Coronavirus: India imeweka zuio la watu kutotoka katika nyumba zao kabisa

Polisi nchini India wakifanya doria ya kuzuia watu kutoka nje Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imeongezeka kwa kasi hivi karibuni

Kuna maswali mengi yanaulizwa nchi ikifungwa kabisa, hali inakuwaje?

India ni kati ya mataifa ambayo yana watu wengi zaidi duniani lakini sasa nayo imejumuka na nchi nyingine kama Mauritius, Uingereza na Afrika Kusini kutangaza marufuku ya watu kutoka nje, ama 'lockdown'.

Kwingineko ni Senegal na Ivory Coast wamechukua hatua ya kutangaza dharura ya kitaifa na kuweka marufku ya watu kutembea usiku.

Nayo Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo, imezuia watu kutoka katika mji mmoja kwenda nyingine.

Lakini wasiwasi unakuja kutoka katika mataifa yote, unaonekana kulingana, wengi wakihofia chakula na mahitaji muhimu yatapatikana vipi?

Haki miliki ya picha Getty Images

Waziri mkuu wa India, Narendra Modi ametangaza zuio la watu kutotoka nje katika nchi nzima ikiwa ni hatua ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Katazo hilo ambalo linaanza kutekelezwa kuanzia usiku wa leo kwa muda wa India na litadumu kwa muda wa siku 21.

"Hakuna mtu atakayeruhusiwa kutoka nje ya nyumba yake kabisa" bwana Modi alisema hayo akihutubia nchi kupitia televisheni.

Waziri Modi amewataka watu kuondoa shaka, lakini kwa haraka watu walijaa katika maduka ya miji mikubwa kama Delhi na miji mingine.

Mwandishi wa BBC nchini India anasema kuwa haijawekwa wazi ni namna gani watu wanaweza kuruhusiwa kutoka nje kwenda kununua chakula na mahitaji mengine muhimu.

Hatua hizo mpya zimekuja baada ya siku za karibuni idadi ya maambukizi kuongezeka kwa kasi.

Kulikuwa na wagonjwa 519 waliothibitiwa kuwa na ugonjwa nchini humo na vifo 10 viliripotiwa kutokea kwa sababu ya ugonjwa huo wa covid-19.

India - ni nchi ambayo ina idadi ya watu bilioni 1.3 -na sasa imeungana na mataifa mengine kuchukua hatua ya kufunga taifa kabisa.

Kwa sasa karibu watu 400,000 duniani kote wana maambukizi ya virusi vya corona huku watu wapatao 17,000 wamefariki.

"Nchi nzima itafungwa kabisa ," bwana Modi alisema siku ya Jumanne.

Aliongeza pia: "Hatua hii imechukuliwa ili kuokoa taifa la India, raia wake wote na familia zote kwa ujumla... kila mtaa, kila jirani anapaswa kujifungia."

Bwana Modi alitoa angalizo kuwa kama India itashindwa kufuata utaratibu huu kwa siku 21... basi tutakuwa tumerudi nyuma hatua kwa miaka 21".

"Itatubidi kulipia uchumi, Hili ni jukumu la kila mmoja wetu."

Baadae bwana Modi alitoa angalizo la suala la mkusanyiko wa watu wengi madukani kutaweza kusababisha ugonjwa huo kusambaa zaidi.

Alisema kuwa serikali itahakikisha chakula kinaletwa majumbani.

Lakini mjini Delhi na mji wa kibiashara wa Mumbai, watu wanahofia kukosa chakula madukani na dawa kwenye maduka.

"Sijawahi kukutana na hali tete kama hii katika maisha yangu," mhudumu wa duka alieleza huko Delhi.

"Tumeuza bidhaa zote kama biskuti, mchele, mikate, unga, mafuta ya kupikia."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu wakiwa wamepanga foleni dukani mjini Mumbai baada ya waziri mkuu kutangaza kufunga nchi

Hatua mpya zinataka biashara zote kufungwa lakini hospitali na huduma za afya kuendelea kama kawaida. Shule na vyuo vikuu vitaendelea kufungwa pamoja na mikusanyiko yote ya watu imezuiwa.

Na yeyote atakayekiuka maagizo ataadhibiwa kifungo cha miaka miwili na faini kubwa.

Katazo hilo limekuja baada ya India kuweka katazo la usafiri la kimataifa na ndani ya nchi.

Treni ukiwa ndio usafiri mkubwa nchini humo pia umesitisha huduma.

Haki miliki ya picha Getty Images

Hatua hii ya India kufunga taifa lake 'lockdown' ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, na huku watu wakiwa wanatakiwa wabaki ndani wakati kipato chao wengi ni cha chini ni swali ambalo linawapa hofu wengi.

Ni kitu ambacho hakiaminiki kutokea wakati wengine wakiofia kufa na njaa badala ya virusi vya corona.

Mfano ,Ramesh Kumar, kutoka jimbo la Uttar Pradesh "Nina kipato kidogo sana, nilikuwa nalipwa dola nane kila siku ninapofanya kazi na fedha hiyo napaswa kuwalisha watu watano.

Kwa hali hii lazima tutaishiwa chakula, najua corona ni hatari lakini siwezi kuona watoto wangu wakifa na njaa," alisema.

Mamilioni ya watu wanapata kipato cha siku, na katika hali hii ya kufungiwa basi ina maana kuwa hawatakuwa wanalipwa kwa muda wa wiki tatu zote.

India kufungwa haitaleta athari kwa uchumi peke yake bali hata kwenye masuala ya kijamii, Taifa hili maisha ya jumuiya ndio kila kitu.

Kwenda kuabudu ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, hatua hii inabadili tamaduni zao moja kwa moja.

Mada zinazohusiana