Coronavirus: Italia yachukua hatua za dharura nchi nzima kudhibiti virusi hatari

Raia wa Italia watakiwa kujiweka karantini kuzuia maambukizi

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Raia wa Italia watakiwa kujiweka karantini kuzuia maambukizi

Italia imeongeza hatua za dharura za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona, ikiwemo kuzuia safari na kupiga marufuku mikusanyiko ya Umma nchi nzima.

Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu Giuseppe Conte aliamuru watu wabaki majumbani na sharti waombe ruhusa na kupata kibali kwa ajili ya safari zenye umuhimu pekee.

Amesema hatua hizo ziliwekwa kwa ajili ya kuwalinda wale walio hatarini kupata maambukizi . ''Hakuna muda zaidi,'' alisema alipohutubia raia kwa njia ya Televisheni.

Vifo vilivyotokana na virusi vya corona sasa vimefikia 463 kutoka 366 siku ya Jumatatu. Athari mbaya zaidi baada ya China.

Idadi ya maambukizi imethibitishwa kufikia 24% kutoka siku ya Jumapili, maafisa walieleza.

Visa vya maambukizi vimethibitishwa kuwepo kwenye miji yote 20 nchini Italia.

Bwana Conte amesema nini?

Conte amesema hatua bora zaidi ni kuwa watu wasalie majumbani. ''Kuna ongezeko kubwa la maambukizi ...na vifo,'' amesema kwenye taarifa yake.

''Italia nzima itakuwa kwenye uangalizi,'' aliongeza.

''Sote tunapaswa kujitoa kwa ajili ya Italia. Tunapaswa kufanya hivyo sasa.

''Hii ndio sababu nimeamua kuchukua hatua ngumu zaidi ili kulinda afya za raia wote.''

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanamke akiwa amevaa Barakoa

Marufuku imegusa maeneo yapi?

Waziri Mkuu Conte ameeleza hatua hiyo inajulikana kwa jina ''Ninabaki nyumbani''- watu wakipigwa marufuku kukusanyika. ''Hakuna mikusanyiko ya starehe za usiku; hatuwezi kuruhusu hili tena,'' alisema

Matukio ya michezo ikiwemo mechi za kandanda zimezuiwa nchi nzima. Shule zimefungwa na vyuo vitabaki vimefungwa mpaka tarehe 3 mwezi Aprili.

Serikali imesema wale wenye sababu za kikazi na kifamilia ambazo haziwezi kuahirishwa wataruhusiwa kusafiri.

Abiria wanaotaka kuondoka wanatakiwa kuwa na sababu za msingi, kama watakavyofanya wanaoingia na ndege nchini humo.

Kwenye vituo vya treni kuna udhibiti pia, abiria hupimwa kiwango cha joto cha mwili. Meli pia zimezuiwa kutia nanga katika bandari kadhaa nchini humo.

Watu wamesema nini?

Mapema Jumatatu, wafungwa saba walipoteza maisha kutokana na vurumai kwenye magereza nchi nzima baada ya mamlaka kupiga marufuku kuwatembelea wafungwa kuepuka kusambaa kwa ugonjwa.

Ghasia zilianza katika mji wa Kaskazini wa Modena katika gereza la Sant'Anna.

Inadhaniwa kuwa watu wapatao wawili walipoteza maisha kutokana na kuzidisha kipimo cha dawa baada ya kuvamia hospitali ya gereza kwa ajili ya dawa ya methadone.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Ndugu wa wafungwa katika gereza la Rebibbia mjini Roma wakiandamana baada ya kuzuiwa kuingia

Katika gereza la San Vittore mjini Milan, wafungwa walichoma moto sehemu ya gereza , kisha walipanda mpaka darini kupitia dirishani wakipunga bendera, maafisa wameeleza.

Kwenye gereza kusini mwa mji wa Foggia, wafungwa kadhaa walitoroka nje ya jengo wakati wa maandamano, Wengi walikamatwa, shirika la habari ya Italia la Ansa liliripoti. Wafungwa tisa bado hawajulikani walipo.

Pia kulitokea vurugu katika magereza mengine Kaskazini mwa Italia mjini Naples na Roma.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Maafisa wa ulinzi wakiwa katika gereza la Sant'Anna wakati wa maandamano

Hali ya sasa duniani

Idadi ya maambukizi dunia nzima sasa ni zaidi ya 111,000, na vifo takribani 3,890.

Kila atakayewasili Israel atawekwa karantini au kutakiwa kujiweka karantini kwa siku 14, amesema Waziri Mkuu Benjamin Natanyahu.

Iran imeripoti vifo 43 vipya kutokana na virusi vya corona katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Takribani watu 237 wamepoteza maisha na 7,161 wameambukizwa nchini humo tangu katikati ya mwezi wa Februari, ingawa takwimu zinadhaniwa kuwa huenda zikawa juu zaidi.