Virusi vya Corona: Sudan Kusini yathibitisha kuwa na mgonjwa wa COVID-19

Dk. Riek Machar Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Dk. Riek Machar ametangaza kisa hicho

Sudan Kusini yathibitisha kuwa na mgonjwa wa kwanza wa Corona .

Makamu wa rais wa Sudan Kusini, Dk. Riek Machar amezungumza na waandishi wa habari mjini Juba siku ya Jumapili, April 05 .

Mgonjwa aliyethibitishwa nchini Sudan Kusini ni msichana wa miaka 29 ambaye ni raia wa kigeni, alikuwa amerejea kutoka bara la Ulaya.

Taarifa kutoka Umoja wa mataifa, zinasema kuwa mtu huyo mwenye maambukizi ni mfanyakazi wa Umoja wa mataifa(UN).

Wizara ya afya nchini humo wakishirikiana na Shirika la afya duniani(WHO) wanaendelea kufanya uchunguzi na kupima watu kama wamepata maambukizi.

Mgonjwa huyo amekuwa nchini Sudan kwa kipindi cha wiki tano na amekuwa akifanyia kazi nyumbani tangu alipoanza kuona dalili.

Hali yake ya afya inaendelea vizuri mpaka sasa.

Watu wote waliohusiana na mgonjwa huyo wamewekwa karantini.

Aidha serikali na umoja wa mataifa wanaendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha watu kujikinga na maradhi hayo kwa kuosha mikono mara kwa mara na kuepuka misongamano ya watu.

Sudan Kusini ni taifa la mwisho barani Afrika kutangaza kuwa na maambukizi ya corona nchini mwake.

Mada zinazohusiana