Virusi vya corona: Waziri asimamishwa kazi kwa kushiriki chakula na rafiki yake A.Kusini

Stella Ndabeni-Abrahams amezua gumzo tangu picha yake akila chakula na rafiki yake

Chanzo cha picha, Stella Ndabeni-Abrahams/Twitter

Maelezo ya picha,

Stella Ndabeni-Abrahams amezua gumzo tangu picha yake akila chakula na rafiki yake

Waziri wa habari nchini Afrika Kusini amesimamishwa kazi kwa miezi miwili mwezi mmoja bila mshahara kwa kupata chakula cha mchana na rafiki yake wakati huu ambao kuna amri ya kutotoka nje.

Stella Ndabeni-Abrahams amezua gumzo tangu picha yake akila chakula na rafiki yake Mduduzi Manana kusambaa mitandaoni wiki hii.

Picha hiyo ikiwaonesha wakifurahia chakula mezani na wanafamilia wa Manana, ilichapishwa kwenye moja kati ya akaunti za mitandao ya kijamii na imekuwa ikirudiwa kuchapishwa na wengine mara nyingi.

Raia wa Afrika Kusini wametakiwa kubaki majumbani mwao wakati huu wa amri ya kutotoka nje- sasa ikiwa ni wiki ya pili, wakiruhusiwa kutoka iwapo wana safari muhimu, kama za kazini, kununua chakula au kutafuta huduma za matibabu.

Rais Cyril Ramaphosa, ambaye alizungumza na waziri huyo kuhusu picha , alisema katika taarifa yake siku ya Jumatano kuwa ''hajashawishika'' na sababu alizozitoa za yeye kwenda kwenye familia ya Manana''.

''Hakuna miongoni mwetu atakayepuuza juhudi zetu za kuokoa maisha wakati huu,'' alisema. Rais aliongeza kuwa ''hakuna aliye juu ya sheria''.

Waziri Ndabeni-Abrahams ameomba radhi akisema ''anasikitishwa'' na vitendo vyake.

''Ninatumai rais na raia wa Afrika Kusini watanisamehe,'' aliongeza.

Taarifa zaid za virusi vya corona:

Chanzo cha picha, Empics

Maelezo ya picha,

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema ''hajashawishika'' na sababu alizozitoa waziri Stella Ndabeni-Abrahams za yeye kwenda kwenye familia ya Manana''.

Awali Bwana Manana, naibu waziri wa zamani, alisema kuwa alimtembelea kwa sababu za kikazi.

Alisema alikwenda nyumbani kwake ili kuchukua barakoa ambazo alikuwa anataka kuzitoa kupitia taasisi yake kusaidia mapambano dhidi ya Covid-19.

Serikali ya nchi hiyo kwa kiasi kikubwa imesifiwa kwa juhudi zake za kudhibiti kuenea kwa virusi, sifa zilizotolewa pia na vyama vya upinzani.

Unaweza pia kutazama:

Maelezo ya video,

Ni lini Chanjo ya corona itapatikana?

Bwana Ramaphosa alitakiwa kuchukua hatua haraka lakini haijajulikana kama hatua zilizochukuliwa dhidi ya waziri huyo zitawaridhisha wale waliokuwa wakitoa wito kwa rais amfute kazi Bi Ndabeni-Abrahams kutokana na kitendo hicho.