme muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwake tena

Kwa zaidi ya miaka 1,000 , cheo cha Amir wa Kano kimekuwa cha heshima na cha kutamaniwa. Viongozi wa kitamaduni hua na mamlaka machache ya kikatiba, lakini huwa wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwasababu wanaonekana kama watu wanaolinda dini na utamaduni.

Kazi za Amir:

  • Alikua na mamlaka kamili kabla ya ukoloni wa Muingereza
  • Alikua sehemu ya utawala wa kikoloni
  • Ana mamlaka machache tangu uhuru
  • Anaoanekana kama mtu anayehifadhi dini na utamaduni
  • Mtu anayeheshimika hususan miongoni mwa Waislamu wa Kaskazini

Lamido Sanusi, Mkuu wa zamani wa Benki kuu mwenye utata, aliingia kwenye mamlaka ya enzi ya Amir mwaka 2014 baada ya kuchaguliwa na wazee na baadae kuidhinishwa na aliyekua gavana wa wakati huo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wafuasi wake wanaamini kuwa Bwana Sanusi(katikati) alifutwa kazi kwa kupinga kuchaguliwa tena kwa gavana mwaka jana

Kama ilivyokua wakati wa uongozi wake katika Benki, ambako alifutwa kazi baada ya kufichua kwamba mabilioni ya dola ya mapato ya mafuta yalipotea, Bwana Sanusi mwenye umri wa miaka 57-alitumia cheo chake kuzungumzia wazi juu ya baadhi ya mambo.Lakini mwenendo wake wa utakatifu zaidi ya wengine uliwakera baadhi ya wanasiasa.

Dalili ya kwanza kwamba mahusiano baina ya serikali ya jimbo na ufalme yalikua si mazuri wakati wote ilijitokeza muda mfupi baada ya kuchaguliwa tena kwa Gavana Ganduje mapema mwaka huu.

Video ilianza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha umati katika jengo la serikali ya Kano ukiondoa kwa nguvu picha za Amir na kuzichana vipande vipande.

Bwana Sanusi ni nani?

Akizaliwa katika familia ya kifalme ya Fulani , Lamido Sanusi alikua Amir wa 14 wa Kano mwaka 2014 baada ya kifo cha mtawala wa zamani Ado Bayero.

Alielezea nafasi hiyo yenye uzito miongoni mwa Waislamu wa Kaskazini mwa Nigeria, kama kazi aliyoitamani kwa muda mrefu maishani mwake.

Kama Amir, alichukua ufalme uliokuwepo miaka mamia kadhaa na alionekana kama kiongozi wa kisiasa wa mamilioni ya Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria.

Katika miaka ya 1990 aliacha kazi iliyokua na malipo maziuri ya benki ili kupatauelewa zaidi wa Kiarabu na masomo ya Uislamu kwa kwenda kwenda kusoma nchini Sudan.

Ni mwanaume ambaye hakuona aibu kuzungumzia masuala yenye utata.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kama Amir, Bwana Sanusi amekua akikosolewa kwa kusikilizwa badala ya kuangaliwa

Zamani kabla hajawa Amir, alipinga kuidhinishwa kwa Sheria ya kiislamu katika baadhi ya majimbo ya kaskazini, akidai kwamba kulikua na masuala muhimu yanayohitaji kushugulikiwa kuliko kupata umaarufu.

Lakini alipata umaaruifu alipokua gavana wa Benki Kuu ya Nigeria.

Ufichuzi wake wa dola bilioni 20 zilizodaiwa kupotea kutoka katika kampuni ya mafuta ulisababisha kufutwa kwake kazi na rais wa wakati huo Goodluck Jonathan.

Serikali ilikana kuwa kulikua na pesa zozote zilizopotea.

Bwana Sanusi alikosoa kufutwa kwake kazi mahakamani lakini uamuzi huo haukubadilishwa. Badae aliondoa kesi yake mahakamani.

Wafuasi wake wanaamini kuwa alifutwa kazi kwa kupinga kuchaguliwa tena kwa gavana mwaka jana. Wanasema kitendo cha gavana kuugawa ufalme wa Kano katika makundi matano na kuwateua maamir wengine nne zaidi, ni ushahidi kwamba alikua anataka kumaliza ushawishi wa Bwana Sanusi.

Wanasema pia kwamba amevunja utamaduni wa Amir kuonekana , badala ya kusikilizwa.