Virusi vya corona: Tanzania Bara yathibitisha wagonjwa 14, Zanzibar watatu

Waziri wa Afya wa Tanzania
Maelezo ya picha,

Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu

Mamlaka za Afya nchini Tanzania zimetangaza wagonjwa wapya 17 wa virusi cya corona nchini humo.

Waziri wa Afya wa Tanzania Bi Ummy Mwalimu ametangaza maambukizi mapya 14 kwa upande wa Bara huku Waziri wa Afya wa Zanzibar Bw Hamad Rashid akitangaza maambukizi mapya matatu visiwani humo.

Wagonjwa wote hao 17 ni raia wa Tanzania.

Kwa upande wa wagonjwa 14 wa Tanzania Bara, 13 wamegundulika Dar es Salaam na mmoja Arusha.

Kufikia sasa watu 49 wameambukizwa virusi vya corona.

Watu 13 kati ya walioambukizwa virusi vya corona wapo jijini Dar es Salaam huku na mwingine mmoja kutokea mjini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Ummy wagonjwa wote wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya.

''Ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu nao unaendelea'' ilisema taarifa hiyo.

Maelezo ya video,

Virusi vya Corona: Jinsi marufuku ya misongamano inavyokumbana na vikwazo Afrika

Kwa upande wa Zanzibar, waziri Hamad ameonya dhidi ya hatari ya kusambaa kwa maambukizi ya ndani.

"Wagonjwa wote hawa hawana historia ya kusafiri nje ya nchi katika siku za hivi karibuni. Hii inathibitisha kwamba maradhi haya sasa tayari yamo kwenye jamii yetu na hivyo kuongeza hatari ya kuambukizana wenyewe kwa wenyeweendapo tahadhari za ziada hazitachukuliwa," imeeleza taarifa yake.

"Wito wangu kwa wananchi ni kwamba, hali ya maambukizo ya maradhi haya hapa nchini ni tete kwani hatujui wangapi kati yetu wameambukizwa. Hatuna budi kila mmoja wetu achukue tahadhari za ziada kuhakikisha tunakatisha mnyororo huu wa maambukizo."

Maeneo ambayo ugonjwa huo umeripotiwa nchini Tanzania ni Dar es Salaam (wagonjwa 32), Zanzibar (12), Arusha (3), Kagera (1) na Mwanza (1).

Hapo jana mamlaka nchini Tanzania zilitangaza marufuku ya ndege za abiria kutua nchini humo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa siku ya Jumapili na mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo (TCAA) ndege za mizigo pekee ndizo ambazo zitaruhusiwa kutua.

"Rubani na wahudumu wa ndege hizo watatakiwa kukaa kwenye karantini katika maeneo yaliyotengwa na serikali kwa gharama zao binafsi," ilisema tangazo hilo.

Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Tanzania inakosolewa na baadhi ya wachambuzi na vyombo vya habari vya kimataifa.

Msimamo wa rais John Magufuli wa kuruhusu sehemu za ibada kuwa wazi pia unakosolewa vikali katika kipindi hiki ambacho mataifa mengi yametangaza marufuku ya mikusanyiko ikiwemo katika sehemu za ibada.