Coronavirus: Marekani yaonya kupigwa raia wa kigeni nchini Ethiopia

Ethiopia imeweka mazuio katika viwanja vyake vya ndege kuzuia maambukizi ya virusi vya corona

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ethiopia imeweka mazuio katika viwanja vyake vya ndege kuzuia maambukizi ya virusi vya corona

Balozi wa Marekani nchini Ethiopia ameonya kuwa wageni wanashambuliwa katika miji kote nchini baada ya kutuhumiwa kuambukizwa Covid-19, ugonjwa wa kupumua unaosababishwa na virusi vya corona.

Katika tahadhari ya usalama iliyowekwa kwenye tovuti yake, balozi huyo alisema "unaendelea kupokea ripoti kuhusu kuongezeka kwa maoni yanayowapinga-wageni" tangu kisa cha kwanza cha virusi kilipothibitishwa nchi hiyo ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika wiki iliyopita.

Kauli za dharau kama "Uchina" na "ferengi" ( wageni) "yameripotiwa kuhusishwa na virusi vya 'corona', ikiashiria mlipuko wa Covid-19 kuhusishwa na wageni nchini Ethiopia", iliongezea.

"Ripoti zinaonyesha kuwa wageni wameshambuliwa kwa mawe, wamekataliwa huduma za usafirishaji ... wakitemewa mate, kukimbizwa kwa miguu, na kushukiwa kuambukizwa na Covid-19," ubalozi uliongeza.

Ethiopia imegundua kuambukizwa kwa watu sita na virusi vya corona wakwanza alikuwa raia wa Japan ambaye alisafiri kutoka nchi ya Afrika Magharibi, Burkina Faso.

Serikali ya Ethiopia imesemaje?

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Abiy Ahmed alipewa tuzo ya amani ya Nobel mwezi Oktoba

Waziri Mkuu wa Ethiopia na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel amewaambia raia wa nchi yake kuwa virusi vya corona havina uhusiano wowote na uraia

Taarifa ya Abiy Ahmed imesema:

''Ni muhimu kufahamu kuwa virusi havina uhusiano na nchi au uraia wa mtu.''

''Kila mmoja yuko katika hatari ya kupata maambukizi hivyo kufuata taratibu zilizowekwa na Wizara ya afya ni muhimu sana''.

''Jitihada za kuzuia zifanye watu kutozingatia utu na huruma kwa wengine''

''Katika jumuia ya ulimwengu kila mmoja ni mwangalizi wa mwenzie. Hivyo hofu isitupore utu wetu.''

Ethiopia mpaka sasa imethibitisha kuwa na wagonjwa sita wa virusi vya corona, akiwemo raia wa Japan na mwanadiplomasia wa Uingereza.