Virusi vya Corona: Kwanini Magufuli awataka Watanzania kumuomba Mungu?

Asilimia 60 ya ufadhili wa kifedha wa bajeti ya Zanzibar unatoka katika sekta ya utalii.
Maelezo ya picha,

Asilimia 60 ya ufadhili wa kifedha wa bajeti ya Zanzibar unatoka katika sekta ya utalii.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amewaomba raia wa taifa hilo kutumia siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2020, kumuomba Mwenyezi Mungu ili kuwaepusha na janga la ugonjwa wa corona.

Katika chapisho lake la mtandao wa Twitter Magufuli amewataka raia wa taifa hilo kusali na kwa imani yake Mungu atawasikia

Zanzibar yathibitisha wagonjwa sita wa corona

Wakati huohuo wagonjwa wengine sita wa virusi vya corona wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo kisiwani Zanzibar.

Hatua hiyo inafanya idadi ya wagonjwa wa virusi hivyo kupanda kutoka watu 18 hadi 24.

Waziri wa Afya kisiwani Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amesema kwamba wagonjwa wote waliopatikana na maambukizi ya virusi vya corona ni raia wa Tanzania na hawana historia ya kusafiri .

Waziri huyo ameongezea kwamba tayari wagonjwa wote wamelazwa katika vituo maalum kwa lengo la kuendelea kupata matibabu.

Serikali ya kisiwa hicho imeendelea kuwasisitizia wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo zinazotolewa mara kwa mara ikiwemo kunawa mikono.

Wizara ya Afya kisiwani vilevile imewaomba wananchi wenye dalili za homa kali , kukohowa na kupiga chafya kujitokeaza katika vituo vya Afya.

Aidha raia kisiwani humo wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wanapowazika watu waliofariki kutokana na virusi hivyo ili kuzuia maambukizi zaidi.

Tangazo hilo linajiri saa 24 baada ya taifa la tanzania kutangaza wagonjwa 29 wapya wa virusi hivyo nchini humo.

Akithibitisha hilo waziri wa Afya Ummi Mwalimu alisema kwamba wagonjwa 26 kati yao wapo katika mji wa Dar es Salaam huko wawili wakipatikana mjini Mwanza na mmoja akiwa katika eneo la Kilimanjaro.

Hatahivyo waziri huyo pia alitangaza habari njema akisema kwamba hadi kufikia Jumatano takriban watu 11 walikuwa wameshapona virusi hivyo lakini akaongezea kwamba watu wanne walifariki.

Ongezeko hilo la wagonjwa linajumlisha wagonjwa wapya sita waliotangazwa na waziri wa Afya wa kisiwa cha Zanzibar.

Dar es Salaam yabuni vituo vya kukusanya sambuli za corona.

Chanzo cha picha, AFP

Dar es Salaam yabuni vituo vya kukusanya sambuli za corona

Wakati huohuo vita dhidi ya maambukizi ya corona vimeimarishwa baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutangaza vituo vya Afya na hospitali ambapo wakaazi watepeleka sampuli zao za ili kupimwa virusi vya corona.

Mkuu huyo anasema kwamba lengo la vituo hiyo ni kuzuia maabukizi ya virusi hivyo hususan wakati huu ambapo kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa.

Makonda amesema kwamba hatua hiyo inajiri baada ya wakaazi walio na dalili za virusi kuingia katika vituo vya Afya na kujichanganya na wengine bila kujua.

Baadhi ya vituo vilivyochanguliwa katika wilaya ya Kinondoni ni Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Afya cha Mgomeni, Kituo cha Afya cha Mikoroshoni, kliniki ya IST Masaki, Hospitali ya TMJ Mikocheni pamoja na Hospitali ya Rabininsia eneo la Wazo.

Katika Wilaya ya Ilala vituo hivyo ni Hospitali kuu ya Amana , Hospitali ya Mnazi mmoja, Hospitali ya Buguruni, Hospitali ya Regency, Hospitali kuu ya Muhimbili, Hospitali ya Aga Khan, na Hospitali ya Hindu Mandal.

Katika Wilaya ya Temeke, wakaazi watapeleka sampuli zao katika hospitali kuu ya Temeke.

Mbagala Hospitali ya Rangi Tatu. Kituo cha Afya cha Yombo, na Hospitali ya TOHS Chan'ombe.

Wilaya ya Ubungo wakaazi wametakiwa kwenda katika hospitali ya Sinza , Kituo cha afya cha Kimara, Hospitali ya Bochi na hospitali maalum ya Mloganzila.

Nao wakaazi wa Wilaya ya Kigamboni watapeleka sampuli zao katika kituo cha Afya cha Vijibweni, Hospitali ya Aga Khan na kituo cha Afya cha Kigamboni