Virusi vya corona: Makubaliano ya kupunguza uzalishaji mafuta yafikiwa: Je hili litamaliza mvutano wa bei?

Opec bado haijatangaza rasmi makubaliano hayo lakini nchi husika zimethibitisha kuwa ziko tayari kwa mabadiliko.

Chanzo cha picha, TASS / Getty Images

Maelezo ya picha,

Opec bado haijatangaza rasmi makubaliano hayo lakini nchi husika zimethibitisha kuwa ziko tayari kwa mabadiliko.

Wazalishaji na washirika wa nchi zinazouza mafuta wamekubaliana kufikia makubaliano na kupunguza uzalishaji kote duniani kwa takriban asilimia 10 baada ya hitaji kupungua pakubwa kwasababu ya amri ya kusalia majumbani kama njia moja ya kukabiliana na virusi vya corona.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa Jumapili kupitia mkutano uliofanyika kwa njia ya video, ni ya kwanza kupunguza uzalishaji mkubwa wa mafuta ambayo hayajawahi kufikiwa siku za nyuma.

Shirika la nchi zinazozalisha mafuta (OPEC) na washirika wake ikiwemo Urusi, lilitangaza mipango ya kufikia makubaliano hayo Aprili 9 ingawa Mexico haikuridhia ombi hilo.

Opec bado haijatangaza rasmi makubaliano hayo lakini nchi husika zimethibitisha kuwa ziko tayari kwa mabadiliko.

Kile kilichothibititshwa hadi kufikia sasa, ni kwamba wazalishaji hao na washirika wake watapunguza uzalishaji wa mapipa milioni 9.7 kwa siku.

Jumatatu, Barani Asia bei ya mafuta ilipanda kwa zaidi ya dola 1 kwa pipa na kiwango cha mafuta ghafi cha asilimia 3.9 yakiuzwa kwa dola 32.71 kwa pipa huku Marekani asilimia 6.1 ikiuzwa kwa dola 24.15 kwa pipa.

Hisa nchini Australia zilipanda kutoka asilimia 3.46 zikiongozwa na wauzaji wa mafuta lakini nchini Japani hisa za Nikkei 225 zilishuka kwa asilimia 1.35 kwasababu ya wasiwasi wa hitaji lililoshuka duniani kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona.

"Makubaliano haya hayajawahi kufikiwa kabla kwasababu sio tu kati ya wazalishaji wa Opec na washirika wake… lakini pia na wauzaji wakubwa duniani ambao ni Marekani pamoja na nchi zingine za G-20 ambazo zimekubali kuunga mkono makubaliano hayo kwa kupunguza uzalishaji," Sandy Fielden, mkurugenzi wa utafiti wa mafuta katika kampuni ya Morningstar, ameiambia BBC.

Rais wa Marekani Donald Trump na waziri wa nishati wa Kuwait Daktari Khaled Ali Mohammed al-Fadhel waliandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, huku waziri wa kawi wa Saudi Arabia na Shirika la habari la Urusi linalomilikiwa na serikali (TASS) wakithibitisha makubaliano hayo Jumapili.

"Kwa uwezo wa Mungu na ungozi wa busara, juhudi na mazungumzo endelevu tangu alfajiri Ijumaa, sasa tunatangaza kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria ya kupunguza uzalishaji kwa takriban mapipa milioni 10 ya mafuta kutoka kwa nchi za wazalishaji wa mafuta OPEC kuanzia Mei Mosi, 2020," ameandika Dr al-Fadhel kwenye mtandao wa Twitter.

Hitaji la mafuta kote duniani linakadiriwa kupungua kwa theluthi moja wakati ambapo zaidi ya watu bilioni tatu wanafuata amri ya kusalia ndani kwasababu ya mlipuko wa virusi vya corona.

kabla ya hapo, mwezi Machi bei ya mafuta ilishuka vibaya baada ya nchi wazalishaji kushindwa kufikia makubaliano ya kupunguza uzalishaji.

Mazungumzo ya awali yalipata pigo baada ya Urusi na Saudi Arabia kushindwa kuafikiana, lakini Aprili 2, bei za mafuta ziliongezeka baada ya Rais Trump kuashiria kwamba anatarajia nchi hizo mbili kumaliza mgogoro wao.

Maelezo ya awali ya makubaliano hayo yaliyowekwa na Opec Ahamisi, yatafanya kundi la nchi wazalishaji na washirika wao kupunguza uzalishaji kwa mapipa milioni 10 kwa siku au asilimia 10 ya usambazaji kote duniani kuanzia Mei mosi.

Uzalishaji wa mapipa mengine milioni 5 unatarajiwa kupungua kutoka kwa mataifa mengine yasio wanachama kama vile Marekani, Canada, Brazil na Norway.

Inasemekana kwamba hatua hiyo itafanya uzalishaji kufikia kiwango cha mapipa milioni nane kwa siku kati ya Julai na Desemba. Kisha uzalishaji utapunguza tena hadi mapipa milioni 6 kati ya Januari 2021 na Aprili 2022.

'Uchambuzi wa makubaliano ya mafuta'

Mchambuzi wa masuala ya mafuta Gaurav Sharma ameiambia BBC kwamba makubaliano yaliyofikiwa Jumapili yalikuwa ya chini ikillinganishwa na mapipa milioni 10 yaliyofikiwa mwanzo siku ya Alhamisi. Mexico ilisita kufikia makubaliano hayo na kuchelewesha kutiwa saini.

Kisha Ijumaa, Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador alisema kwamba Bwana Trump alipendekeza kupunguza uzalishaji zaidi ya hapo kwa niaba yake jambo ambalo si kawaida kwa Rais wa Marekani ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipinga Opec.

Bwana Trump alisema Washington itasaidia Mexico lakini hakutoa maelezo ya kina kuhusu mpango huo.

"Sasa imejitokeza kwamba Mexico inatulizwa kutokana na msimamo wao ili kurejesha hali ya kawaida sokoni, na kusababisha mashaka zaidi kwa ahadi ya Marekani," Bwana Sharma amesema.

"Upunguzaji uzalishaji kwa Urusi na Saudi Arabia kwa mapipa milioni 2.5 kwa siku kutoka kiwango kilichokubalika cha mapipa milioni 11 kwa siku ni changamoto. Kwa kipindi kirefu 2019, Urusi ilionesha kutotimiza kwa kiwango kikubwa makubaliano ya awali ya kupunguza uzalishaji, Kwahiyo kuna uwezekano mkubwa hatua hiyo ikaishia kuwa tangazo tu sokoni."

Aliongeza kwamba kutabiri kupungua kwa hitaji kipindi kijacho ni jambo linaweza kutokea hata kufikia kupunguzwa kwa mapima milioni 18.5 kwa siku.