Coronavirus: Chumba cha wagonjwa mahututi ni nini na ni wagonjwa gani wanastahili kukitumia?

Hospital bed

Chanzo cha picha, Science Photo Library

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ni miongoni mwa watu ambao wamekitumia chumba cha wangonjwa mahututi huko St Thomas' hospital mjini London.

Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na ushauri wa madaktari wake.

Lakini je chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ni chumba cha aina gani haswa?

ICU ni wodi maalum ambayo imetengwa kutoa huduma kwa wagonjwa ambao wako katika hali mbaya na wanahitaji uangalizi wa karibu.

Vyumba hivi vina idadi ndogo ya wagonjwa na wahudumu wengi ili waweze kutoa huduma ya moja kwa moja itakapohitajika.

Na pia mashine zinazotumika ni za hali ya juu.

Kuna vitanda 500 vya wagonjwa mahututi katika hospitali mpya ya Nightingale Uingereza.

Nani anahitaji huduma za chumba cha wagonjwa mahututi?

Kuna sababu nyingi kwanini mtu anaweza kuhitaji aina hii ya huduma.

Baadhi ya wagonjwa huwekwa kwenye chumba hichi hadi watakaporejesha fahamu zao baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa.

Wengine wanakihitaji kwasababu ya majeraha mabaya baada ya kupata ajali.

Waziri Mkuu wa Uingereza, aliwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwasababu dalili za maambukizi ya virusi vya corona zilikuwa hazioneshi kuimarika.

Coronavirus inaweza kuathiri mapafu na inaonekana pengine Waziri Mkuu alikuwa na matatizo ya kupumua.

Ni huduma gani inayotolewa ICU?

Sio kila mgonjwa mwenye maambukizi ya corona atahitaji mashine ya kupumilia na hivyo basi kuhitajika kupelekwa ICU.

Wengine wanaweza kuwekwa kwa mashine nyengine ambayo inatumia shinikizo la chini kusukuma oksijeni katika njia ya kupumulia kupitia aina fulani ya barakoa.

Wagonjwa wanaotumia aina hii ya mashine wanaweza wakawa wanapumua kawaida tofauti na mashine ya kupumulia yaani ventilator ambapo mtu hudungwa sindano ya kupoteza fahamu.

Wagonjwa katika chumba cha ICU watakuwa wameunganishiwa mashine nyingi tu tofauti tofauti, kupitia mirija, nyaya na kebo ili kufuatilia vile mwili unavyokabiliana na hali hiyo.

Na pia wanaweza kupewa dawa kwa njia ya mishipa au njia zingine za matibabu ikiwemo ya lishe.

Hospitali ya St Thomas inatajriba ya kutibu wagonjwa wa corona katika vyumba vyao vya wagonjwa mahututi.

Kwa walio katika hali mbaya zaidi wanaweza kutumia mashine ya kusaidia mtu kuishi yaani life support machine ambayo hutekeleza baadhi ya majukumu yanayoendeshwa na moyo na mapafu.

Hata hivyo mashine hizo ni kidogo sana nchini Uingereza.

Kupata afueni ukiwa chumba cha wagonjwa mahututi

Punde tu mtu atakapopata afueni ya kutosha, ataondolewa katika chumba hicho na kuhamishwa hadi chumba kingine. Hii inatoa fursa kwa mgonjwa mwengine anayehitaji huduma kama hiyo kwa haraka kuipata kwa wakati unaofaa.

Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuondoka hospitali siku chache baada ya kutoka chumba cha wagonjwa mahututi hata hivyo kuna wale ambao wanaweza kuhitajika kuwa hapo kwa wiki au miezi kadhaa.

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video,

Boris Johnson ahamishwa hadi chumba cha wagonjwa mahututi