Virusi vya Corona: Je, kodi ya nyumba inastahili kuondoshwa katika kipindi hiki cha janga la Covid-19?

makaazi
Maelezo ya picha,

Makaazi

Nchini Uganda, rais Yoweri Museveni amesema kuwa haikubaliki kwa wenye nyumba kuwafurusha wapangaji wao wanashindwa kulipa kodi katika kipindi hiki.

Mlipuko wa virusi vya corona umepindua kabisa mfumo wa maisha ya watu ya kila siku. Wataalamu wanasema hili ndilo janga kubwa zaidi kulikumba dunia toka kuisha kwa Vita ya Pili ya Dunia miaka 75 iliyopita.

Marufuku za kutoka nje, na hatua nyengine za kudhibiti kusambaa kwa virusi zimewekwa sehemy mbalimbali duniani. Moja ya athari yake kubwa ni kuanguka kwa vipato vya watu.

Shirika la Kazi Duniani (ILO) linakadiria kuwa takribani wafanyakazi bilioni 3.3 wameathirika na janga la virusi vya corona baada ya sehemu zao za kazi kufungwa kabisa ama kwa kiasi.

'Watu watapata wapi pesa za kodi?'

"Wenye nyumba ambao wanajaribu kuwafurusha wapangaji wao kwa sababu ya kodi, hilo halikubaliki. Tupo katika janga hili la Covid-19 kwa pamoja. Dunia haiishi leo; unaweza kudai pesa yako baadae kipindi hili liwa limeisha," ameandika Yoweri Museveni katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

Nchini Kenya, rais Uhuru Kenyatta amewapongeza wenye nyumba ambao wamesamehe ama kupunguza kodi ya pango kwa wapangaji wao.

Wapo watu kadhaa wanaomiliki nyumba za makazi na biashara ambao wametangaza msamaha kwa kipindi hiki, na kutaka wengine waige mfano wao mwema.

"Nawashukuru baadhi ya wenye nyumba ambao wamepunguza kodi ya pango ya kila mwezi ili kusaidia wapangaji wao, hususani wale waliothirika zaidi kiuchumi kupata sehemu ya kulala. Kutokana na hilo, nawaomba wengine waige mfano huu wa kujitoa kifedha. Huu ni wakati huruma na kuwaelewa wengine," rais Kenyatta alieleza siku ya Jumatatu.

Nchini Tanzania, hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam pia aliwaomba wenye nyumba kupunguza kodi.

"Nimeongea na wenye nyumba na kuwataka wapunguze kodi kwa asilimia 50 ili kusaidia kufanya biashara na kuangalia hali ya uchumi ilivyo kwa sasa kama mnavyofahamu corona imeathiri hali ya kifedha," alisema Makonda wiki iliyopita.

Hoja za viongozi hao, pamoja na wapangaji katika nchi zote hizo ni kuwa kutokana na janga lilopo kwa sasa ni vigumu watu kupata pesa za kujikimu kimaisha ikiwemo kulipa kodi.

'Hamuwezi kukaa tu bila kulipa'

Hata hivyo kuna upande wa pili wa shilingi, wenye nyumba, baadhi yao wanategemea kodi kuendesha maisha yao.

Na hata viongozi wanaotaka watu kupunguziwa kodi wanalizungumza hilo kwa njia ya ushauri zaidi.

Nchini Uingereza, chama cha wenye nyumba kimewaambia wapangaji kuwa wasitarajie kuwa janga la corona itakuwa ruhusa ya kuacha kulipa kodi.

Uongozi wa chama hicho unasema kuwa endapo kila mtu atasamehewa ama kupata punguzo la kodi katika kipindi hiki basi soko la nyumba nchini humo litaporomoka.

Hata hivyo chama hicho kimewataka wanachama wao kuwa waelewa kwa wapangaji wao ambao wameathika vibaya kiuchumi. Na kutaka maelewano yoyote ya punguzo ama kusimamisha kutoza kodi yafanyike baina ya mpangaji na mwenye nyumba.

"Lakini hii si ruhusa ya kutolipa kodi popote pale ulipo, hauwezi ukakaa bure tu," ameeleza mkuu wa chama cha wenye nyumba Bw Ben Beadle.

Mapatano hayo ya wenye nyumba na wapangaji wao yanatarajiwa kufanyika katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi huu wa Aprili.

Serikali ya Uingereza pia imetangaza marufuku ya miezi mitatu ya wapangaji kutimuliwa na wenye nyumba.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kuwalinda wale watakaoshindwa kulipa kodi katika kipindi hiki.

Wenye nyumba wanataka kuwe na makubaliano ya namna gani watalipwa pesa zao katika miezi itakayofuatia.

Hata hivyo, umoja wa wapangaji wa jijini London unataka hatua zaidi zichukuliwe na kufuta madeni hayo ili wapangaji "wasibebe mzigo mwengine wa kulipa madeni ya nyuma ambayo yatawaumiza kiuchumi."

Chama cha wanafunzi nchini humo pia kimewataka wenye nyumba kutowalipisha kodi wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamelazimika kurudi makwao mpaka pale watakapotangaziwa vyuo kufunguliwa.